Ufaulu waongezeka kiduchu matokeo kidato cha pili, darasa la nne 2023
- Ufaulu ulioongezeka ni chini ya asilimia moja.
- Wasichana wafanya vizuri matokeo darasa la nne huku wavulana wakifanya vizuri kidato cha pili.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) pamoja na matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) leo Jumapili Desemba 7, 2023 ambapo ufaulu umeongezeka kiduchu kwa ngazi zote mbili.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam amesema ufaulu wa jumla kwa matokeo ya SFNA umeongezeka kutoka asilimia 82.95 ya waliofaulu mwaka jana hadi 83.39 mwaka 2023.
“kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 0.39 kwa wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea na darasa la tano ikilinganishwa na mwaka 2022,” amesema Dk. Mohamed.
Bofya hapa kuona matokeo kidato cha pili
Jumla ya watahiniwa milioni 1.6 wa darasa la nne wakiwemo wasichana 864,482 sawa na asilimia 51.05 walisajiliwa kufanya mtihani wa Taifa uliofanyika Novemba 2023, ambapo wanafunzi 147,837 sawa na asilimia nane ya waliosajiliwa hawakufanya mtihani huo.
Kati ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na darasa la tano,wasichana ni 681,259 sawa na asilimia 84.79 na wavulana ni 606,675 sawa na asilimia 81.78 ambapo takwimu zinaonesha wasichana wamefaulu vizuri ikilinganishwa na wavulana.
Bofya hapa kuona matokeo darasa la nne
Wakati wastani wa ufaulu ukiongezeka kwa chini ya asilimia moja kwa matokeo ya darasa la nne 2023, hali inafanana na matokeo ya upimaji wa FTNA ambapo ufaulu umeongezeka kwa 0.13.
Kwa mujibu wa Dk.Mohamed wanafunzi 592,741 kati ya 694,769 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 85.31 wamefaulu ambapo wamepata Madaraja ya I, II, III na IV.
“Kati ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na Kidato cha Tatu, Wasichana ni 314,949 sawa na asilimia 83.66 na Wavulana ni 277,792 sawa na asilimia 87.28,” amebainisha Dk. Mohamed.
Aidha, wakati wasichana wakifanya vizuri zaidi kwenye matokeo ya darasa la nne, wavulana wameibuka vinara katika matokeo ya kidato cha pili ambapo wakwimu zinaonesha wavulana wamefaulu kwa asilimia 87.28 wakiwaacha nyuma wasichana kwa asilimia nne.
Latest



