Sh97.1 bilioni kujenga daraja la Jangwani Dar es Salaam
- Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 390 utakamilika baada ya miaka miwili.
Dar es Salaam. Wakazi wa Dar es Salaam wanaotumia barabara ya Morogoro kwenda katikati ya jiji sasa watapata ahueni baada ya Serikali kusaini mkataba wa ujenzi wa daraja kubwa eneo la Jangwani litakalogharimu zaidi ya Sh97 bilioni.
Ujenzi wa daraja hilo la Jangwani katika Mto Msimbazi utapunguza maumivu kwa wakazi wa jiji hilo la kibiashara ambao wakati wa masika hulazimika kupita njia mbadala kutokana na kufurika kwa maji katika eneo hilo linalounganisha Magomeni na Kariakoo.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza leo (Oktoba 22, 2024) katika hafla ya utiaji saini mkataba huo kuwa ujenzi wa daraja hilo umetengenewa Sh97.1 bilioni kutoka Benki ya Dunia na utakamilika baada ya miaka miwili.
Daraja litakalojengwa, kwa mujibu wa Bashungwa, litakuwa na urefu wa mita 390 na barabara za maungio kwa pande zote mbili za daraja zenye jumla ya urefu wa mita 700.

Mchoro unaoonesha mwonekano wa Daraja la Jangwani ujenzi ukikamilika. Picha/TANROADS.
Kwa kawaida eneo hilo la Jangwani hufurika maji na kukata mawasiliano kiasi cha kuathiri huduma za usafiri wa mwendokasi, daladala na magari binafsi ambayo mengi hulazimika kupita barabara mbadala zikiwemo barabara ya Kawawa na Ali Hassan Mwinyi.
Hali hiyo husababisha foleni kubwa ya magari licha ya Serikali kuendelea kuboresha miundombinu katika jiji hilo la kibiashara mwaka hadi mwaka.
Mafuriko hayo mbali na kuathiri huduma za uchukuzi, huathiri pia miundombinu ya huduma ya mabasi yaendayo haraka kikiwemo kituo cha abiria na karakana ya Jangwani.
Ujenzi wa daraja hilo umekuwa ukiahidiwa kwa zaidi ya miaka 10 sasa bila ya utekelezaji huku Serikali ikikosolewa vikali kwa kujenga miundombinu ya mabasi yaendayo haraka eneo hilo bila daraja na miundombinu ya kukabiliana na mafuriko.
“Hizi Sh 97.1 bilioni ni sehemu ya ‘package’ ambayo tumewezeshwa na Mh Rais ya kusaidia mkoa wa Dar es Salaam baada ya athari kubwa za miundombinu zilitokea baada ya mvua za El-nino kutokea,” amesema Bashungwa.
Kigogo, Mkwajuni kujengwa madaraja ya kisasa.
Ujenzi wa daraja la Jangwani unatarajia kwenda sanjari na ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi ambazo humomonyoka wakati wa mafuriko na kujaza mchanga kiasi cha kuongeza athari za mafuriko katika mitaa ya jirani.
Mbali na fedha hizo za kujenga daraja, kuna Sh125 bilioni ambayo ipo kwenye hatua ya mwisho kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja la Kigogo lenye urefu wa mita 50, daraja la Mkwajuni lililopo Kinondoni lenye mita 20.
Madaraja mengine yanayotarajiwa kujengwa kwa kutumia fedha hiyo ni pamoja na daraja la Kisarawe, Amani, Gomvu, Geti jeusi, daraja la Mzinga, mifereji ya maji barabara ya Morocco, Afrikana, Mwenge, Mlalakua, na daraja la Mtongani jimbo la Kawe.
Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja la Jangwani utaenda sambamba na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi kupitia mradi wa uendelezaji wa bonde la mto Msimbazi (DMDP II).
Latest
