Vyombo vya udhibiti vyaibua mkanganyiko ukuaji wa biashara, uwekezaji Tanzania

April 10, 2019 8:43 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkanganyiko huo unatokana na muingiliano wa majukumu unaosababisha usumbufu kwa wafanyabiashara na wawekezaji wakati wakitimiza shughuli zao.
  • Umbali wa kutoka makao makuu na maabara za taasisi ya mionzi hadi eneo wanalofanyia kazi nayo ni kero kwa wadau wa maendeleo.
  • Majaliwa amewataka mawaziri wa sekta wakae pamoja kupitia sheria na mgawanyo wa majukumu wa taasisi za udhibiti ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa.

Dar es Salaam.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Jenista Mhagama akutane na mawaziri wa sekta nyingine ikiwemo zinazoshughulikia uwekezaji na biashara ili watafute namna ya kuondoa mkanganyiko wa majukumu uliopo kwenye vyombo vya udhibiti hapa nchini.

Vyombo hivyo vya udhibiti ni pamoja na  Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 

Vyombo vingine ni  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na taasisi ya mionzi.

Majaliwa ametoa agizo hilo jana (Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020 ambapo bunge lilikubali kupitisha Sh148.8 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema licha ya Serikali kujenga mazingira wezeshi na rahisi ya kufanya biashara na uwekezaji, bado kumekuwepo na malalamiko ya mgongano wa maslai wa vyombo hivyo kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

“Changamoto nyingine ambayo imeonekana kuwa kikwazo cha biashara na uwekezaji ni muingiliano wa majukumu ya taasisi hizo. Kwa mfano, uwepo wa majukumu yenye kufanana kwa TFDA, TBS, Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi ya Maziwa, Bodi ya Nyama, Baraza la Mifugo, EWURA, SUMATRA na TANROADS ni kikwazo kikubwa katika kurahisisha mazingira ya kufanya biashara,” amesema Majaliwa.

Amebainisha kuwa  Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu mamlaka hizi na namna ya utendaji kazi wake. 


Soma zaidi: 


Miongoni mwa kero hizo ni mchakato wa muda mrefu wa kupata leseni za biashara, gharama za usajili wa bidhaa zinazotozwa na TFDA, suala la viwango vya TBS na  madai ya kuwepo kwa unyanyasaji unaofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana na polisi dhidi ya wafanyabiashara.

Miundombinu ya barabara ni miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa biashara na uwekezaji. Picha! Mtandao.

Kero nyingine aliyowekwa wazi na Majaliwa ni umbali wa kutoka makao makuu na maabara za taasisi ya mionzi hadi eneo wanalofanyia kazi kama vile bandari na viwanja vya ndege.

Kutokana na mkanganyiko huo, tayari ametoa maelekezo kwa Mawaziri wa sekta husika chini ya uratibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) wakae pamoja kupitia sheria na mgawanyo wa majukumu wa taasisi za udhibiti ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza mawaziri husika wahakikishe kuwa wakuu wa Mamlaka ya Mapato na taasisi zake, wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria bila kuwabughudhi wafanyabiashara na wawekezaji.

Wakati wa mjadala huu, wabunge 142 walichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kati ya hao, wabunge 98 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja bungeni na wabunge 44 walichangia kwa njia ya maandishi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...