TFDA yawakamata 2 kwa kuuza dawa bandia
- Yabaini uwepo wa toleo (batch) la dawa bandia ya binadamu ya vidonge aina ya Duo-cotexcin sokoni.
- Watu wawili wakamatwa kwa kuuza dawa hizo ambazo hazina viwango vya ubora.
- Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari na kutoa taarifa wanapokutana na dawa wanazozitilia mashaka.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imetahadharisha umma kuhusu matumizi ya toleo (batch) la dawa bandia ya binadamu ya vidonge aina ya Duo-cotexcin kutokana na kutokidhi vigezo vya ubora vinavyotakiwa katika soko la dawa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFDA, dawa hiyo inatumika kutibu ugonjwa wa malaria, inadaiwa kutengenezwa kwa kughushi na kiwanda cha Zhejiang Holley Nanhu Pharmaceutical Co.Limited cha nchini China.
Kasha la dawa hiyo linaonesha namba ya toleo kuwa ni 170,259, na ilitengenezwaFebruari 25,2017 na muda wake wa kuisha ni Februari, 2019.
Aidha mamlaka hiyo imeweka bayana kuwa hadi sasa jumla ya makasha 22 ya vidonge 9 kila moja ya dawa bandia hiyo yalikutwa kwenye maduka mawili ya dawa ya Julieth Francis Madrina na Swaib Abrahaman eneo la Kinondoni Mkwajuni na ambapo watuhumiwa wamekamatwa ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Taarifa hiyo iliyotolewa na ofisi ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, imetahadharisha umma, wafanyabiashara na watoa huduma za afya kuwa makini na makasha ya dawa hiyo pale wanapopewa kutoka maduka ya dawa na vituo vya kutolea huduma ya afya.
Aidha ametoa rai kwa watoa huduma za afya kurudisha dawa hizo na kutoa taarifa kwa mamlaka hiyo ili taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa na kuwataka watanzania kutoa taarifa punde wanapobaini uwepo wa dawa bandia madukani na sehemu zinginezo ili kuendelea kulinda afya za wengine.

Matumizi ya dawa bandia yanatajwa kuathiri zaidi afya ya binadamu. Picha| Daily Nation
Kubainika kwa dawa hiyo bandia kumekuja baada ya taarifa muhimu zinazotakiwa kuwepo kwenye dawa kutokuwepo au kutofautiana na vigezo vilivyowekwa na mamlaka hiyo.
Mathalani, tarehe ya kutengenezwa, namba ya toleo na mwisho wa matumizi ya dawa halisi zipo katika kasha la ndani huku dawa bandia zikikosa taarifa hizo katika kasha la ndani lenye dawa hizo (blister pack). Pia maandishi ya namba ya usajili yaliyochapishwa kwenye kasha la nje la dawa halisi, yaani (secondary pack) yamepangika vizuri katikati ya kasha na maandishi hayo kwenye dawa bandia hayajapangika vizuri.
Karatasi ambatanishi ya dawa halisi (package insert) ina nembo ya Holley-Cotec katika pande zote mbili na ina maelezo ya lugha ya kiingereza na kifaransa huku dawa bandia nembo ya Holley-Cotec kukosekana kwenye upande wa maelezo ya kiingereza
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa rangi halisi ya vidonge ni bluu iliyokolea zaidi na kasha lake la kufungashia vidonge (blister pack) lina ng’aa ambapo rangi ya vidonge bandia kuwa bluu iliyofifia na kasha lake la kufungashia kutokung’aa yaani limefifia.
Namba ya toleo iliyopo kwenye kasha la ndani la dawa halisi inafanana na iliyopo kwenye kasha la nje huku namba hiyo kwenye dawa bandia kwenye kasha la ndani (toleo namba 150644) ni tofauti na iliyopo kwenye kasha la nje (toleoNa.170259).
Latest