‘Stop’: Ukatili wa kijinsia sokoni ulivyokomeshwa Dar

September 8, 2021 7:58 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni mwa mbinu ni kwa kuwajengea uwezo wanawake kujiamini na kutambua haki zao.
  • Kutumia faini na adhabu kwa wanaotenda vitendo hivyo.
  • Kuongeza idadi ya wanawake kwenye vyombo vya maamuzi.

Dar es Salaam. Akiwa kwenye banda lake, mama wa makamu yupo kwenye heka heka za kufunga na kupanga mboga za matembele kwenye meza kwa ajili ya kuwahudumia wateja wake katika soko la Kinyerezi mkoani Dar es Salaam.

Mama huyo, Stella Mwandri, ni miongoni mwa wanawake waliopo katika soko hilo lilipo katika Manispaa ya Ilala wanaosaka riziki kwa kufanya biashara ya mbogamboga na bidhaa nyingine. 

Katika meza hiyo ambayo wengine wanaweza kuichukulia poa, Stella anapaita ofisini na amepanga mbogamboga mbalimbali zikiwemo matembele, spinachi, mchicha.  

“Ninapata wateja wengi zaidi na biashara yangu inakua,” anasema Stella huku akiendelea na kuchambua mboga ili kuwarahisishia wateja wake mchakato wa kupika.

Furaha aliyonayo mwanamke huyo ni kutokana na uhuru alionao sokoni hapo baada ya kutokomezwa kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia walivyokuwa wakifanyiwa wanawake hapo awali katika masoko mbalimbali mkoani hapa. 

Kutokana na ukatili wa kijinsia kupungua katika masoko ya Halmashauri ta Ilala, wanawake wana uhuru wa kufanya biashara zao bila kipingamizi. Picha| Gift Mijoe.

‘Leo ni bora kuliko jana’

Vitendo hivyo, vilivyokuwa vimeshamiri katika soko hilo na masoko mengine ya mkoa huu, ni pamoja na lugha chafu, vipigo na wanawake kutopata fursa sawa za biashara na uongozi. 

Hata hivyo, kwa sasa ni nadra kushuhudia heshima na utu wa mwanamke ukishushwa. 

“Tulikuwa tunadhalilishwa sana wanawake, ukikuta kijana ameanza kutukana hapo ni matusi tu na mengi yanatudhalilisha sisi wanawake,” anasema Tatu Lazaro, mama lishe katika soko la Kigogo Fresh lililopo Pugu.

Mabadiliko hayo yanayoshuhudiwa sasa ni matunda ya mafunzo yaliyotolewa kwa nyakati tofauti na wadau wa usawa wa kijinsia katika masoko mkoani hapo. 

                   

Shirika lisilokuwa la kiserikali la Equality for Growth (EFG) lilitoa mafunzo kwa wanawake katika masoko 15 ya Dar es Salaam yaliyohusu usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamii ikiwemo kuwapa uwezo kumudu biashara zao.

“EFG imetufundisha sisi kama wanawake kujitambua ndani ya soko, Kwa sasa tukimuona kijana anatukana, tunamuita kama wanawake tunamkanya. Hatutaki matusi sokoni, hapa ni eneo la kazi,” anasema Tatu.

Mafunzo hayo yamewasaidia wanawake kujiamini, kutambua na kuzipambania haki zao. 

Mbali na kupambania haki zao, maarifa hayo yamewafungulia fursa mbalimbali za kibiashara, kiuongozi na kuwaondolea vikwazo vya uchumi vilivyokuwa vinawakabili. 

Afisa Mradi wa Equality for Growth (EfG), Susan Sitta ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa wamekuwa wakitoa elimu hiyo katika masoko tangu mwaka 2011. 

Awali, Susan anaeleza kuwa, utafiti masokoni ulifanywa katika masoko hayo na kubaini kuwa unyanyasaji wa kijinsia ilikuwa katika kiwango cha juu ikiwemo rushwa ya ngono.

