Nini kifanyike kuzuia ugonjwa wa kisukari?

November 6, 2021 8:15 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Inashauriwa kupunguza matumizi ya sukari nyingi na vyakula vilivyokobolewa.
  • Mtindo mbaya wa maisha huathiri uwezo wa homoni ya insulini kushughulika na kiwango cha sukari mwilini.
  • Kisukari ni moja ya visababishi vikuu ya vifo duniani.

Dar es Salaam. Idadi ya watu wenye kisukari duniani imeongezeka kutoka watu milioni 108 mwaka 1980 hadi watu milioni 422 kwa sasa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Idadi kubwa ya wagonjwa imeongezeka katika nchi zenye uchumi wa kati kuliko zile zenye uchumi wa juu. Kisukari kinatajwa kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo duniani ambapo watu milioni 1.5 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.

Endapo ugonjwa wa kisukari usipodhibitiwa, unaweza kusababisha upofu, kufeli kwa figo na magonjwa ya moyo. 

Ili kupunguza kasi ya ugonjwa wa kisukari inashauriwa kuzingatia njia zifuatazo:

Kupunguza matumizi ya sukari na vyakula vya wanga vilivyokobolewa

Vyakula vya wanga ni pamoja  na ngano na mahindi ambavyo kwa mazoea ya baadhi, huvikoboa kabla ya kusaga na kupata unga wa ngano na sembe kwa ajili ya kupikia.

Vyakula hivi husababisha ongezeko la kiwango cha sukari kwenye damu pamoja na kuchochea ongezeko la homoni ya insulini ambayo hushughulikia kiwango cha sukari mwilini.

Inashauriwa kutokukoboa nafaka hizo na badala yake kuzisaga kama zilivyo ili kuepukana na hatari ya kisukari.

Badala ya kutumia sukari nyingi kwenye vyakula, unaweza kula matunda na mbogamboga. Picha Medical news today.

Fanya mazoezi mara kwa mara

Mazoezi husaidia kuchochea homini ya insulin kufanya kazi yake vizuri. Pia mazoezi husaidia kiwango kidogo cha kichocheo cha insulini kutumika katika kuendesha kiwango sahihi cha sukari kwenye damu.

Ni vyema ukachagua mazoezi ambayo unayafurahia ili uweze kufanya mara kwa mara. Mfano kukimbia, kuruka kamba, kuogelea, kuendesha baiskeli na kutembea angalau nusu saa kila siku.

Mbali na kukuepusha na kisukari mazoezi yatakusaidia kuimarisha misuli, mifupa na maungio ya mwili.

Epuka uzito kupita kiasi

Japokua siyo watu wote wenye ugonjwa wa kisukari wana uzito uliopita lakini asilimia kubwa ya watu wenye ugonjwa wa kisukari hupitia changamoto hiyo.

Hali hiyo husababisha homoni ya insulini kutofanya kazi vizuri katika kuhakikisha kiwango sahihi cha sukari kwenye damu hivyo huufanya mwili kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.

Uzito uliopitiliza unaweza kupungua kwa kutokula kwa wingi vyakula vyenye mafuta mengi na wanga, kufanya mazoezi, na kutumia zaidi vyakula vitokanavyo na mimea kama mboga za majani na matunda.

Uzito uliopita kiasi unaathiri utendaji kazi wa homoni ya insulini ambayo inashughulikia kiwango cha sukari kwenye damu. Picha| people.com.

Tumia vyakula vyenye makapi mlo

Vyakula hivyo ni kama mboga za majani, matunda, na nafaka ambazo hazijakobolewa.

Vyakula hivi huchukua muda mrefu kusagwa mwilini na hivyo kiwango kidogo cha sukari ndiyo huingia kwenye damu, kinyume cha vyakula vilivyokobolewa.

Endapo kiwango kidogo cha sukari kinaingia kwenye damu na insulini inafanya kazi vizuri, mtu anakuwa amepunguza hatari ya mwili kupata ugonjwa wa kisukari.

Kuacha matumizi ya sigara

Sigara ni kichochezi kikubwa cha kupata ugonjwa wa kisukari pamoja na magonjwa ya moyo.

Inaenda mbali zaidi na kuwa sababu ya magonjwa makubwa ikiwemo saratani, kiharusi, magonjwa ya mapafu na uoni hafifu.

Sigara husababisha sumu ya “nicotine” kuingia mwilini na hivyo kusababisha homoni ya insulini kutokufanya kazi vizuri katika kuhakikisha kiwango sahihi cha sukari kwenye damu.

Kula vyakula sahihi na kubadilisha mtindo wa maisha kuwa kuijali afya yako kwani itakusaidia kuulisha mwili wako kiwango sahihi cha sukari na hivyo kuzuia ugonjwa huo.

Makala haya yameandaliwa na Afisa Lishe, Irene Kweka kutoka mkoani Dodoma. Ni mbobezi wa ushauri lishe kwa wagonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na kutengeneza mpango mlo (diet plan) kwa watu wenye uzito uliopita, wajawazito na watoto. Unaweza kumpata kupitia baruapepe: irenekweka7@gmail.com au nambaya simu, +255621870995.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW