Wauguzi: Moyo wa utoaji huduma za afya duniani

May 17, 2020 11:19 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Heshima kwa muuguzi inapaswa itambulike kwa jamii yote.
  • Hujitolea sana kuwahudumia wagonjwa wakiwa hospitali.
  • Ni taaluma muhimu iliyojaa upendo na uvumilivu mwingi. 

Mei 12 kila mwaka ni sikukuu. Ni siku maalumu ya kusherehekea mashujaa wa sekta ya afya yaani wauguzi. Siku hii pia huakisi tarehe ya kuzaliwa ya muasisi wa taaluma ya kisasa ya uuguzi mwanamama Florence Nightingale. 

Taaluma ambayo kupitia kwayo imegusa maisha ya wengi na ni moyo wa utoaji wa huduma ya afya duniani. Florence ameiasisi taaluma hii kuanzia miaka ya 1860 na kufunua na kuonesha namna ambayo upendo, huruma na kujitolea ni muhimu katika utoaji huduma kwa wagonjwa.

Anafahamika kwa jina maarufu la “the lady with the lamp” yaani “mwanamke mwenye taa ya chemli” jina ambalo alilipata kutokana na kuwahudumia wanajeshi wa kiingereza kwenye vita ya Crimenia. 

Siyo lengo langu kueleza sana kuhusu hadithi za kweli hizi, lakini moja ya vitu vikubwa alivyofanya mwanamama Florence ni kuasisi shule ya kwanza ya wauguzi huko Uingereza mwaka 1860.

Kuanzia hapo taaluma hii imetukuka na kuheshimika duniani kote. 

Pamoja na hayo, bado heshima na stahiki inayostahili taaluma hii haijawa katika kiwango kinachostahili. Watu wengi huchukulia taaluma hii kama taaluma ya watu ambao hawakufanya vizuri shuleni ama watu ambao wamekosa sehemu ya kwenda.

Lakini pia watu wengi huwachukulia wauuguzi kama watumwa katika kada za afya jambo ambalo siyo sahihi. Hakuna huduma ya afya isiohitaji uangalizi na huduma ya muuguzi.


 Zinazohusiana


Muuguzi hutumia muda mwingi akihudumia wagonjwa na kuhakikisha kuwa wanapata faraja na kupata dawa ndani ya wakati. Muuguzi husafisha mgonjwa na kuhakikisha hakuna upenyo wa maambukizi.

Ninapomtazama muuguzi namtazama kama kiongozi wa kundi kubwa la muziki wa Orchestra. Kundi hili huwa na wataalamu wenye uzoefu na ustadi katika upigaji wa vyombo. Orchestra huwa na kuanzia wapiga vyombo 70 hadi 100 na zaidi. Lakini bila kiongozi hawafai kitu. Kwani yeye huamua mapigo na mwenendo wa ala za muziki na mpangilio mzima. 

Hawa ndiyo wauguzi, huamua katika timu nzima ya wataalamu mbalimbali wa afya wao huwa ni kiini na ndiyo watoa muelekeo na ufanikishwaji wa huduma hadi kwa mgonjwa. Heshima kwa muuguzi inapaswa itambulike kwa jamii na itambulike kuwa ni kada ambayo inahitaji moyo mpana na moyo wa kujitoa. 

Ni kada yenye hadhi ya nyota tano na hakuna huduma ya afya bora bila muuguzi. 

Ni watu wanaopaswa kuheshimika sana kwenye jamii maana wanafanya kazi ya kuokoa maisha ya watu wanaotibiwa hospitali. Picha|dreamstime.com

Nimekutana na watu ambao hutoa maneno machafu na makali kwa wauguzi yenye kejeli na dharau wakisahau kuwa hawa ndio hupokea mama zetu wanapojifungua. Husahau wauguzi hutoa huduma moja kwa moja hadi wakati ambao hawajiwezi. Ninadiriki kusema “malaika wa Mungu hutenda kazi ya uponyaji kupitia wauguzi”

Unapofika hospitali, ukakutana na muuguzi baada ya kusoma makala haya mtazame kwa upole na mpongeze kwa kazi yake ya kujitolea ya kugusa maisha ya wagonjwa. 

Mueleze kuwa yeye ni shujaa ambae ijapokuwa wimbo wake haujaimbwa wala sifa hazijataradadi lakini tabasamu na faraja aliotoa kupitia kujitoa kwake ni tunu tosha kwa utumishi wake uliotukuka.

Nimalizie kwa kusema kuwa taaluma ya uuguzi ni taaluma ya wito na ni taaluma ya wanaume na wanawake kwa pamoja. Wapendwa wauguzi, mchango wenu katika kusukuma gurudumu la afya ni wa thamani kubwa sana, unatambulika na saluti kubwa kwenu. 

Nyinyi ndio moyo wa utoaji huduma za afya. Kongole nyingi kwenu mashujaa. 

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mazoezi tiba na mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW