Ubia wa malipo tiketi za ndege utakavyozifaidisha ATCL, CRDB
- Wateja wa ATCL sasa kulipia tiketi za ndege katika matawi yote ya CRDB.
- Utapunguza usumbufu wa kutegemea njia moja ya malipo.
- Pia utachochea ujumuisha wa kifedha na ukuaji wa sekta ya anga.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha linaongeza ushindani katika sekta ya usafiri wa anga nchini, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa mara nyingine limeimarisha uhusiano na wateja wake kwa kuwaongezea mfumo mwingine wa malipo ya tiketi za ndege.
Hatua hiyo imekuja baada ya ATCL kuingia ubia na benki ya CRDB wa kuunganisha mfumo wa malipo ili kuwawezesha wateja wa shirika hilo kulipia tiketi zao za ndege kupitia matawi na wakala wa benki hiyo katika maeneo mbalimbali Tanzania.
Malipo hayo yatafanyika katika matawi 268 ya benki hiyo nchini, huduma za fedha kwa njia ya simu (SimBanking) na wakala wa CRDB zaidi ya 20,000 waliopo maeneo mbalimbali.
Mkurungezi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema ubia huo wa kibiashara wa kuunganishwa kwa mifumo ya malipo ya benki ya CRDB ni muendelezo wa mikakati ya ukuaji wa shirika hilo ambapo wateja wake wanahitaji uwanda mpana wa kufanya malipo na kupata huduma bora popote walipo.
“Ni imani ushirikiano huu na Benki ya CRDB utasaidia kufikia azma yetu ya kutoa huduma bora za usafiri kwa njia ya anga,” amesema Matindi wakati wa uzinduzi wa ubio huo Desemba 14, 2021 jijini Arusha.
Septemba 9 mwaka huu, shirika hilo lilianzisha mpango wa “kibubu” unaowawezesha mwananchi kulipia kidogo kidogo mpaka atakapo kamilisha malipo ya tiketi yake ya ndege.
Katika mpango huo, mwananchi atatakiwa kuweka Sh50,000 kwa mara ya kwanza na kiasi kinachobakia atatakiwa kulipa kidogo kidogo kwa kiwango anachokimudu mpaka safari yake itakapofika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Denge la Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi katika uzinduzi wa huduma ya malipo ya tiketi za ndege za ATCL kupitia mtandao wa Benki ya CRDB. Picha| ATCL.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumzia ubia huo amesema utawarahisishia wateja wa ATCL kufanya malipo popote walipo kulingana na machaguo yao ya ya njia ya kulipia.
“Pamoja na kuwa wateja watakuwa wakilipia tiketi zao kwa urahisi, vilevile uunganishwaji wa mfumo huu wa malipo na mfumo wa ATCL utasaidia kuongeza ufanisi katika upande wa upokeaji wa malipo ya tiketi,” amesema Nsekela.
Kabla ya mfumo huo, tiketi za ndege za ATCL zilikuwa zinalipiwa kwa njia ya mtandao kupitia kadi ya benki hiyo ya ‘TemboCard’ pekee hivyo kuongezeka kwa njia hizo nyengine kunawapa wateja uhuru wa kufanya malipo kwa njia ambayo ni rahisi kwao kwa wakati husika.
Hatua hiyo inaongeza wigo wa ujumuishaji wa mifumo ya fedha nchini ili kuwapata fursa wananchi uwanja mpana wa kupata huduma kuliko kutegemea sehemu, jambo linalosaidia kuongeza kasi ya biashara na shughuli za maendeleo.
Kwa sasa, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lnachuana vikali na Shirika la ndege la Precision Air baada ya kampuni ya ndege ya FastJet kumwaga manyanga miaka miwili iliyopita.
Katika hotuba zake Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisema kuwa Serikali yake itaendelea kuilea ATCL kimkakati ii liweze kujiendesha kwa ufanisi na kibiashara ikiwemo kulitua mzigo wa madeni makubwa na kulipa ahueni ya baadhi ya tozo na kodi.
ATCL ina vituo zaidi ya 23 ambavyo ndege zake zinatua ndani na nje ya nchi ambapo inatarajia kufufua safari ambazo zilisitishwa hasa wakati wa janga la Uviko-19.
Latest



