Mpango kumwakilisha Rais Samia Uswisi
- Ni Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani utakaofanyika kwa siku 5.
- Unahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje lya Bara la Afrika.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk.Isdor Mpango anatarajiwa kumuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) utakaofanyika kwa siku tano Davos nchini Uswisi.
Hii ni mara ya 54 kwa mkutano huo kufanyika Duniani huku ajenda kuu zikiwa ni kujenga upya uaminifu, kukuza ajira, akili bandia, nishati, mazingira, ulinzi na ushirikiano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Franco Singaile Msaidizi wa Makamu wa Rais, leo Januari 14, 2024 Dk.Mpango tayari ameshawasili nchini Uswisi kwa ajili ya mkutano huo utakaofanyika kuanzia Januari 15 hadi 19 ambapo pia anatarajiwa kuhudhuria mikutano mingine ukiwemo wa uchumi na uwekezaji.
“Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais atahudhuria mikutano mbalimbali inayohusu masuala ya uchumi na uwekezaji, utawala bora, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kilimo,” inasema taarifa ya Singaile.
Aidha, Mpango atafanya mazungumzo ya na viongozi wa mataifa na mashirika mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.
Mkutano huo unahudhuriwa na wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, watendaji wakuu wa mashirika ya Kimataifa, wakuu wa taasisi na makampuni mbalimbali duniani pamoja na wafanyabiashara.
Miongoni wa wahudhuriaji hao wapo viongozi kutoka Bara la Afrika akiwemo Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Nigeria Bola Tinubu huku António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) akitarajiwa kushiriki mkutano huo.
Latest