Watanzania waishio China watolewa hofu virusi vya corona
- Ubalozi wa Tanzania nchini humo umesema mpaka sasa hakuna Mtanzania aliyethibitika kupata ugonjwa huo.
- Wametakiwa kuchukua tahadhari muhimu za kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.
- Watakaopata changamoto yoyote watakiwa kuwasiliana na ubalozi.
Dar es Salaam. Watanzania waishio nchini China wametakiwa kuwa watulivu na waendelee kuzingatia maelekezo ya Serikali ya nchi hiyo katika kuchukua tahadhari muhimu za kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.
Virusi hivyo husababisha matatizo ya kupumua ambapo dalili zake zinasemekana kuwa homa, kikohozi kikavu kisha baada ya wiki moja, mwathirika anakuwa na matatizo ya kupumua na kuhitaji matibabu kwa haraka.
Taarifa iliyotolewa leo (Januari 28, 2020) na Ubalozi wa Tanzania nchini China, inaeleza kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu Mtanzania aliyeathirika na ugonjwa huo kutoka nchini China, Vietnum, Korea Kaskazini na Mongolia zilizopo katika eneo la uwakilishi la ubalozi wa Tanzania katika kituo cha Beijing
“Serikali ya China imechukua hatua madhubuti kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo. Aidha, Serikali ya China kwa ujumla wake inalipatia kipaumbele stahiki suala la uwazi na kuujulisha umma kuhusu kuchukua tahadhari, kuzuia maambukizi zaidi na kutoa tiba ya ugonjwa huo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ubalozi wa Tanzania nchini China umewataka Watanzania waishio nchini humo kuwa watulivu na kuendelea kufuata maelekezo wanayopewa ili kujikinga na maambukizi mapya ya virusi hivyo.
“Aidha, ubalozi unawasihi Watanzania kuwasiliana haraka na ubalozi, mamlaka za vyuo, jimbo, jiji pale itakapojitokeza changamoto ya aina yoyote,” inasomeka sehemu ya taarifa ya ubalozi huo.
Hadi kufikia mchana wa leo zaidi ya watu 100 wameshafariki kutokana na homa inayosababishwa na virusi hivyo. Wengi wa watu walioambukizwa wapo katika mji wa Wuhan ambapo ndipo vilipozuka virusi hivyo ambapo umewekwa chini ya masharti magumu ya raia wake kutosafiri.
Katika mji huo, raia wa kigeni wote wametakiwa kuwa na subira na waendelee kukaa mahali walipo, Serikali hairuhusu ndege za kukodi (chartered flights) kutua Wuhan wala usafiri wowote wa umma kwenda katika jiji hilo.
Pia Serikali ya China haitoruhusu kuwahamishia raia wa kigeni katika miji mingine kwa lengo la kuendelea kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.
Wakati huo huo, mataifa kote duniani yanapanga kuwaondoa wafanyakazi wao wa kibalozi pamoja na raia kutoka maeneo ya China yaliokumbwa na virusi vya Corona vinavyosambaa kwa haraka.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya China, Xinhua, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ana imani kuhusu uwezo wa nchi hiyo wa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona.
Katika mkutano na maafisa wa serikali ya China mjini Beijing, Tedros amesema ameidhinisha hatua za Serikali ya China za kukabiliana na mlipuko huo kufikia sasa na kushauri kuondolewa kwa raia wa kigeni nchini humo.