Wanasayansi wabaini mwamba nadra wa matumbawe duniani
Mwamba huo unapatikana karibu na kisiwa cha Tahiti huko bahari ya Pasifiki. Picha| UNESCO.
- Mwamba huo unapatikana karibu na kisiwa cha Tahiti huko bahari ya Pasifiki.
- Mwamba huo uko kwenye kina kati ya mita 30 hadi 65 ukiwa na urefu wa kilomita tatu
- Ni sehemu muhimu ya mazalia na chakula cha viumbe vya baharini.
Dar Es Salaam. Timu ya wanasayansi iliyotumwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika kufanya utafiti baharini imebaini moja ya miamba nadra sana na kubwa zaidi wa matumbawe karibu na kisiwa cha Tahiti huko bahari ya Pasifiki.
Taarifa iliyotolewa jana Januari 20, 2022 na UNESCO huko Paris, Ufaransa imesema mwamba huo uko katika hali nzuri na matumbawe yana umbo la ua la waridi na ugunduzi wake ni jambo la thamani kubwa.
“Hadi leo hii, tunafahamu vyema zaidi kilichoko mwezini kuliko kilichoko chini ya bahari. Ni asilimia 20 tu ya eneo la chini ya bahari ambalo ramani yake inafahamika.
“Ugunduzi huu wa kipekee huko Tahiti unaonesha kazi ya kipekee ya wanasayansi ambao chini ya uratibu wa UNESCO wanapanua ufahamu wetu wa kile kilichoko chini ya miguu yetu,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay.
Mpiga picha wa Ufaransa na mwaanzilishi wa 1 Ocean Campain akiwa chini ya bahari katika harakati za kupiga picha. Picha| UNESCO
Ni ugunduzi usio wa kawaida
Mwamba huo wa matumbawe uko kwenye kina cha kati ya mita 30 hadi 65 na urefu wake ni kilometa 3 katika mapana ya mita za upana 30 kwa 60, na hivyo kufanya kuwa mwamba wa matumbawe wenye hali bora zaidi na mkubwa kuwahi kurekodiwa na kufahamika duniani.
Mapana ya maumbo ya waridi ya matumbawe hayo ni mita 2.
Hadi sasa, idadi kubwa ya miamba ya matumbawe inayojulikana duniani iko kwenye kina cha hadi mita 25. Hivyo ugunduzi huu unaashiria kwamba kuna miamba mingi zaidi kwenye bahari, kwa kina cha zaidi ya mita 30.
“Haikuwa kitu cha kawaida kuweza kuona matumbawe haya makubwa na mazuri ya rangi ya poda ambayo yametanda eneo kubwa ambalo macho yanaweza kuona. Ilikuwa kama kazi ya sanaa” amesema Alexis Rosenfeld, ambaye ni mpiga picha kutoka Ufaransa na muasisi wa kampeni iitwayo “1 Ocean Campaign” na aliongoza timu hiyo ya wanasayansi ya kupiga mbizi.
Soma Zaidi:
- Bustani za matumbawe na uzuri uliojificha Ghuba ya Tanzania
- Makumbusho ya baharini inayongojewa kwa hamu Australi
Ugunduzi huu ni sehemu ya mpango wa kimataifa wa UNESCO kuchora ramani ya bahari.
Miamba ya matumbawe ni chanzo muhimu cha chakula kwa viumbe wa baharini, hivyo ugunduzu wa mwamba huo unaweza kusaidia utafiti kuhusu bioanuwai.
Viumbe wanaoishi kwenye miamba wanaweza kuwa muhimu kwa utafiti wa dawa na miamba pia inaweza kutoa ulinzi dhidi ya mmomonyoko wa fukwe na hata majanga kama tsunami.
Hatua ya UNESCO katika tafiti za baharini
Tume ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Bahari (Ocean Commission IOC) ya UNESCO, iliyoanzishwa mwaka wa 1960 na kuunganishwa na nchi 150, ndiyo inaratibu programu za kimataifa ikiwemo ramani ya bahari na mifumo wa tahadhari ya majanga kama vile tsunami pamoja na miradi ya utafiti wa kisayansi.
Pia ni Wakala na mlezi wa maeneo ya kipekee ya bahari, kupitia hifadhi 232 za viumbe hai baharini na maeneo 50 ya Urithi wa Dunia wa bahari yenye thamani Bora zaidi Ulimwenguni.
UNESCO inaongoza muongo wa Umoja wa Mataifa wa Sayansi ya Bahari kwa Maendeleo Endelevu, kutoka 2021 hadi 2030, ambayo mwaka huu inaonekana katika kuandaa mikutano mikuu kadhaa ya kimataifa ambayo itakuza uhamasishaji wa pamoja kuhusu uhifadhi wa bahari.
Latest
