Tanzania yatangaza riba ya benki kuu ya asilimia 5.5 ikianza sera mpya ya fedha
- Gavana wa BoT aeleza kuwa riba hiyo itatumika baina ya benki hiyo na benki za biashara na taasisi nyingine za kifedha.
- Riba za huduma za benki za biashara zitaendelea kupangwa kwa mujibu wa soko.
Dar es Salaam. Hatimaye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kiwango cha kwanza cha riba cha asilimia 5.5 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024, ikiwa ni mwanzo wa safari ya matumizi ya sera mpya ya fedha ya kutumia riba kudhibiti mfumuko wa bei na kukuza uchumi.
Mapema mwezi huu BoT ilitangaza kuwa itaanza kutumia mfumo mpya wa sera ya fedha wa riba na kuachana na mfumo wa awali uliokuwa unatumia ujazi wa fedha kudhibiti mfumuko wa bei.
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba ameeleza leo Januari 19, 2024 jijini Dar es Salaam kuwa baada ya kufanya tathmini ya kina ya mwenendo wa uchumi na matarajio yake, Kamati ya sera ya fedha (MPC) ya BoT iliamua kupanga kiwango cha riba kuwa asilimia 5.5 kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

“Uamuzi wa kamati ya sera ya fedha katika kupanga riba hii umezingatia mahitaji ya kuthibiti mfumuko wa bei kwa kipindi cha muda wa kati usizidi asilimia 5 wakati ukichagiza ukuaji wa uchumi kufikia lengo la asilimia 5.5 au zaidi mwaka 2024 na kuhakikisha utulivu wa sarafu,” amesema Tutuba wakati akisoma sera ya fedha.
Tutuba ameeleza kuwa kiwango hicho cha riba kilichotangazwa kitatumika katika kufanya biashara baina ya BoT na benki za biashara na taasisi za kifedha na kitatumika kama rejeo kwa taasisi hizo.
Katika mkutano huo uliohusisha watendaji wakuu wa benki za biashara na taasisi nyingine za kifedha na wanahabari, Tutuba amesema anaamini kuwa riba hiyo itaziongoza taasisi za kifedha katika shughuli zao ikiwemo ubainishaji wa riba kwa wateja jambo litakalosaidia utekelezaji wa sera hiyo ya fedha.
— Bank of Tanzania (@BankOfTanzania) January 19, 2024
“Ifahamike kwamba utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia riba ya benki kuu haimaainishi kuwa tunaweka kiwango elekezi au ukomo wa riba kwa huduma zinazotolewa na benki na taasisi za kifedha. Riba kwa ajili ya huduma zinazotolewa na benki na taasisi za kifedha zitaendelea kupangwa kwa mujibu wa soko,” amesema.
Kuanzia kutumika mfumo huo wa sera ya fedha ya riba kunahitimisha safari ya miaka 28 ya BoT kutumia sera ya ujazi wa fedha kudhibiti mfumuko wa bei ambayo miaka ya hivi karibuni imebainika kuwa na mapungufu kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya kutimiza matakwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kwa sasa kutokana na mabadiliko ya teknolojia, ni rahisi fedha kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa watu wengine kwa haraka zaidi kupitia simu za mkononi.
Latest
