Majaliwa akataa kufungua ofisi ya Tanesco Kagera

September 20, 2021 12:13 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kutolidhishwa na thamani ya ujenzi wake.
  • Asema gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo yaliyopo.
  • Aagiza Tanesco kuwa makini katika matumizi ya fedha.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo yaliyopo.

Amesema akiweka jiwe la msingi atakuwa amehalalisha majengo mengine yajengwe kwa gharama hiyo kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko majengo yaliyopo. 

“Nini kilisababisha hadi kibanda kidogo cha mlinzi kikajengwa kwa Sh7 milioni? Kina matofali mangapi kama siyo ulaji ni nini? Hii si sahihi sijaweka jiwe la msingi wala kufungua na kile kibao kilichoandikwa jina langu kiondolewe. Serikali ipo makini katika usimamizi wa miradi na haya ni maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amekataa kufungua ofisi hiyo leo Septemba 20, 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

Mradi wa ujenzi huo umegharimu Sh483.42 milioni ambapo uzio umegharimu Sh94.2 milioni, jengo la ofisi Sh253.8 milioni na stoo Sh51.5 milioni.

Waziri Mkuu amesema Serikali inajenga majengo makubwa ya vituo vya afya ambayo ni jengo la mapokezi ya wagonjwa, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, nyumba ya daktari, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka na korido kwa gharama ya Sh500 milioni.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Tanesco uhakikishe katika miradi yake mingine ya ujenzi gharama zilingane na aina na idadi ya majengo.

Meneja Mwandamizi Usambazi wa Tanesco Makao Makuu, Mhandisi Nathanasias Nangali ambaye alisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, amesema mradi huo ulianza Septemba 11, 2018 na kukamilika Februari 08, 2020 kwa gharama za Sh483.5.

Amesema mkandarasi aliyenga mradi huo ni kampuni ya M/S RK Investment chini ya usimamizi wa mkandarasi mshauri Tanesco kitengo cha miliki.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW