Nini hatma ya wakazi wa mikoa 10 maskini zaidi Tanzania?

October 12, 2023 10:23 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Simiyu, Kagera na Singida.
  • Wakuu wa mikoa wapata kigugumizi kubainisha mikakati ya kuchechemua uchumi.
  • Wachambuzi wasema ni kutokana na kukosa dira makini ya uchumi.

Dar es Salaam. Licha ya pato la Taifa kuongezeka kwa asilimia 4.7 na kufikia Sh141.8 trilioni mwaka 2022, ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja katika baadhi ya mikoa nchini bado kizungumti jambo linalowafanya baadhi ya Watanzania kuendelea kuishi katika lindi la umaskini.

Kitabu cha takwimu za msingi za Tanzania kwa mwaka 2022 (Tanzania in Figures ) , kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kinaonesha kuwa wastani wa pato la mtu kwa mwaka katika mikoa 15 nchini bado upo chini ya wastani wa pato la mtu mmoja kitaifa ambalo ni Sh2.8 milioni.

Uchambuzi zaidi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa katika baadhi ya mikoa pato la mtu mmoja mmoja liko chini mara mbili zaidi ya wastani wa Taifa wakati baadhi imebakisha senti kadhaa kuufikia wastani huo.

Wastani wa pato la mtu mmoja mmoja hutokana na kugawa jumla ya pato ghafi katika eneo husika na idadi ya watu waliopo sehemu hiyo kwa kipindi fulani.

Ifuatayo ni orodha ya mikoa ambayo wakazi wake wana kipato kilicho chini ya wastani wa pato la taifa ambalo linatajwa kuwa kwenye pato la uchumi wa kati wa chini kwa mujibu wa viwango vya Benki ya Dunia (WB). 


Soma zaidi : Bei ya maharage, mchele haishikiki Singida


10. Rukwa 

Licha ya kuwepo katika orodha ya mikoa inayozalisha kwa wingi mazao ya chakula nchini Tanzania, Rukwa ni miongoni mwa mikoa masikini nchini ambapo kila mwananchi katika mkoa huo anakadiriwa kuwa na kipato cha Sh2.3 milioni kwa mwaka ambacho kipo chini ya wastani wa pato la Taifa.

Katika Ripoti ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18 iliyotolewa na NBS, Rukwa ulitajwa kama mkoa wenye kiwango kikubwa zaidi cha umasikini  wa mahitaji ya msingi ukiwa na asilimia 45.

Hii ina maana kuwa kaya 45 kati ya 100 zilizopo mkoani Rukwa zilikuwa na mahitaji ya msingi.

Nje na ardhi yenye rutuba inayowezesha shughuli za kilimo kufanyika mkoani humo, Rukwa ina utajiri wa vyanzo vya maji ikiwemo Ziwa Tanganyika ambapo shughuli za uvuvi na usafirishaji hufanyika. 

Fursa nyingine za kiuchumi zilizopo mkoani humo ni pamoja na utalii, madini, ufugaji pamoja na viwanda ambavyo vingeweza kutumika kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na kuchangia kuwaondoa kwenye lindi la umaskini. 

9. Songwe

Pamoja na pato la mtu mmoja mmoja kuongezeka kutoka Sh2.1 milioni mwaka 2021 hadi Sh2.2 bado Mkoa wa Songwe umeendelea kusalia katika orodha ya mikoa masikini zaidi nchini Tanzania kwa kigezo hicho cha kiuchumi.

Takwimu za NBS zinaonesha kiwango kilichoongezeka kwa mwaka kutoka 2021 hadi 2022 ni Sh 134,321 pekee.

Hata hivyo, Songwe si mkoa mkongwe sana, ulianzishwa mwaka 2016 kwa kumegwa baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mbeya na kwa mujibu wa Sensa ya  mwaka 2022 mkoa huo una wakazi takriban 1.3 milioni.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Happynes Seneda ameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa mikakati iliyopo ni pamoja na kuanza kuuza bidhaa zilizochakatwa kuliko malighafi jambo litakalochechemua uchumi wa mkoa huo.

“Uongezaji wa thamani kwa bidhaa zinazozalishwa Songwe unafanyika kwenye mikoa mingine badala ya hapa, kiuchumi tunapoteza mapato,” amesema Seneda.

Kwa mujibu wa Seneda, kuanza rasmi kwa shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika mkoa huo kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Songwe na kwa wakazi wa eneo hilo.


Soma zaidi : Zifahamu kozi sita zitazopewa kipaumbele mkopo wa HESLB ngazi ya Diploma 2023 – 24


8. Katavi

Ikiwa imepita miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, Mkoa wa Katavi wenye kilomita za mraba 47,527 bado ni miongoni mwa mikoa 10 masikini zaidi sawa na dada yake Rukwa.

Pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka 2022 lilikuwa Sh1.9 milioni, ambalo ni la chini kwa wastani wa pato la Taifa kwa asilimia 29.

