‘SMS kwa Maisha’ yazinduliwa kupunguza uhaba wa dawa Zanzibar
- Teknolojia hiyo mpya ya matumizi ya simu inalenga kupunguza uhaba wa madawa na kuboresha afya za watu Zanzibar.
- Utafuatilia mchakato wa usafirishaji na usambazaji wa dawa katika maeneo ya mijini na vijijini.
Dar es Salaam. Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar wataanza kufaidika na maboresho ya huduma za afya, baada ya Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Vodacom Tanzania kufanikiwa kuzindua mfumo mpya wa kufuatilia usafirishaji na usambazaji wa dawa katika vituo vya afya ili kuhakikisha dawa zinakuwepo wakati wote.
Uhaba wa madawa hujitokeza wakati ambapo maduka ya dawa hushindwa kuwa na dawa za kutosha kulingana na mahitaji, hali ambayo husababisha madhara makubwa katika utoaji wa huduma za afya.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika leo Zanzibar ambapo Wizara ya Afya ya Zanzibar, Vodacom Tanzania na kampuni Novartis zitashirikiana kwa kutumia teknolojia iliyoendeshwa na kampuni tanzu ya Vodafone (Mezzanine) na kutoa mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo huo ili kuboresha upatikanaji wa dawa muhimu kwa watu wa Zanzibar.
Utekelezaji wa mfumo huo mpya wa kufuatilia usafirishaji wa dawa utafanyika kupitia programu ya ujumbe wa simu za mkononi unayojulikana kama SMS kwa Maisha (SMS for life) kuwezesha kufuatilia usambazaji wa dawa katika vituo vya afya.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya ya Zanzibar, Harusi Suleiman amesema Programu hiyo itafanikisha kukabiliana na changamoto hiyo kupitia ubunifu wa teknolojia ambao utasaidia taasisi zinazotoa huduma za afya kufuatilia mahitaji na mfumo wa ugavi wa madawa ukianza kutumika Zanzibar.
“Utaboresha zaidi mfumo wetu wa utoaji wa huduma za afya, kuhudumia vizuri wagonjwa na kuboresha maisha,” amesema Suleiman.
Teknolojia hiyo itatumika katika vituo vya afya vilivyopo chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar vipatavyo 190 vya Pemba na Unguja, kuwezesha kupata taarifa ya kila wiki ya mahitaji na matumizi ya dawa na kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kwa wakati katika vituo vya afya kulingana na mahitaji ya wagonjwa wanaowahudumia.
Aidha, Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika inayosimamia Biashara ya bidhaa za Kijamii ya Novartis, Nathan Mulure amesema makubaliano haya ya kufanya kazi pamoja ni mfano mzuri wa sekta ya umma na binafsi kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini.
“Kwa ushirikiano wa pamoja na Vodacom na Mezzanine, tunaweza kuleta mabadiliko chanya kupitia ubunifu wa teknolojia kuhakikisha mfumo wa huduma za afya wa Zanzibar unakidhi matakwa ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kiafya”amesema Mulure.
Uhaba wa dawa huvikumba zaidi vituo vya afya vilivyoko vijiji kutokana na changamoto mbalimbali za usafiri ikiwemo miundombinu mibovu ya barabara.
Lakini Vodacom Tanzania wamebainisha kuwa mfumo huo unaokoa muda na gharama za usafiri kwa sababu taarifa ya mahitaji ya dawa inafika kwa wakati na kuwawezesha wasambaj kuyafikia maeneo yaliyokusudiwa kirahisi.
“Kupitia SMS kwa Maisha vituo vya afya vilivyopo maeneo ya mbali na mjini vitaweza kutoa taarifa ya mahitaji yake ya madawa kwa haraka na kwa ufanisi,” amesema Mkurugenzi wa Biashara kutoka Vodacom, Arjun Dhillon.
SMS for Life ilianzishwa mwaka 2009 na kampuni ya Novartis ikiwa na lengo la kusaidia kuzuia uhaba wa dawa za malaria Tanzania. Lakini kutokana na ufanisi wake ilijitanua kwenye magonjwa na bidhaa zingine.
Kwa sasa SMS for Life imefika maeneo mbalimbali ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya maeneo ya vijijini katika nchi za Afrika kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma na wananchi.