Watumiaji wa visimbuzi waongezeka licha ya sakata la “chaneli za bure”
- Idadi ya watumiaji wa visimbuzi imeongezeka kwa kasi kwa watumiaji zaidi ya 533,000 hadi milioni 2.7 ndani ya mwaka mmoja.
- Wadau wameiomba Serikali kurudisha chaneli za kutokulipia (Free-to-Air) katika visimbuzi hivyo kwa kuwa bado watu wengi hawapati idhaa hizo za kitaifa.
- Ongezeko hilo linawapa matumaini baadhi ya wamiliki wa chaneli na wadau wengine wa habari katika uzalishaji zaidi wa maudhui yatakayowafikia watu wengi.
Dar es Salaam. Licha ya kuwepo sakata la kuondolewa kwa chaneli zisizolipiwa Agosti 2018, idadi ya watumiaji wa visimbuzi imeongezeka kwa kasi kwa watumiaji zaidi ya 533,000 hadi milioni 2.7 ndani ya mwaka mmoja.
Pamoja na ukuaji huo, bado wadau wameiomba Serikali kurudisha chaneli za kutokulipia (Free-to-Air) katika visimbuzi hivyo kwa kuwa bado watu wengi hawapati idhaa hizo za kitaifa.
Takwimu za Mawasiliano za robo ya mwisho ya mwaka 2018 (Oktoba hadi Disemba) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa visimbuzi zimeongezeka toka milioni 2.23 mwaka 2017 hadi 2.76 kwa mwaka jana.
Matokeo ya takwimu hizo yanabadili nadharia ya awali iliyokuwepo kuwa huenda uamuzi wa TCRA kuamuru kampuni za Multichoice (DStv), Azam na Zuku kuondoa chaneli zisizolipiwa zingefanya watumiaji wengi kuvikacha visimbuzi kutokana na kukosa huduma walizokuwa wakizipenda.
Mbali na kufuta nadharia hiyo, ongezeko hilo linawapa matumaini baadhi ya wamiliki wa chaneli na wadau wengine wa habari katika uzalishaji zaidi wa maudhui yatakayowafikia watu wengi.
Kati ya visimbuzi milioni 2.7 vilivyorekodiwa mwaka jana, asilimia 58.9 ni vile vya dijitali vya kulipia kupitia mitambo ya ardhini (DTT) ikifuatiwa na vile vya setilaiti.
Kabla ya Serikali kuamuru kwa chaneli za FTA kwenye visimbuzi hivyo vya Azam, Zuku, na Azam, watumiaji wote walikuwa wakizipata chaneli za ndani zote zikiwemo ITV, Channel Ten, EATV, Star Tv lakini baada ya uamuzi huo hazipatikani tena.
Serikali ilieleza kuwa uamuzi huo ulifanywa kuhakikisha sheria za ugawaji leseni za uonyeshaji maudhui zinafuatwa na kuhakikisha kuwa chaneli zisizolipiwa zinaonyeshwa katika visimbuzi vinavyotumia mitambo ya kurushia matangazo iliyosimikwa nchini.
Hata hivyo, baada ya kuondolewa kwa chaneli hizo huenda katika visimbuzi vya Azam, Zuku na DStv huenda kumewafanya baadhi ya watu kuhamia katika visimbuzi vyenye chaneli zisizolipiwa na kusababisha idadi ya visimbuzi kuongezeka mwaka jana.
Zinazohusiana: Haya yanaweza kuisadia chaneli mpya ya Utalii Tanzania kuifikia dunia kirahisi
Watumiaji wa huduma za simu benki wazidi kupaa Tanzania, wafikia milioni 23
Wadau wanaona kuna haja ya Serikali kukaa na wenye visimbuzi ili chaneli ziweze kuonekana kwa wote kwasababu kuongezeka kwa idadi ya watumiaji kunatakiwa kwenda sambamba na upatikanaji wa maudhui mbalimbali ambayo hayapatikani katika visimbuzi vyote.
“Maudhui ya vipindi vya ndani hayafikii watumiaji wa visimbuzi vyote. Mfano, mimi sina kisimbuzi cha chaneli za bure hivyo hata habari ya ITV inabidi niangalie kwenye njia za digitali,” amesema Dk Geoffrey Karokola, Mhadhiri wa Tehama wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dk Karokola, anayetoka katika Kitengo cha Kompyuta, anasema suala la visimbuzi linapaswa kuangaliwa upya kwa sababu idadi ya watumiaji wa visimbuzi iliyoongezeka huenda isiakisi hali halisi kwa kuwa kuna watu wengi wangependa kununua hivyo.
Ameeleza kuwa kutokuwepo kwa baadhi ya chaneli za kutokulipia kumeleta tofauti katika upatikanaji wa taarifa ndani ya jamii.

Kati ya visimbuzi milioni 2.7 vilivyorekodiwa mwaka jana, asilimia 58.9 ni vile vya dijitali vya kulipia kupitia mitambo ya ardhini (DTT) ikifuatiwa na vile vya setilaiti. Picha| Mtandao.
Lakini licha ya watumiaji visimbuzi vya kulipia kuongezeka bado kuna changamoto hasa kwa chaneli ndogo ambazo hazijajitanua vya kutosha kimasoko katika kurusha matangazo yao katika visimbuzi hivyo kutokana na gharama zao za uendeshaji.
Hii inalazimisha wapenda maudhui mbalimbali wasiokuwa na kisimbuzi fulani kutafuta njia mbadala ya kupata maudhui kupitia mtandaoni.
Kwa mujibu wa TCRA kuna jumla ya televisheni za mtandaoni 84 zilizosajiliwa mpaka Oktoba 16, 2018 ambazo zimekuwa kimbilio kwa baadhi ya watu wasiokuwa na visimbuzi wanavyovihitaji hususan katika kufuatilia taarifa za habari kutoka chaneli za ndani.
“Serikali ilegeze masharti ili chaneli zionekane kote na ziwafikie Watanzania wengi,” amesema Bavon Benjamin mwazilishi wa chaneli ya Native Bongo TV inayorushwa kwenye baadhi ya visimbuzi vyenye leseni ya kurusha FTAs.
Benjamin anasema kutokurushwa kwa chaneli za ndani katika baadhi ya visimbuzi kumesababisha watazamaji wachache kwa chaneli changa hivyo hata wanaoleta matangazo wanapeleka kwa chaneli kongwe kuwafanya wao wakose matangazo ambayo yangeleta mapato mengi.
“Ili urushe chaneli yako katika mkoa mmoja katika visimbuzi vya chaneli za bure mmiliki inakupasa ulipe milioni 2.2 kwa mwezi na kwa Dar es Salaam uwe na milioni 4.4 kwa mwezi hivyo ni changamoto kwetu,” amesema Benjamin.
Latest
