Unayoweza kumfundisha mtoto kutumia vizuri fedha

February 13, 2020 9:00 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfundishe kuweka akiba, mpe kazi ambayo utamlipa kiasi fulani cha pesa na wakati mwingine mkopeshe fedha ili baadaye akulipe.
  • Tabia hizi zitamjenga mtoto kujua thamani ya pesa na kutumia vizuri hata atakapokuwa mtu mzima. 

Kuitunza familia kwa sehemu kubwa ni jukumu la kifedha ambalo wazazi hufanya. Ili kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji yote wanayotaka, wazazi na walezi hupambana huku na kule kupata fedha za kumudu gharama za mahitaji hayo. 

Kumpa mahitaji yote mwanao haitoshi. Ni zaidi ya hapo. Mzazi bado ana jukumu la kumsaidia mtoto wake kujifunza tabia ya kutafuta, kutumia na kuweka akiba ya fedha. 

Watoto wanapata mtazamo sahihi wa fedha tangu wakiwa wadogo. Kwa hiyo ni muhimu kwa wazazi kuanza kuwafunza tabia za kusaka na kutunza fedha tangu wakiwa wadogo. 

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Michigan cha nchini Marekani wa watoto kuhusu mtazamo wa fedha wa mwaka 2018, unaeleza kuwa mtoto akifundishwa kutumia vizuri fedha itamsaidia kujisimamia katika masuala ya mipango yake hata akiwa mtu mzima.

“Utafiti unapendekeza kuwa wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wao kuelewa kwanini wananunua au wanataka kununua kitu fulani,” anaeleza Profesa Scott Rock katika ripoti ya utafiti huo. 

Kama wewe ni mzazi hujui uanzie wapi katika kumjenga mtoto wako kuhusu masuala ya fedha, dondoo hizi zinaweza kukusaidia kuimarisha fikra zake: 


Mfundishe kuweka akiba

Mbali na kumfungulia akaunti ya benki kwa ajili ya kumuwekea fedha, bado una jukumu la kumfundisha mtoto wako kutunza fedha zake mwenyewe nyumbani. 

Hizi ni zile fedha ndogo ndogo unazompa. Mfundishe kutotumia fedha zote anazopata hata kama ni zawadi, atumie kiasi kidogo na kinachobaki atunze. 

Ili kuhakikisha anawajibika vizuri katika  tabia hiyo, weka utaratibu wa kumpa zawadi ikiwa atafikia malengo mliyowekeana ya kutunza fedha. 

Mwandishi wa vitabu wa Marekani, Gretchen Rubin, anasema zawadi au kukubali kazi nzuri anayofanya mtu inamhamasisha kufanya vizuri zaidi na kujiona unamjali na kumthamini kwa kile anachofanya, jambo linaloleta matokeo chanya na kujenga tabia inayodumu muda mrefu.

Tabia ya kuweka akiba itamsaidia mtoto kuepuka matumizi holela ya fedha. Picha|NASA Federal Union.

Mshirikishe katika mipango ya familia

Kama mtoto wako yuko katika nafasi nzuri ya kuelewa mambo, mshirikishe katika kuandaa bajeti na matumizi ya familia, bajeti za mwezi za kawaida au mambo ya maendeleo.

Njia shirikishi ni pamoja na kumuuliza nini anadhani kinafaa kifanyike kwa kiasi cha pesa kilichopo.  Hii itamsaidia kuongeza uwezo wake wa kufikiria na kuona umuhimu wa kupanga matumizi. 


Zinazohusiana: 


Mpe kazi ya malipo

Watoto wanapenda kucheza na kufanya kazi hasa wakiwa wadogo. Unaweza kutumia njia hii kuwapa kazi zilizo ndani ya uwezo wao kwa ahadi ya kuwapa fedha kidogo. 

Hali hiyo itawasaidia watoto kujiona wanawajibika kufanya kazi kwa bidii na kujipatia kipato hata pale wanapokuwa wakubwa. Fanya naye kazi pamoja na baadaye mpe kiasi fulani cha pesa kuonyesha unathamini kazi nzuri aliyofanya, jambo litakalomjenga kupenda kazi daima. Hakikisha unamdhibiti katika jambo hili ili asione kila kazi anayofanya anastahili pesa.

Baada ya kumkabidhi pesa, ni muhimu kumkumbusha kuweka akiba na kutumia kwa matumizi yanayofaa. 

Sambamba na hilo, unaweza kumjengea utamaduni wa kumkopesha fedha. Siyo kila atakapohitaji pesa ni lazima umpe. Wakati mwingine mwambie unamkopesha na atatakiwa kurudisha. Hii itamfanya aone thamani ya pesa na kutumia vizuri. 


Mfungulie akaunti ya benki

Kama uchumi wako unaruhusu, ni vema kumfungulia mwanao akaunti ya benki ya akiba ambayo utakuwa unamhifadhia fedha kwa ajili maisha yake ya baadaye au ikitokea dharura inayomuhusu. 

Mwambie mtoto wako ana akaunti benki na madhumuni ya kumfungulia akaunti hiyo. Hii ni njia mojawapo ya kumzoesha mtoto kuweka akiba na kuthamini kila fedha anayopata.

Ukimfungulia mtoto akaunti ya benki atajiona anathaminiwa na kupendwa. Picha| Nation Sacco.

Mfunze kuwekeza anachopata

Unaweza kumfundisha mtoto kuwekeza fedha zake katika shughuli ndogo ndogo ikiwemo kutengeneza barafu, vitafunwa na kuviuza akiwa nyumbani au hata kupeleka madukani. Hii ni tofauti na kuweka akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Katika suala hili, mtoto anajifunza kufanya biashara kwa kuwekeza fedha kidogo anayoipata ili kupata faida lukuki ya faida. 

Hili inaweza kulifanya katika muda wa ziada na linatakiwa kufanyika kwa uangalizi wa karibu wa mzazi ili lisimtoe mtoto katika kutimiza masomo ya darasani. 

Hata hivyo, unatakiwa kufahamu kuwa siyo njia zote zinazoweza kumjenga mtoto katika matumizi mazuri ya fedha, muhimu ni kumsoma kwanza mtoto wako kabla ya kutumia njia hizi. 

Enable Notifications OK No thanks