WhatsApp yaongeza udhibiti kujiunga na makundi ya mtandao huo
- Watumiaji wamepewa udhibiti wa kukubali au kukataa mialiko inayowataka kujiunga katika makundi yanayoanzishwa katika mtandao huo.
- Udhibiti huo utasaidia kuondoa malalamiko ya watumiaji ambao wamekuwa wakiunganishwa katika makundi bila idhini yao.
Dar es Salaam. Huenda malalamiko ya baadhi ya watumiaji wa mtandao wa WhatsApp kuunganishwa katika makundi ya mtandao bila ruhusa yao yakapungua kama siyo kuisha kabisa, baada ya uongozi wa mtandao huo kufanya maboresho katika sera zake za faragha.
Kwa mujibu wa taarifa ya WhatsApp ya maboresho mapya ya faragha (New privacy settings for Group), makundi hayo yamekuwa ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha watu wa rika tofauti katika mazungumzo ya pamoja, lakini washiriki wa makundi hayo wanahitaji udhibiti na uhuru wa kuingia kwenye makundi wanayoyataka.
“Kwa kuwa watu wanageukia kwenye makundi kwa ajili ya mazungumzo muhimu, watumiaji wameomba udhibiti zaidi juu ya uzoefu wao katika makundi hayo.
“Leo, tunaanzisha mipangilio ya faragha mpya na kukaribisha mfumo ili kukusaidia kuamua nani anayeweza kukuongeza kwenye makundi,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Ili mtumiaji afaidike na maboresho hayo anatakiwa kwenda kwenye anatakiwa kwenda kwenye mpangilio ya programu ukurasa wake wa WhatsApp kisha gusa akaunti (Account) >faragha (privacy) > kundi (groups).
Hapo mtumiaji anatakiwa kuchagua moja ya machaguo matatu: “Hakuna” (nobody); “Wasiliana na mimi” (my contacts); au “Kila mtu” (everyone).
Zinazohusiana:
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- Wadau mtandaoni watoa neno WhatsApp kudhibiti habari za uongo
“Kila mtu” inamaanisha utaunganishwa na kila kundi utakalounganishwa hata kama hujatoa idhini.
“Hakuna” inamaanisha kuwa mtumiaji hataingizwa au kuunganishwa kwenye kundi mpaka atoe idhini yake.
“Waasiliani na mimi” inamaanisha kuwa mtumiaji ataunganishwa kwenye makundi na watu waliopo katika orodha ya kitabu cha anuani zake tu (contacts).
Katika hatua hizo mbili za mwisho, mtumiaji wa WhatsApp anayemwalika mtumiaji mwingine kwenye kundi anatakiwa kutuma mwaliko wa faragha kupitia mawasiliano binafsi (private invite through individual chat ) huku mtumiaji aliyealikwa akipewa hiari ya kujiunga na kundi hilo kwa kupewa siku tatu za kukubali mwaliko kabla ya muda huo kuisha.
“Kwa sifa hizi mpya, watumiaji watakuwa na udhibiti zaidi juu ya ujumbe wa kundi wanaopokea. Mipangilio hii mpya ya faragha itaanza kugeuka kwa watumiaji wengine kuanzia leo na itakuwa inapatikana duniani kote katika wiki zijazo kwa wale wanaotumia toleo la karibuni la WhatsApp,” inaeleza taarifa hiyo ya WhatsApp iliyotolewa Aprili 3, 2019.