Mapato vituo vya makumbusho ya taifa yaendelea kupaa Tanzania

August 3, 2023 9:12 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yameongezeka kwa asilimia 53.9.
  • Utalii wa ndani wachangia kupaa kwa mapato hayo.
  • Serikali yajipanga kufanya maboresho zaidi ya vituo hivyo.

Dar es Salaam. Mapato yatokanayo na utalii wa vituo vya makumbusho ya Taifa yameongezeka hadi kufikia Sh 687.6 milioni, kwa mwaka 2022/2023  huku idadi ya watalii wa ndani ikichangia ongezeko hilo.

Tangu mwaka 2021 Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikiripoti ongezeko la mapato yatokanayo na vivutio hivyo ambapo mwaka 2020/21 ilikusanya Sh338.2 milioni na hadi Aprili mwaka 2021/22 ilikusanya Sh443.2 milioni.

Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022 kinachotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mapato hayo yameongezeka kwa asilimia 53.9 kutoka Sh446.6 milioni hadi 687.6 milioni.

Ofisi hiyo inaeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali kutangaza na kuboresha vivutio vya Mwalimu Nyerere kilichopo Butiama, Maji Maji (Songea) pamoja na kijiji cha Makumbusho kilichopo Dar es Salaam

Mbali na Jitihada hizo, kuongezeka kwa idadi ya watalii hususani watalii wa ndani kumechangia kupaisha mapato hayo zaidi.

Kijiji cha Makumbusho ni mojawapo ya kivutio maarufu cha utalii chenye zaidi ya nyumba 30 za asili ambazo ni somo kwa utamaduni wa Tanzania. Picha| 7 Toucans.

Mwaka 2022/2023 kulikuwa na jumla ya watalii milioni 1.09 waliotembelea vituo vya makumbusho ya Taifa ambapo kati ya hao milioni 1.08 ni watalii wa ndani  na 11,383 watalii wa nje.

Idadi hiyo ni sawa na kusema asilimia 98 ya watalii wote waliotembelea makumbusho ya Taifa kwa mwaka 2022/2023 walitoka ndani ya nchi ya Tanzania.

Hiyo inamaanisha kwa kila watalii 10 waliotembelea vivutio vya makumbusho ya taifa watalii tisa walikuwa Watanzania au katika watalii 100, 98 kati yao ni Watanzania waishio nchini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,vituo vya makumbusho ya Taifa vilichochangia kupaa kwa mapato hayo ni pamoja na nyumba ya utamaduni na  kijiji cha makumbusho vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Vingine ni Azimio la Arusha na Elimu ya Viumbe vilivyopo mkoani Arusha, Vita vya Maji Maji na kituo cha Dk Rashid Kawawa (Ruvuma), Mji Mkongwe Mikindani (Mtwara) pamoja na Mwalimu J.K Nyerere kilichopo Butiama mkoani Mara.


Zinazohusiana


Elimu kwa wananchi yachangia

Kwa upande wake Afisa Uhusiano kutoka makumbusho ya Taifa Joyce Mkinga amesema kuongezeka kwa watalii wa ndani kunamaanisha kuongezeka kwa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutembelea makumbusho hizo.

“Inamaanisha kuwa watu wameanza kufahamu kuwa kuna makumbusho ambayo wanaweza kutembelea…suala lingine ni kuongezeka kwa mapato japo viingilio ni vidogo mtoto ni Sh10,000 na mkubwa Sh2500,” amesema Mkinga.

Ili kuendelea kushuhudia ongezekpo hilo la watalii Mkinga amesema ni  vyema kuendelea kuelimisha kuhamasisha watanzania kutembelea makumbusho hususani kwa vijana ili kujifunza utamaduni na historia ya Tanzania.

“Hiki ni kizazi kipya unapoongelea Mwalimu (Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere) hawajawahi kumuona… tunahitaji kuelimisha zaidi wanafunzi wa shule ya msingi hata watanzania juu ya historia ya Tanzania,”ameongeza.

Mbali na elimu inayoendelea kutolewa, makumbusho hiyo hutumia vyombo vya habari, matamasha ya muziki wa asili, maonyesho ya kitaifa pamoja na mbio ndefu (marathon) kama njia ya kutangaza vivutio hivyo zaidi.

Ukitembelea makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam utapata historia ya wanyama wakubwa walio wahi kutokea Tanzania(Tanganyika) akiwemo Dinosaur.Picha|Esau Ng’umbi.

Serikali yaahidi kuboresha utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Nchnegerwa aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2023/2024 amesema Serikali imejipanga vyema kuboresha shughuli za utalii nchini ikiwemo kuanzisha huduma za kutangaza utalii kidigitali.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara itatekeleza majukumu yake kwa

kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama ifuatavyo…kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili, malikale na makumbusho na kuyatangaza kidijitali,” amesema Nchengerwa.

Enable Notifications OK No thanks