Tanzania, Malawi kujenga kituo cha pamoja mpakani Kasumulu
Rais John Magufuli (Kulia) na mwenzake wa Malawi Profesa Arthur Peter Mutharika. Picha|Mtandao
- Kituo hicho kitakuwa kiungo muhimu cha biashara baina ya nchi hizo mbili na kurahisisha shughuli za uhamiaji.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha zinaimarisha na kuendeleza biashara inayofanyika mipakani, Tanzania na Malawi zinakusudia kujenga kituo cha huduma za pamoja katika mpaka wa Songwe/Kasumulu unaotenganisha nchi hizo mbili.
Kituo hicho kwa lugha ya kigeni One Stop Border Post (OSBJT) ni mojawapo ya hatua za kurahisisha biashara na uhamiaji miongoni mwa raia wa nchi zote mbili.
Hatua hiyo imefikiwa jana (Aprili 24, 2019) katika Ikulu ya Lilongwe na Rais John Magufuli na mwenzake wa Malawi Profesa Arthur Peter Mutharika ambapo ujenzi wa kituo hicho ni miongoni mwa maagizo waliyotoa kwa mawaziri wa nchi zote mbili kushughulikia ili kuharakisha shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara na miradi ya maendeleo katika nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, mawaziri hao wametakiwa kuharakisha utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya utalii, usafiri wa anga na kutatua changamoto zinazokikabili Kituo cha Mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center Ltd) kilichopo Jijini Dar es Salaam.
Kituo hicho cha mpakani kitaipa Tanzania fursa kubwa ya kukuza biashara ya mipakani katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Rais Magufuli amesema Tanzania na Malawi zina kila sababu ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika kukuza uchumi wa nchi hizo, kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza zaidi biashara ikilinganishwa na hali ilivyo sasa ambapo biashara kati ya nchi hizo mbili kwa takwimu za mwaka 2018 ilikuwa na thamani ya Sh146.112 bilioni.
Soma zaidi: Rais Magufuli ziarani nchini Malawi
Katika kuhakikisha biashara kati ya nchi hizo mbili inaimarika, Rais Magufuli amesema Tanzania imeendelea kuweka juhudi kubwa za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo kuimarisha bandari ya Dar es Salaam na Mtwara, kujenga bandari kavu na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mbambabay (ushoroba wa Mtwara) ambayo itawawezesha wafanyabiashara wa Malawi kutumia bandari ya Mtwara ambayo iko urnbali mfupi wa kilometa 820.
“Tumeamua kuimarisha bandari ya Mtwara kuiwezesha kupitisha tani 1,000,000 kwa mwaka ikilinganishwa na tani 400,000 za sasa, tunakamilisha barabara ya Mbinga-Mbambabay ili Ndugu zetu wa Malawi msilazimike kupitisha mizigo yenu Dar es Salaam, kwahiyo natoa wito kuwa baada ya mwaka mmoja anzeni kutumia bandari ya Mtwara,” amesema Rais Magufuli.
Ziara ya Rais Magufuli ni ya kwanza katika nchi za Kusini mwa Afrika tangu aingie madarakani mwaka 2015.
Kwa upande wake, Rais Mutharika amesema watendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania ili kuhakikisha nchi hizo mbili zinafaidika na rasilimali zilizopo.
Amesema atahakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa wakati ili kuchochea ustawi wa uchumi wa nchi zote mbili.