Vyeti vya kuzaliwa kwa watoto kupatikana ngazi ya kata Tanzania
- Majaribio yaanza kufanyika Mkoa wa Mwanza.
- Itarahisisha watoto wengi kupata vyeti hivyo.
- Mpaka sasa watoto milioni 6 wa umri chini ya miaka mitano wamepata vyeti vya kuzaliwa.
Mwanza. Serikali imezindua zoezi la utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano litakalofanyika ngazi ya kata ili kuongeza kasi ya utoaji wa vyeti hivyo kwa kundi hilo.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Haki za Kisheria kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Lina Msanga amesema kabla ya uzinduzi huo zoezi la utoaji wa vyeti lilifanyika ngazi ya halmashauri pakee ambapo toka zoezi hilo lianze jumla ya watoto milioni 6 wenye umri chini ya miaka mitano wameshasajiliwa nchini kote.
Amesema kwa sasa zoezi la utoaji wa vyeti ngazi ya kata kwa majaribio linaanza mkoani Mwanza ambapo jumla ya kata 191 na vituo vya afya 389 vitashiriki katika kutoa vyeti hivyo.
“Na tunatarajia vituo hivyo kuongezeka na kufikia 580 mkoani Mwanza na zoezi hili litakuwa na mafanikio makubwa,” amesema Lina katika uzinduzi huo uliofanyika leo Agosti 31, 2021 Wilayani Nyamagana katika Mkoa wa Mwanza.
Cheti cha kuzaliwa humsaidia mtoto kutambulika pamoja na wazazi wake kisheria ili kupata msaada wakati apatapo matatizo.
Pia husaidia kupata hati ya kusafiria nje ya nchi hivyo basi kumuwezesha mtu kujulikana kwamba ni raia wa nchi gani na kuwawezesha wanafunzi kujiunga na vyuo na kupata mikopo ya elimu ya juu.
Vile vile cheti cha kuzaliwa ni kitambulisho cha msingi ili kupata kitambulisho cha Taifa kinachomwezesha mtu kupata mkopo, dhamana katika sehemu yoyote ile nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi ametaja mila , desturi na tamaduni za baadhi ya makabila nchini zimekuwa kikwazo cha watoto wengi kukosa fursa ya kuandikishwa kupata cheti cha kuzaliwa.
Amewataka wazazi kuhakikisha watoto wote waliozaliwa kimila wanaandikishwa ili wasipoteze taarifa zao muhimu pale zitakapohitajika huko mbeleni.
“Lipo tatizo la wazazi kushindwa kupewa majina kutokana na sababu za kimila, niombe watoa huduma za afya kuchukua taarifa zao ili baada ya muda wazazi watakapowapatia majina warudi kwenye vituo husika ili kusajiliwa,” amesema Profesa Kabudi.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel alimhakikisha Waziri huyo kuwa zoezi hilo litasimamiwa vizuri na mkoa huo utakuwa wa mfano.
Latest