Hata hivyo, Katavi ndio mkoa wenye baadhi ya huduma chache zaidi za kijamii nchini ikiwemo shule na vituo vya afya ambapo ina jumla ya shule 328 pamoja na vituo 134 vya kutolea huduma za afya, kiwango cha chini ikilinganishwa na baadhi ya mikoa mingine yenye idadi sawa ya watu.

Uchambuzi zaidi wa kitakwimu wa Nukta Habari umebaini kuwa idadi ya shule zilizopo mkoa wa Tanga ni mara nne ya shule zilizopo mkoani Katavi huku idadi ya vituo vya afya vilivyopo Dar es Salaam ni mara tano ya vile vilivyopo mkoani humo.

7. Kigoma

Mkoa huu unasifika kwa kuwa na ardhi yenye rutuba ya kutosha, uoto wa asili na hali ya hewa ya kuvutia, pamoja na Ziwa Tanganyika. Aidha, unatajwa pia kuwa ni miongoni mwa mikoa yenye  bionuai adimu yenye kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi. 

Kwa hivyo shughuli za uchumi kama utalii, kilimo na uvuvi zinafanyika kwa wingi katika mkoa huo.

Hata hivyo, mkoa huu bado haujafanikiwa kuondoka kwenye orodha ya mikoa yenye kipato cha chini kwa kuwa wastani wa pato la wakazi wa mkoa huo ni Sh1.9 milioni kwa mwaka.

6. Tabora

Huu ndio mkoa mkubwa zaidi nchini Tanzania ukiwa na kilomita za mraba 76,151 pamoja na wakazi zaidi ya milioni 3.3. Ukubwa wa mkoa wa Tabora ni mara 54 ya mkoa wa Dar es Salaam.

Pamoja na kwamba ni miongoni mwa mikoa yenye zaidi ya watu wengi zaidi nchini kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, pato la Sh1.8 milioni kwa mwaka kwa wakazi wa mkoa huo umeufanya ushike nafasi ya sita kwenye orodha ya mikoa masikini zaidi nchini Tanzania.

Tabora ni maarufu zaidi kwa kilimo cha mazao ya biashara kama tumbaku, pamba, alizeti pamoja na chikichi ambayo kama yakitumiwa vyema yanaweza kuinua uchumi wa mkoa huo.

Aidha, uzalishaji wa mazao ya nyuki kama asali na nta unafanyika kwa wingi katika mkoa huo maarufu kwa kuwa na kuku wengi wa kienyeji.


Soma zaidi : Unayopaswa kufahamu kuhusu mikopo ya HESLB ngazi ya Diploma 2023 – 24


5. Dodoma

Umaarufu wa mkoa huu hautokani tu na zabibu zake tamu ambazo hutumika kutengeneza aina mbalimbali za mvinyo bali kuhamishiwa kwa shughuli za Serikali kwa kuufanya kuwa makao makuu ya nchi kumeuongezea hadhi na umaarufu zaidi.

Idadi ya watu kwenye mkoa huu uliopo katikati mwa Tanzania si ya kutia shaka, kwani mpaka mwaka 2022 walikuwa na zaidi ya wakazi milioni 3 ambao wastan wa kipato chao kwa mwaka mzima ni Sh1.7 milioni ambacho bado ni cha chini ya wastani wa pato la taifa kwa zaidi ya nusu.

Uchambuzi wa takwimu hizo za NBS unaonesha kuwa ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja uliporomoka kwa asilimia 2.4 mwaka 2022 ukilinganisha na ule wa 2021 ambao ulipanda kiduchu kutoka mwaka 2020.

Huenda ujenzi wa miradi mikubwa ya Serikali kama barabara, miradi ya kilimo, pamoja na reli ya kisasa ikachechemua ukuaji wa uchumi wa wakazi wa mkoa huo jambo litakaloinua pato lao.

4. Pwani

Huu ndio mkoa ambao kasi ya ukuaji wa wastani wa pato la wakazi wake umeporomoka kwa kiwango kikubwa kuliko mikoa yote nchini ambapo takwimu za NBS zinaonesha ukuaji umeshuka kwa asilimia 26.

Mwaka 2021 wastani wa pato la mtu mmoja katika mkoa huo ulikuwa ni Sh2.3 milioni na mwaka 2022 ulishuka hadi Sh1.6 milioni.

Hata hivyo, huenda kasi ya ongezeko la watu katika mkoa huo wa kiviwanda ikawa ni miongoni mwa sababu ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, kasi ya ongezeko la watu mkoani Pwani mwaka 2022 iliongezeka na kufikia 6.1 kutoka ukuaji wa 2.2 mwaka 2012.

Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kumeifanya Pwani kuwa miongoni mwa mikoa masikini zaidi licha ya kusifika kwa uwepo wa fursa lukuki za kiuchumi ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo, ufugaji pamoja na bandari kavu.

3. Singida 

Taarifa rasmi zinabainisha kwamba huu ni miongoni mwa mikoa kongwe nchini Tanzania ukiwa na umri wa miaka 60 hivi sasa kwa kuwa ulianzishwa miaka miwili tu baada ya uhuru wa Tanganyika.

