Rais Samia aagiza matumizi namba moja ya utambulisho Tanzania
- Rais Samia asema utaratibu huo utarahisisha upatikanaji wa huduma.
- Roboti lawa kivutio uzinduzi wa 5G ya Airtel
- Matumizi hayo yatapunguza ulazima wa kubeba taarifa nyingi wakati wa kujisajili kupata huduma.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza kuanzishwa kwa mfumo utakaowezesha matumizi ya namba ya moja ya utambulisho katika huduma mbalimbali zinazotolewa nchini, hatua itakayowaokoa mamilioni ya Watanzania na adha ya kusaka vitambulisho lukuki kutoka katika taasisi za umma.
Kwa sasa Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ana zaidi ya vitambulisho vinne tofauti vyenye namba tofauti kikiwemo kitambulisho cha Taifa (NIDA), namba ya mlipa kodi (TIN), pasi ya kusafiria, kitambulisho cha mpiga kura na leseni ya udereva kwa wanaoendesha vyombo vya moto.
Kila kitambulisho kati ya hivyo kina na namba yake na kinatolewa na taasisi husika jambo linalowafanya wahitaji kutumia muda mwingi na fedha kuvisaka.
Rais Samia ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa baharini iliyofanyika leo Agosti 9, 2023 Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na kuzitaka wizara husika kutekeleza kwa wakati ili kuepusha ulazima wa kuwa na vitambulisho vingi vyenye taarifa kinzani.
“Kila Mtanzania ahakikishe taarifa alizozitoa NIDA ni sahihi, kama sio sahihi arekebishe ili tumtambue kwa taarifa alizozitoa…nitoe wito huo kwa taasisi zote zinazotoa huduma kwa Watanzania kutumia namba moja ya NIDA,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:
- Mtandao wa 5G wazinduliwa kwa mara ya kwanza Tanzania
-
Dar es Salaam kinara matumizi huduma za simu Tanzania
Hivi karibuni kumekuwa na uhitaji mkubwa wa vitambulisho vya Taifa ili kuweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo maombi ya kazi, pasi za kusafiria na usajili wa baadhi ya huduma kama laini za simu na huduma za afya.
Licha ya mahitaji hayo makubwa ya kitambulisho cha Taifa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni alieleza Mei mwaka huu kuwa Watanzania milioni 23.9 tu ndio waliosajiliwa na mamlaka ya vitambulisho vya Taifa.
Masauni aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka 2023 aliwaambia wabunge kuwa kwa kipindi cha Julai 2022 na Mei 2023 Watanzania 774,594 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ndio waliosajiliwa.
Pamoja na maagizo hayo Rais Samia ameitaka NIDA kuandaa mfumo utakaokusanya mahali pamoja taarifa zote za Mtanzania kuanzia anazaliwa mpaka anakuwa mtu mzima.
“NIDA wana namba wanazotoa kwa Watanzania, akizaliwa leo aingizwe kwenye mtandao na taarifa zake tunaanza kuzikusanya…ili taasisi nyingine zichukue hizo taarifa na kuzifanyia kazi,” amesema kiongozi huyo wa juu wa nchi wakati akizindua mtandao wenye kasi ya 5G kutoka kampuni ya mawasiliano Airtel utakaowawezesha watanzania kupata huduma ya intaneti kwa kasi zaidi.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa amevaa Kifaa Maalum kijulikanacho kama Teknolojia Ukweli Halisi (Virtual Reality Device) mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mkongo wa Mawasiliano Baharini cha Kampuni ya Airtel. Picha|Ikulu/Twitter.
Roboti lawa kivutio
Uzinduzi huo uliovuta hisia za wengi kwa kushirikisha roboti katika hafla hiyo, pia imetengeneza mwanzo mzuri wa Tanzania kuunganishwa na mataifa mengine ya Asia na Ulaya mara baada ya kukamilika kwa mkongo wa mawasiliano wa baharini utakaowekwa na Airtel 2Afrika.
Roboti hilo refu lilikuwa kivutio kwa wahudhuriaji wa hafla hiyo baada ya kubeba nembo ya 5G na kisha kutembea kwa mbwembwe kwenda kupeleka nembo hiyo kwenye jukwaa kuu na kutokomea.
Airtel inakuwa kampuni ya tatu ya mawasiliano Tanzania kutoa huduma za intaneti ya kasi ya 5G baada ya Vodacom kuzindua huduma hiyo Septemba 2022 na Tigo mapema mwaka huu.
Kasi ya mtandao ya 5G inasaidia kuongeza ufanisi katika mawasiliano katika sekta ya viwanda, afya, elimu, habari na burudani.
Latest



