Corona: Hatari inayowakabili wavuvi, wafanyabiashara wa samaki

September 2, 2021 1:01 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wapuuzia tahadhari dhidi ya Corona.
  • Baadhi yao wanatumia barakoa kwa dharura tu kuingia sokoni na si kujikinga.
  • Serikali yasema itaendelea kuwaelimisha ili kutokomeza ugonjwa huo. 

Mwanza. Ni majira ya saa 6 mchana katika Soko la samaki la kimataifa la Mwaloni jijini Mwanza, pilika pilika za hapa na pale zikiendelea.

Licha ya uwepo wa Corona, soko hili lina umati mkubwa wa watu wasiojali tahadhari. Wapo wanaonunua, wapo wanaouza na wengine wakiendelea na shughuli za upakiajii wa samaki kwenye magari ili kupeleka katika maeneo ya biashara.

Katika soko hili lililopo kando kabisa ya Ziwa Victoria tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa kujikinga na Corona (Uviko-19) ikiwa ni pamoja na kujenga masinki ya kunawia mikono na jumbe zikiwa zimebandikwa kwenye kuta za jengo kuwakumbusha watu wanaoingia na kutoka kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

Hata hivyo, wanaofuata tahadhari hizo ni wachache huku wengi wao wakiendelea na shughuli zao bila kufahamu wajibu wao wa kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya ugonjwa huo.

Wavuvi na wafanyabiashara waliozungumza na Nukta Habari wanasema wanaendelea kuchukua tahadhari japo si kwa kiwango kinachotakiwa na Serikali.

“Huu ugonjwa umekuwa wa kawaida, hapa kuna vifaa lakini ukienda sehemu nyingine hawachukui tahadhari kwa hiyo hakuna maana yoyote,” anasema John Mlonja akiwa amebeba mzigo wa samaki begani wakati akitoka sokoni hapo bila kuvaa barakoa.

Wafanyabiashara wa dagaa wakiwa katika mwalo wa Mswahili jijini Mwanza. Mwalo huu ni moja ya michache inayofuata taratibu za kukabiliana na Uviko-19 lakini baadhi ya wachuuzi huvua barakoa baada ya kuingia mwaloni. 

Wafanyabiashara katika soko hilo wanasema huchukua tahadhari hasa kuvaa barakoa kwa dharura hasa kama wana safari za kwenda katika ofisi za umma.

“Hatulazimishi watu kuchukua tahadhari licha ya kuweka  sehemu ya kunawia mikono na matangazo ya kuvaa barakoa lakini bado mapokeo ya watu ni madogo,” anasema Mwenyekiti wa soko hilo, Magafu Fikiri.

Mwenyekiti huyo alipoulizwa kuwepo kwa kifaa cha kupimia joto la mwili (thermometer) kwa ajili ya kupimia dalili za awali za ugonjwa huo alisema hakipo na kwamba kila mmoja anachukua tahadhari kwa muda wake.

“Changamoto tunayokutana nayo ni imani waliyojengwa na hayati John Magufuli kuwa wamtegemee Mungu, kila unayemwambia anawe mikono na kuvaa barakoa anasema Rais Magufuli alitueleza kumtegemea Mungu kwenye kila jambo,” anasema Fikiri.

Hali katika soko hilo inafanana na masoko mengine ya kuuzia samaki ya Buhongwa,  Kamanga, Soko Kuu na Ilonganzara mkoani hapa.
a ya viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel kufika katika soko hilo hivi karibuni na kuwahimiza wafanyabiashara kuchukua tahadhari hakuna lililobadilika.


Wengine wazingatia tahadhari lakini…

Wakati wafanyabiashara katika soko la samaki la kimataifa la Mwaloni wakipuuzia tahadhari dhidi ya Uviko-19, wenzao wa mwalo wa Mswahili wamepiga hatua kubwa katika kujikinga na ugonjwa huo. 

Katika mwalo huo kila mtu anayeingia ndani ananawa mikono na kuvaa barakoa.

Mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Mkuyuni ulipo mwalo huo, Nyamhanga Marwa anasema hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia katika mwalo huo maarufu kwa kuuza dagaa na samaki bila kunawa mikono na watu wanazingatia utaratibu uliowekwa na uongozi. 

