Majaliwa atoa onyo matumizi yasiyo sahihi ya Tehama kwa vijana
Maadhimisho haya yanalenga kuwakumbusha na kuiwezesha jamii na Taifa kwa ujumla kutambua mchango mkubwa wa vijana katika maendeleo ya nchi na kuwapa fursa nyingi vijana kumuenzi na kumkumbuka Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Awataka wajiepushe na utapeli, wizi wa mtandaoni.
- Pia wajiepushe na uchachezi na kutunza amani ya nchi.
- Vijana watakiwa kutumia Tehama kujikwamua kimaisha.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi hususani vijana wajiepushe na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ikiwemo wizi, utapeli wa fedha n auchochezi unaofanywa kwa njia ya mtandao.
Pia amewaasa vijana nchini wajiepushe na kujiunga na makundi yasiyofaa, kujiingiza kwenye majukwaa ya uchochezi kwani vitendo hivyo vinavuruga amani, utulivu na mshikamano wa Taifa.
Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Oktoba 12, 2021 alipozindua maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa katika viwanja vya Mazaina wilayani Chato mkoani Geita.
“Kutokana na umuhimu huo Serikali imesisitiza matumizi sahihi ya Tehama kwenu vijana kwani ninyi ndiyo watumiaji wakubwa na wahanga wakubwa wa Tehama,” amesema Majaliwa.
Badala yake amewataka kutumia Tehama kama nyenzo ya kujiajiri na kufanya shughuli zitakazowasaidia kuboresha maisha yao kwa sababu ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.
“Vijana wengi wamefanikiwa kutokana na matumizi sahihi ya Tehama hususan kwa kufanya biashara kwa njia ya mtandao. Vijana wameweza kuanzisha na kuendesha vituo vya huduma za intaneti na pia kuanzisha wakala wa huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu,” amesema Majaliwa.
Aidha, amewataka vijana watumie fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira inayoikabili dunia kwa sasa.
“Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini pia tunayo fursa ya uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani,” amesema Majaliwa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda amesema wiki ya vijana imeanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha na kuwapa nafasi vijana na wadau wa shughuli za maendeleo yao kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali yanayowahusu kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Amesema maadhimisho hayo ambayo yalianza Oktoba 8, 2021 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14 yamehudhuriwa na vijana zaidi 1,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao pamoja na mambo mengine wamepata mafunzo ya aina mbalimbali yakiwemo na ya matumizi bora ya Tehama.