NMB yatakiwa kupunguza mikopo chechefu
- Hatua hiyo itasaidia benki kuepuka hasara.
- Pia yatakiwa kupunguza riba kwa mikopo inayotoa.
Dar es Salaam. Serikali imeitaka benki ya NMB kuongeza jitihada katika kupunguza mikopo chechefu na riba wanazotoza kwa wateja wake ili kupunguza hasara kwa benki na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba ametoa agizo hilo Septemba 3, 2021 alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa benki hiyo ofisini kwake jijini Dodoma.
Amesema suala la mikopo chechefu ni changamoto ya muda mrefu ingawa baadhi ya mikopo hiyo imekuwa ikisababishwa na benki zenyewe.
“Hili la mikopo chechefu inabidi muwe makini sana katika kutathmini utoaji wa mikopo kwa wateja unakuta mteja hana historia nzuri ya masuala ya kibenki halafu mnamkopesha mnadhani nini kitatokea?,” amehoji Tutuba.
Kwa mujibu Taasisi ya Mabenki Tanzania (TIOB), mikopo chechefu (Non-Performing Loans (NPL)) ni takwimu inayotumika kama kiashiria kinachoonyesha uwiano kati ya mikopo isiyolipwa na jumla ya idadi ya mikopo ambayo imetolewa na benki au taasisi ya fedha.
Mikopo hiyo lilianza kujulikana zaidi mwaka 2017 baada ya idadi ya mikopo isiyolipwa kwa wakati kuongezeka.
TIOB inasema mikopo chechefu ni jambo la kawaida kwa taasisi yoyote ya fedha huku taasisi zikitakiwa kuwa na utaratibu ambao utadhibiti mikopo ya aina hii isiwe mingi.
Uhaba wa kitambulisho cha aina moja kwa Watanzania wote umechangia kwa wateja wasio waaminifu kufanikiwa kupotosha taasisi za fedha kuhusu madeni yao mengine wakati wanapoomba mikopo na matokeo yake kusababisha ongezeko kubwa la mikopo chechefu.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao na ujumbe kutoka Benki ya NMB ofisini kwake jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameiagiza benki ya NMB kuongeza jitihada za kupunguza riba za mikopo kwa wateja wao, changamoto ambayo imekuwa ni ya muda mrefu kwa taasisi za fedha nchini.
“Na sisi kama Serikali tunaahidi kuwa tutaendelea kufanya kazi na nyinyi kwa kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kuwezesha sekta hii ya fedha kukua kwa ustawi,” amesema Tutuba.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna ameahidi kuyatendea kazi maagizo yote yaiyotolewa na Serikali na kubainisha kuwa benki hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali wakati wote.
Amesema benki hiyo iko vizuri kwa sasa katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo uwekezaji, uendeshaji, mikopo pamoja na amana ambapo kwa mwaka jana benki hiyo ilipata faida ya Sh206 bilioni baada ya kodi na kutoa gawio la Sh68.5 bilioni kwa wanahisa wote, huku Serikali ikipata gawio la Sh21.8 bilioni.
Latest