“Hali imebadilika sana ni tofauti na siku zilizopita na hii ni baada ya  kuenea kwa habari kuwa mkoa wa Mwanza una idadi kubwa ya wagonjwa wa Corona hivyo haturuhusiwi kabisa kuingia ndani ya mwalo huu kama hauna barakoa au kunawa mikono,” anasema Laurencia Mathayo, mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza.

Wachuuzi wa samaki na dagaa katika mwalo wa Mswahili wakiwa wananawa mikono kabla ya kuingia ndani ya mwalo huo. Picha zote|Mariam John/Nukta.

Licha ya watu kusisitiziwa kunawa mikono na kuvaa barakoa wanapoingia katika mwalo huo, lakini baadhi yao wafikapo ndani huzivua barakoa zao na kuendelea na shughuli zao kwa sababu hakuna udhibiti kama ilivyo getini. 

Hali hiyo inazidi kuwaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Uviko-19 kama wenzao wa soko la samaki la kimataifa la Mwaloni.

Tahadhari dhidi ya Corona haitakiwi kufanywa tu sokoni bali hata kwa wanaotembeza samaki na dagaa mtaani ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo unaoitesa dunia kwa sasa.

“Nafanya biashara ya kusambaza dagaa kwenye nyumba za watu, ninapofika hapo nahakikisha nawaomba maji nanawa ndipo naanza kuwahudumia lakini pia huwa ninavaa barakoa wakati wote,” anasema Emiriana John ambaye anaendelea na shughuli za kupembua dagaa ili kuwahi wateja wake mtaani. 

Masoko mengine ya kuuzia samaki ya Buhongwa,  Kamanga, Soko Kuu na Ilonganzara mkoani hapa nayo ni wachache waliofika katika maeneo hayo na kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.

 Wapo waliofika na kunawa kabla ya kuingia sokoni, wapo waliovaa barakoa na wengine walionekana kutojali.

“Ni kweli ugonjwa wa corona upo na tunaambiwa unaua, na sio kwamba hatuchukui tahadhari barakoa tunazo,” anasema  Esta Emmanuel muuzaji wa samaki katika Soko Kuu la Mwanza huku akifungua barakoa aliyokuwa ameifunga  kwenye kitenge na kumwonyesha mwandishi wa habari hii.  

Huenda kuupuzia tahadhari kunaweza kukazidisha maambukizi ya wimbi la tatu la Uviko-19 kwa wavuvi na wafanyabiashara jijini hapa na kuwaweka katika hatari kupata vifo.

Kwa mujibu wa Wizira ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kasi ya maambukizi ya Uviko-19 nchini Tanzania imezidi kuongezeka na hadi Julai 22 watu 858 walikuwa wanaugua ugonjwa huo kutoka watu 408 waliorekodiwa mwanzoni mwa Julai. 

                   

Viongozi kuendelea kutoa elimu

Mjumbe wa ulinzi wa rasilimali za Ziwa Victoria (BMU), Mwajuma Chamliho  anasema wanaendelea kutoe elimu kwa watu wote ili kuongeza mwamko wa kuchukua tahadhari kwa kuwa wengi hawajali. 

“Katika mwalo huu (wa Mswahili) bado hatujapata athari yoyote ya kifo au licha ya kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaoingia hapa lakini bado nia ya Serikali ni njema tutaendelea kuwahamasisha,” anasema Mwajuma.

Hivi karibuni uongozi wa mkoa wa Mwanza ulitangaza kukaza masharti ili kukabiliana na Uviko-19 ikiwemo kusitisha mikusanyiko isiyo ya lazima na kuagiza vifaa vya kunawia mikono viweke katika maeneo ya umma. 

Miongoni mwa hatua ni Mkuu wa Mkoa huo Robert Gabriel  kutembelea mialo na kuagiza mamlaka kusimamia na kuwaongoza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

“Niwaombe viongozi wa wilaya, tarafa na kata kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji kwenye maeneo hayo, mtu anapoenda sokoni hakikisha kuna ndoo za kunawia mikono na amevaa barakoa  ili wakati wanapobadilishana fedha isiwepo namna inayoweza kusababisha maambukizi,” anasema Gabriel.

Makala hii ni sehemu ya mfululizo wa ripoti maalum za kukabiliana na Uviko-19 zinazowezeshwa na Shirika la International Media Support na Umoja wa Ulaya (EU).

 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV