Serikali kuongeza ushiriki wa wananchi migodini, yawataka kuwekeza uzalishaji wa Kinywe
- Waziri Mavunde asema ushiriki wa wananchi utakuza sekta ya madini
- Awataka kuwekeza katika uzalishaji wa madini ya kimkakati ikiwemo kinywe.
Mwanza. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imedhamiria kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli mbalimbali za madini ikiwemo kuongeza usambazaji wa wa bidhaa migodini.
Waziri wa Wizara ya Madini Anthony Mavunde, aliyekuwa akizungumza kwenye kikao kilichohusisha watoa huduma kwa wamiliki wa leseni za madini, taasisi za fedha, vyama vya wachimbaji wa madini, taasisi za Umma amoja na taasisi za wizara hiyo, amesema dhamira ya Serikali ni kuwaongezea uwezo Wanachi ili kushiriki katika sekta hiyo muhimu.
“Lazima tubadilishe jambo hili, ni eneo ambalo nitalisimamia kwa dhati, vitu vingi bado vinaagizwa nje, tunaweza kuwajengea uwezo watu wetu ili wazalishe ndani na huu ndio utaratibu wetu sisi,” amesema Mavunde Januari 5, 2024 jijini Mwanza.
Pia, kupitia Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri inatarajia kufanya utafiti wa kina wa madini nchi nzima utakaoondoa uchimbaji wa madini wa kubahatisha na kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwemo idadi ya kampuni kubwa za uchimbaji wa madini zitakazopelekea ongezeko la watoa huduma kwenye migodi ya madini, ushiriki wa watanzania na sekta binafsi.
Soma zaidi:Jela miaka 100 kwa kukutwa na meno ya tembo, Mwanza
Madini ya kimkakati kukuza uchumi shindani
Aidha, Waziri Mavunde amewataka wadau wa madini kujipanga kwenye uwekezaji katika madini ya kimkakati kwa kuwa mahitaji yake yanaendelea kuongezeka duniani.
“Mfano mahitaji ya madini aina ya kinywe (graphite) yanatarajiwa kufikia asilimia 500 kwenye uchumi wa dunia ifikapo mwaka 2050 na madini haya tunayo, hivyo ni vyema tukaanza kujipanga kwenda kwenye uchumi shindani.” amesema Waziri Mavunde.
Mbali na kukuza uchumi huenda madini haya kachangia kupunguza athari za mazingira asilimia kubwa kutokana na uwezo wake wa kutengeneza bidhaa zisizoharibu mazingira.
Mbali na kutunza mazingira madini ya Kinywe hutumika kutengeneza thamani mbalimbali za nyumbani.Picha|Earth Magazine.
Rais Samia aliyekuwa anazungumza na wahudhuriaji wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya makubaliano kkati ya Serikali na kampuni tatu za uchimbaji madini April 17, 2023 jijini Dodoma, alisema madini hayo yatavutia wawekezaji wengi kutoka nje.
“Yanatumika kutengeneza mabetri ya magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na mitambo mbalimbali Tanzania tumebarikiwa kuwa na madini haya na inafanya nchi kuangaliwa zaidi na wawekezaji wakubwa zaidi duniani,” alisema Rais Samia.
Kwa mujibu wa Chidiel Mshana, msimamizi wa mgodi wa Lindi Jumbo, unaosimamia ujenzi wa mgodi wa madini ya Kinywe Ruagwa mkoani Lindi, madini hayo yatanza kuchimbwa mwezi Machi mwaka huu na kuwezesha uzalishaji wa tani 40 za madini hayo kwa mwaka.
Mshana alitoa ahadi hiyo wakati akitoa taarifa kwa Waziri wa Madini Anthony Mavunde Disemba 28, 2023 mkoani Lindi.