Mwanzo mpya: Tanzania, Ujerumani zaanzisha majadiliano ya ushirikiano

October 27, 2021 5:44 am ยท Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Ujumbe wa Serikali ya Ujerumani ulioshiriki majadiliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ukiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu. Kutoka kulia walioketi ni Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Hess, Kiongozi wa Ujumbe wa Ujerumani, Marcus Von Essen, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje, Amina Khamis Shaaban na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil. Tukio hilo limefanyika Jijini Dar es Salaam ambapo Ujerumani imetoa msaada wa Euro milioni 71 (Tsh. 190.5 bilioni) kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.


  • Ujerumani imeipatia Tanzania msaada wa Sh190.5 bilioni.
  • Fedha hizo ni kwa ajili ya kuboesha huduma za kijamii, afya ya mama na mtoto.
  • Nchi hizo mbili zaanzisha majadiliano baada ya kukwama tangu 2015.

Dar es Salaam. Huenda ustawi wa maisha ya wanawake na watoto ukaongezeka hivi karibuni baada ya Tanzania na Ujerumani kuanzisha upya majadiliano ya ushirikiano na uboreshaji wa miundombinu ya huduma za kijamii na kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Ujerumani imeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 71, sawa na Sh190.5 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya maji, uendelezaji wa maliasili na utalii, uboreshaji wa afya ya mama na mtoto.

Nyaraka za makubaliano ya msaada huo zimetiwa saini jijini Dar es Salaam kati ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje, Amina Khamis Shaaban na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Ujerumani, Marcus Von Essen.

Naibu Katibu Mkuu, Shaaban akizungumza baada ya kutiwa saini kwa nyaraka hizo Oktoba 26, 2021, ametaja maeneo yatakayonufaika na msaada huo kuwa ni afya ya mama na mtoto iliyotengewa Sh64.2 bilioni na mradi wa kuzuia migogoro baina ya wanyamapori na binadamu utatumia Sh16.1 bilioni.

โ€œMaeneo mengine yatakayonufaika na fedha hizi ni mpango wa kufidia upotevu wa makusanyo ya maduhuli katika sekta ya utalii kutokana na upungufu wa watalii walioingia nchini kwa sababu ya ugonjwa wa UVIKO 19, kuzuia ujangili, kuboresha miundombinu kwenye makazi na jamii inayozunguka maeneo ya Hifadhi za Taifa, utakaogharimu Euro milioni 15 (Sh42.7 bilioni),โ€ amesema Shaaban.ย 

Fedha nyingine Sh53.5 bilioni zitaelekezwa kuboresha huduma ya maji katika miji inayokua na kiasi kingine kitatumika kuboresha usalama wa maji katika maeneo ya baadhi ya miji nchini.

Kwa mujibu wa mkataba huo, Sh8 bilioni zitatumika katika masuala ya kulinda haki za akina mama na wasichana wanaokabiliwa na changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa kuwapatia msaada wa kisheria.

Shaaban ameishukuru Ujerumani kwa kuanzisha majadiliano na Tanzania baada ya kusitisha mijadala hiyo tangu mwaka 2015 na kuahidi kuwa fedha zitakazotolewa zitatumika ipasavyo na kwa malengo yaliyokusudiwa.

Wakizungumza katika Hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Hess na Kiongozi wa Ujumbe wa Ujerumani ulioshiriki majadiliano yaliyofanikisha kupatikana kwa msaada huo, Marcus Von Essen, wamesema Ujerumani imeamua tena kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo ya Tanzania.

Katika makubaliano mapya, Ujerumani itajikita zaidi kusaidia afya ya mama na mtoto, kusaidia masuala ya bima ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), maji na usafi wa mazingira, usimamizi wa fedha za umma, kuhifadhi maeneo ya urithi wa dunia ikiwemo Pori la Akiba la Selous na kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya kikatili.

Aidha, wamesema kuwa Ujerumani itarejesha mipango yake ya kusaidia miradi ya maendeleo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo tayari nchi yao imeanza kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa maji visiwani humo.

Pia Ujerumani itatoa kiasi kingine cha fedha Alhamisi Wiki hii ambapo mikataba ya misaada kadhaa itasainiwa kati ya nchi hiyo na Tanzania ikiwa ni mwanzo mpya wa kuhakikisha kuwa Ujerumani inashirikiana na Tanzania katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW