PSSSF: Wastaafu wanapata mafao kwa wakati

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Suleiman Mzee kushoto akipokea kitabu baada ya kutembelea banda la PSSS jijini Mwanza ambako maonyesho wiki ya huduma za kifedha yanafanyika. Picha na Mariam John
- Yasema malipo ya mafao yanatolewa ndani ya siku 60.
Dar es Salaam. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewatoa hofu wastaafu kucheleweshewa mafao yao kwa sababu imeanza kufanya malipo ndani ya siku 60 baada ya muhusika kukamilisha taratibu zote.
Afisa habari wa Mfuko wa PSSSF, Abdul Njaidi akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayofanyika Jijini Mwanza, amesema kisheria hakuna mwanachama anayecheleweshewa malipo yake baada ya kustaafu kwani kisheria mfuko unalipa mafao ndani ya siku 60.
“Tunalipa mafao ndani ya siku 60 na iwapo kuna mwanachama anapata changamoto ya kucheleweshewa malipo yake ndani ya kipindi hicho afike katika ofisi zetu ili aweze kusaidiwa,” amesema Njaidi.
Amesema katika maonyesho hayo wamepokea wanachama wengi ambao wamefika kufuatilia michango yao kutoka kwa waajiri.
Kuhusu waajiri ambao hawachangii michango yao kwa wanachama, Psssf hutuma taarifa za kuwambusha ili wahakikishe wanawachangia na kwamba hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi yao.
Awali Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Hifadhi ya Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu, Omary Mziya amekumbusha jukumu ya kimsingi waajiri kuchangia michango yao ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa ili kulinda maslahi ya wanachama na wananchi.
Lengo ni kuongeza wigo wa utoaji huduma na kuboresha mafao.
“Kama Ofisi ya Waziri Mkuu tunao wajibu wa kuwakumbusha waajiri kuweka michango ya wafanyakazi wao na hii imesaidia sana kupunguza malalamiko ya watu kutowekea fedha zao lakini pia kuendelea kutoa elimu ya kuwaelimisha wanachama ikiwemo kuwakumbusha waajiri kupeleka michango ya wafanyakazi wao,” amesema Mziya.
Mmoja wa wanachama waliotembelea banda hilo, Jofrey Jonas amesema pamoja na kufuatilia michango yake lakini pia alipita kuulizia kuhusu mikopo ya elimu inayotolewa na taasisi hiyo.
Latest