Sera, sheria jumuishi kumaliza migogoro matumizi rasilimali asilia
- Wadau wa mazingira wamesema sheria zinazosimamia rasilimali asilia zilizopo sasa ni nyingi, jambo linaloteta mkanganyiko katika utekelezaji.
- Serikali yashauriwa kuwashirikisha wananchi ili kuongeza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali hizo.
- Washauri sera na sheria zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili kuongeza uelewa wananchi.
Dar es Salaam. Huenda migogoro ya ardhi na matumizi mabaya ya rasilimali asilia ikapungua iwapo sera na sheria mbalimbali zinazohusiana nazo zitajumuishwa ili kuondoa utata wakati matumizi ya rasilimali hizo.
Kwa sasa Tanzania ina sheria 13 zinazosimamia rasilimali asilia ikiwemo madini, misitu, ardhi, maji ambazo zimekuwa zikiibua migongano ya maslahi wakati wa utekelezaji wake.
Katika kikao cha wadau wa uhifadhi mazingira kilichoandaliwa na taasisi ya Policy Forum kilichofanyika leo (Februari 22, 2019) jijini Dar es Salaam wadau wamependekeza kuwa sheria hizo zinapaswa kujumuishwa ili kuondoa mkanganyiko katika kuzitekeleza.
Mshauri wa masuala ya sheria kutoka taasisi ya Ujamaa Community Resource Team (UCRT), Edward Lekaita amesema uwepo wa sheria nyingi zinazosimamia jambo moja unaleta mkanganyiko na kuzuia wananchi na Taifa kunufaika na rasilimali hizo.
“Mgongano wa sheria na sera imekuwa kizuizi kikubwa katika utekelezaji wa sheria nyingi, na zaidi mkanganyiko huo uliotokana na sheria hizi umetengeneza mkanganyiko mwingine katika masuala ya maslahi, haki, upatikanaji, usimamizi na umiliki wa rasilimali hizo,” amesema Lekaita.
Ameishauri Serikali kuzipitia upya sheria na sera zilizopo ili kutafuta sheria moja itakayosimamia rasilimali asilia ambapo katika mchakato wote wananchi washirikishwe kikamilifu.
Amezitaja baadhi ya sheria zinazosimamia rasilimali asilia ni pamoja na Sheria ya Uhifadhi Wanyama pori ya mwaka 1974 ambayo ilifanyiwa marekebisho na ikaitwa Sheria ya Uhifadhi Wanyama Pori namba 5 ya mwaka 2009; Sheria ya Ardhi ya Kijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999.
Sheria nyingine ni Sheria ya Misitu ya mwaka 2002; Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004; Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya mwaka 2009.
Soma zaidi: Wachimbaji wa madini Geita kupata mkopo kuendeleza rasilimali zao
Kwa mujibu wa Leikata, ambaye pia ni mwanachama baraza la Muungano wa Kimataifa wa Ardhi (ILC Global Council), Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya mwaka 2009 inaruhusu shughuli za kiuchumi kufanyika mita 200 kutoka kwenye chanzo cha maji huku Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ikiruhusu shughuli hizo zifanyike mita 60 kutoka chanzo cha maji.
“Sheria hizi mbili zingejumuishwa ili kuepusha mkanganyiko, uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vya maji,” amesema Wakili huyo.
Tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa nusu ya idadi ya watu duniani wanategemea moja kwa moja rasilimali asilia na nchi zinazoendelea kama Tanzania zinategemea zaidi wanyama pori, maji, misitu kama rasilimali za msingi kuendeleza maisha yao.
Baadhi ya watu walioudhuria kikao cha kujadili matumizi ya rasilimali asilia kilichoandaliwa na taasisi ya Policy Forum leo jijini Dar es Salaam. Picha|Daniel Samson.
Wakati akichangia katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Chambani Pemba, Yussuf Hussein amesema ushirikishwaji wa wananchi katika mabadiliko ya sheria ni muhimu lakini ulenge kuzitafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili ili zieleweke kwa urahisi.
Amesema idadi ya watu inaongezeka na kama hatua za haraka hazitachukuliwa kupima ardhi na kuidhinisha matumizi yake kulingana na makundi mbalimbali katika jamii, migogoro ya rasilimali itaendelea kushamiri katika jamii.
“Tubadilike tuachane na mazoea kwasababu idadi ya watu inaongezeka na ardhi haijapimwa,” amesema Mbunge Hussein.
Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni amesema ikiwa sheria za sasa zitafanyiwa marekebisho zitasaidia kuongeza uwajibikazi na uwazi wa matumizi ya rasilimali asilia na kuwafaidisha wananchi ambao wanategemea kuendesha maisha yao.
Latest
