Mfumuko wa bei mwezi Oktoba wabaki pale pale
- Umebaki asilimia nne sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Septemba 2021.
- Kabati, viatu vya wanaume na vitabu navyo vimeshuka bei.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba 2021 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa Septemba mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Oktoba 2021 ulikuwa asilimia nne ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Septemba 2021.
Taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyotolewa leo Novemba 8, 2021 imeeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na kushuka kwa bei ya bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo na vileo (vinywaji baridi) katika kipindi kilichoishia Oktoba 2021.
Licha ya mfumuko wa jumla kubaki tambalale, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba 2021 umepungua hadi asilimi 4.5 kutoka asilimia 4.6 ya mwezi Septemba.
Kati ya bidhaa zilizoshuka ni pamoja na samaki kwa asilimia2.4, bidhaa za kuokwa (asilimia 2.5), viazi mviringo (asilimia 1.4) na ndizi za kupikwa ambazo zimeshuka kwa asilimia 1.5.
Bidhaa zisizo za chakula zilizoshuka bei ni pamoja na kuni kwa asilimia 3.6, viatu vya wanaume pamoja na samani kama kabati (asilimia 1.1) na vitabu kwa asilimia 2.7.
Latest