“Unyanyasaji wa kijinsia ulikuwa kwa kiwango cha asilimia 97 masokoni. Wanawake walikuwa wakipitia bugdha, matusi, rushwa za ngono na vipigo,” anasema Susan.

Namna walivyotokomeza ukatili wa kijinsia

Licha ya wanawake kujitambua na kutoa elimu kwa jamii hasa sokoni kuhusu usawa wa kijinsia, wamejiwekea utaratibu unaowawezesha kudhibiti vitendo vya ukatili visijirudie tena katika maeneo yao ya biashara.

Tofauti na miaka ya nyuma, wanawake katika masoko mbalimbali mkoani hapa wameingia katika vyombo vya maamuzi kwa kugombea nafasi za uongozi ili kutetea maslahi yao.

Makamu Mwenyekiti wa soko la Kigogo Fresh, Nasra Mgwami ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz)  kuwa uongozi wa soko hilo umefanikiwa kufikia kiwango cha 50 kwa 50.

Anasema awali uwakilishi wa wanawake kwenye uongozi wa soko ulikuwa mdogo na ndiyo ilikuwa chanzo cha wanaume kuwakosea heshima wanawake na kutokuyatilia maanani maslahi yao.

“Kama unavyoniona, Makamu mwenyekiti ni mimi, mwana mama, mweka hazina naye ni mwanamama. Wanawake tumeshikilia nafasi kubwa na wawakilishi ni wengi kwenye uongozi wa soko,” anasema Nasra.

Hali hiyo imesaidia mgawanyo mzuri wa rasilimali za soko ikiwemo maeneo ya kufanyia biashara kwa uwazi na usawa kwa makundi yote mawili.

Watunga sheria ndogo ndogo

Kwa sasa baadhi ya masoko mkoani hapa yamejiwekea kanuni za faini kwa mtu anayefanya udhalilishaji sokoni ikiwemo kutukana matusi kwa wanawake.

“Wanawake walikuwa mwanzoni wananyanyasika asilimia kubwa, tulivyoingia kwenye uongozi, tumelisimamia hilo, sasa hivi watu wanafanya kazi bila kunyanyasika,” anasema Katibu wa Soko la Kigogo Fresh, Athuman Omary.

Faini hizo zimepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo na kuwafanya wanawake wajisikie huru kufanya shughuli zao.

Hata hivyo, kazi bado inatakiwa kuendelea kuwasaidia wanawake masokoni kwa sababu ukatili wa kijinsia haujaisha kabisa na umeanza kurejea taratibu kutokana kuingia watu wapya kila siku ambao hawajapewa elimu.

“Tutaendelea kutoa elimu na wadau wetu wa usaidizi wa kisheria walikuwa masokoni wiki mbili zilizopita, bado changamoto ipo,” anasema Susan kutoka EFG.

Watu wanaobanika kuwanyanyasa wanawake katika masoko jijini hapa wanapewa adhabu ya kulipa faini na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Picha| Gift Mijoe.

Serikali nayo haipo mbali

Vita ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia hupaswa kufanywa kuanzia ngazi za chini za Serikali.

Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa Ya Kigogo B, Emmanuel Tarimo anasema Serikali inafanya kazi kwa kuhakikisha miundombinu ipo sawa kwa ajili ya wanawake kufanya biashara na shughuli zao nyingine katika mazingira rafiki.

Katika ngazi ya kitaifa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina mpango wa kuendelea kudhibiti ukatili wa wanawake unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini. 

Waziri wa wizara hiyo Dk Dorothy Gwajima aliliambia Bunge wakati  akiwasilisha bajeti ya wizara yake Jijini Dodoma Mei, 2021 kuwa Sh1.6 bilioni  zimetengwa kwa ajili kuratibu uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na masuala ya jinsia katika sheria.

“Jumla ya Sh791 milioni zimetengwa kwa ajili ya kuratibu kampeni za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Dk Gwajima kwenye hotuba yake.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW