Serikali ya Tanzania yazungumzia uvaaji wa barakoa
- Katibu mkuu wizara ya afya asema Serikali haijawahi kuzuia watu kuvaa barakoa.
Mwanza. Serikali ya Tanzania imesema haijawahi kuzuia watu kuvaa barakoa kwa kuwa zinasaidia kujikinga na magonjwa ya mfumo wa hewa na si lazima ugonjwa wa corona pekee.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Mabula Mchembe amewaambia wanahabari jijini Mwanza, waliokuwa wameuliza kuhusu suala la uvaaji barakoa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa covid -19, kuwa ipo miongozo iliyotolewa na wizara ya afya na haijawahi kufutwa.
“Hatujazuia kuvaa barakoa isipokuwa tunataka mtu avae kulingana na eneo lililopo maana si Covid -19 pekee ndiyo inayoambukiza hata mafua pia, kwa hiyo ni vema mtu kujikinga akiwa eneo lolote,”amesema Prof Mchembe.
Amesema kuwa magonjwa yanayotokana na mfumo wa upumuaji ni mengi yakiwemo mafua ya kawaida ambayo nayo huenezwa kwa njia ya upumuaji.
“Serikali ilishatoa mwongozo kuhusu uvaaji wa barakoa uchague wapi uvae na wapi usivae kikubwa ni kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa virusi vinaenea sehemu mbalimbali vinaweza kuwa kwenye nguo ukatembea navyo au kuvishika kwenye mikono,” amesema kiongozi huyo.
Soma zaidi:
- Vigogo walioteka huduma za kifedha simu za mkononi Tanzania
- Jinsi ya kujinasua kwenye upweke, unyonge
Prof Mchembe alikuwa jijini Mwanza kutembelea hospitali za rufaa za Bugando na Sekou Toure kuangalia hali ya wagonjwa wenye matatizo ya upumuaji ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kupima afya mara kwa mara ili kufahamu hali zao.
Profesa Mchembe amesema katika hospitali ya mkoa wa Mwanza, Sekou Toure kuna wagonjwa watano ambao wamelazwa wakiwa na tatizo na upumuaji.
“Niishauri jamii iwe na utaratibu wa kupima afya na wasiwe na hofu kuwa kila ugonjwa wa kushindwa kupumua unatokana na Covid bali wachukue tahadhari,”amesema Prof Mabula.
Uongozi wa hospitali ya rufaa Bugando umesema hospitali hiyo imejipanga kutoa huduma kwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali.
“Hawa wagonjwa wanaofika wenye matatizo ya kupumua, pumu na kisukari wanapatiwa matibabu vizuri kwakuwa wanahitaji mashine za oksijeni za kupumulia,” amesema Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa Bugando, Dk Fabian Massaga.