Pamoja na ukongwe wake, wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka katika mkoa huo bado umekuwa chini ya wastani kwa miaka mitano mfululizo huku ukuaji wa pato ukipanda na kushuka kwa nyakati tofauti.

Mwaka 2022 wakazi wa mkoa wa Singida unaosifika kwa uzalishaji wa alizeti kwa wingi walikuwa na pato la Sh1.5 milioni ambalo nalo limeshuka kutoka 1.6 milioni iliyoripotiwa mwaka 2021.

2. Kagera

Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mitano mfululizo kipato cha wakazi wa Kagera kwa mwaka kimefikia Sh1.4 milioni ukiwa ni ukuaji wa asilimia 18 kulinganisha na ule wa asilimia 3 wa mwaka 2021.

Ukuaji huo umeiwezesha Kagera yenye zaidi ya wakazi milioni 2.9 kupanda kutoka nafasi ya kwanza iliyokuwa inaushikilia mwaka 2021 na kuwa ndio mkoa maskini zaidi Tanzania.

Kagera ina ukwasi wa vyanzo vya shughuli za uchumi ikiwemo ziwa Victoria wka uvuvi, vivutio vya utalii, ufugaji pamoja na hali ya hewa nzuri kwa shughuli za kilimo ambapo miongoni mwa mazao yanayostawi zaidi ni kahawa pamoja na ndizi.

Nukta Habari ilifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa ili kufahamu mikakati ya kuinua uchumi na pato la wakazi wa mkoa huo ambapo aliahidi kuzungumza baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka NBS Agosti 30 saa nane mchana mwaka huu, ingawa hakupokea tena simu alipopigiwa baadaye.

1.Simiyu

Simiyu ni miongoni mwa mikoa mipya iliyoanzishwa mwaka 2012, ambapo maeneo ya mikoa ya Shinyanga pamoja na Mwanza yalimegwa ili kuupata mkoa huu ambao kwa sasa una zaidi ya wakazi 2.1 milioni.

Kama Kagera, nao kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mitano ndio umefikia wastani wa pato la Sh1.4 milioni kwa mwaka ambalo kwa mujibu wa takwimu za NBS ndio mkoa masikini zaidi kwa mwaka 2022 ukichukua nafasi ya Kagera ambayo sasa ni ya pili.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18 iliyotolewa na NBS Simiyu ilitajwa kwenye orodha ya mikoa yenye kiwango kikubwa cha umasikini wa mahitaji ya msingi ukiwa na asilimia 39.2.

Tovuti ya Mkoa huo inabainisha kuwa Simiyu ina eneo lenye kilomita za mraba 11,479 linalofaa kwa shughuli za kilimo na ufugaji.

Eneo hilo ni kubwa mara 10 zaidi ya mkoa wa Dar es Salaam ambalo lingeweza kutumika kuzalisha mazao ya biashara pamoja na chakula na kuukwamua mkoa huo kutoka kwenye lindi la umaskini.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda alionekana kutokukubaliana na takwimu za NBS kuwa mkoa wake ulikuwa na watu masikini zaidi Tanzania kwa kigezo cha pato la mtu mmoja mmoja akidai kuwa pato la mkoa huo lilikuwa likihesabiwa katika mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Nukta Habari ilifanya jitihada za kumtumia takwimu rasmi zilizopo kwenye kitabu cha hali ya uchumi mwaka 2022, na kumuomba aelezee mipango ya Serikali kuinua uchumi wa wakazi wa mkoa huo na tarehe 30 Agosti alitoa ahadi ya kuzungumza baadaye ambapo hapokea tena simu.

Wachambuzi wanena

Fredy Oddo ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Tanzania, ameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa sababu inayofanya baadhi ya mikoa kuwa na kipato cha chini ni kutokuwepo kwa mikakati ya kutumia vyema rasilimali zilizopo maeneo hayo.

“Sera na vipaumbele vya Taifa vinasema nini kuhusu hilo, mathalani ukanda wa Ziwa Victoria kulipaswa kuwe na viwanda vya kusindika samaki, kisha sisi ndio tuuze nje, badala yake wageni ndio wanaonekana wanaongeza thamani wakati kitu pekee kinachofanyika ni kutoa minofu na kuwagandisha,” amesema Oddo.

Oddo ameongeza kuwa kukosa mikakati ya kuongeza thamani malighafi zitokanazo na rasilimali zilizopo nchini kunafanya wakazi wa mikoa hiyo kuendelea kutofaidika na rasilimali hizo kwani huuza kwa bei ya chini.

Kwa mujibu wa Oddo, ili kuondokana na kadhia hiyo ni muhimu kwanza kubadili fikra za Watanzania kwa kuwashibisha maarifa ya namna ya kusimamia na kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo katika maeneo yao huku Serikali ikianzisha na kutekeleza mikakati ya uendelezaji wa rasilimali.

Hata hivyo, tayari hatua kadhaa zimeshaanza kuchukuliwa na Serikali ikiwemo kubadili mitaala ya elimu ambayo sasa imejumuisha elimu ya amali na mafunzo stadi ili kuwawezesha wahitimu kuwa na maarifa hitajika katika jamii husika.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks