Rais Samia awalilia wanafunzi nane waliofariki ajalini Mtwara
Gari la Shule ya Msingi ya King David baada ya kutumbukia shimoni. Picha | Gazeti la Mwananchi.
- Vifo hivyo vinadaiwa vimetokea baada ya basi lililokuwa limebeba wanafunzi wa Shule ya Msingi ya King David kutumbukia shimoni katika eneo la Mjimwema, Mikindani, mkoani Mtwara.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti na wafiwa waliopoteza ndugu kufuatia vifo vya watu 10 wakiwemo wanafunzi nane vilivyosababishwa na ajali ya basi la shule.
Ajali hiyo imetokea leo saa moja asubuhi Julai 26, 2022 katika eneo la mteremko la Mjimwema, Kata ya Magengeni, kuelekea Mitengo, Mikindani, Mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Nicodemus Simon Katembo, waliopoteza maisha ni watoto nane (wasichana 5 na wavulana 3) na watu wazima wawili ambao ni dereva na msaidizi wa gari hilo.
Majeruhi ni 19 (wasichana 13 na wanaume 6) ambao wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Ligula mkoani Mtwara kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
ACP Katembo amesema ajali hiyo imehusisha basi dogo la wanafunzi aina ya Hiace lenye namba ya usajili T 207 CTS mali ya shule binafsi ya awali na msingi ya King David iliyopo mkoani humo.
Ajali hiyo imetokana na gari hilo kushindwa kuhimili breki katika mteremko na kupoteza mwelekeo na hivyo kutumbukia kwenye korongo.
Rais Samia amewapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Katika Salamu zake za pole alizoziandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia amesema amesikitishwa na vifo hivyo na ametoa pole kwa wote waliopoteza jamaa zao.
“Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema na awajalie majeruhi wapone haraka,” amesema Rais Samia katika ukurasa wake.
Nimesikitishwa na vifo vya wanafunzi 8 wa Shule ya Msingi King David na watu wazima wawili vilivyotokea leo eneo la Mjimwema, Mikindani, mkoani Mtwara. Natoa pole kwa wote waliopoteza jamaa zao. Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema na awajalie majeruhi wapone haraka.
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) July 26, 2022
Latest