Wanafunzi SJUIT wavumbua teknolojia kuwadhibiti madereva walevi
- Itasaidia kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na ulevi.
- Ni wakati wa Serikali kuwekeza kwa vijana wabunifu kupunguza changamoto zilizopo katika jamii.
Ernest Mchome, Mwanafunzi mwaka wa nne kitivo cha Uhandisi Umeme (SJUIT) akielezea jinsi mfumo wa kugundua dereva aliyekunywa pombe unavyofanya kazi. Picha| Zahara Tunda.
Dar es Salaam. Licha ya ulevi kuwa sababu kubwa ya ajali za barabarani, wanafunzi wabunifu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT) wamevumbua teknolojia itakayowadhibiti madereva walevi na kupunguza ulemavu na vifo vinavyotokana na ajali hizo.
Ernest Mchome, Imaan Sebastian na Frank Temu wanaosoma mwaka wa nne katika kitivo cha Uhandisi Umeme chuoni hapo wamevumbua kifaa kubaini kiwango cha kilevi kilichopo kwenye damu ya dereva (Alcohol Detection System) ambacho hufungwa kwenye gari.
Kinakuwa na urefu wa mita tatu kutoka alipo dereva na kinanusa harufu ambayo itapimwa kama pombe imezidi kiwango kinachohitajika na kupeleka taarifa hizo moja kwa moja kwenye mfumo wa kompyuta utakaosimamiwa na wataalamu.
“Hiki kifaa kinapima ulevi kati ya kile kiwango cha 0.05g/dl hadi 0.06g/dl hivyo dereva akifikia hapo kifaa kitapiga kelele kumtaarifu dereva amezidisha kiwango cha pombe na anahitaji kupaki gari pembeni,” anasema Ernest Mchome, mmoja wa wanafunzi waliobuni mfumo huo.
Askari wa barabarani wataweza kupata taarifa za dereva aliyelewa na kuzifanyia kazi kwa wakati ikizingatiwa kuwa kinaonyesha muda na eneo dereva alipo.
Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, kifungu cha 45 (Driving a motor vehicle with blood-alcohol concentration above prescribed limit.) kinakataza mtu kuendesha gari akiwa amekunywa pombe zaidi ya kipimo cha ni 0.08g/dl. Kiwango hicho kinachotumika katika nchi yetu ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango ambacho kimewekwa kimataifa ambacho ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na 0.02g/dl kwa dereva asiye na uzoefu.
Sheria hiyo bado haijatekelezwa ipasavyo kuwabana madereva ambao kwa kujua au kutokujua wanaendelea kutumia vileo wakati wa kuendesha vyombo vya usafiri.
Wanafunzi hao wanaamini kuwa mfumo huo utasaidia kupunguza ajali na wamewaomba wadau kujitokeza kuwawezesha ili wakamilishe mradi wao ambao uko katika hatua za majaribio.
“Serikali ituunge mkono, ili vijana tuendelee na ubunifu tunaoufanya, usiishie kwenye maonyesho,” anasema Yona Laizer mmoja ya wadau wa masuala ya vijana.

Jinsi mfumo wa kugundua kiwango cha pombe unavyounganishwa kwenye gari. Picha| Rodgers George
Kulingana na Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) juu ya usalama barabarani zinaeleza kuwa katika nchi zilizoendelea asilimia 20 ya madereva waliojeruliwa vibaya katika ajali walikutwa na kiasi kikubwa cha pombe katika damu. Katika nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika ikiwemo Tanzania inafikia hadi asilimia 69.
Akizungumzia ubunifu wa wanafunzi hao wakati wa maonyesho ya miradi ya ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuendeleza vipaji na ubunifu wa vijana ambao wanagundua teknolojia zitakazosaidia kutatua changamoto katika jamii.
“Huu ni ubunifu mkubwa inabidi mtafutiwe nafasi wiki ya nenda kwa usalama barabarani muweze kuonyesha watu wengi zaidi,” amesema Mavunde.
Latest