Safari ya kulipa kisasi inayowaingiza majasusi matatani
- Ni filamu ya ‘Bullet Train’ inayomhusu baba anayesaka kisasi cha mwanae.
- Kufikia azimio hilo, damu ya watu wengi inamwagika.
- Filamu hii itakujibu swali la ulazima wa kisasi maishani mwako.
Jiweke kwenye viatu vya huyu mzazi. Siku moja, anashuhudia mwanae akirudishwa kwa muumba wake tena bila huruma. Na anayefanya hivyo, anakamilisha misheni yake kwa kumsukuma mtoto huyo kutoka juu ya bati la nyumba.
Ewaa!, hasira ambayo unahisi ndiyo anayokuwa nayo Yuichi Kimura ambaye mtoto wake ameuwawa kikatili. Ili kuhakikisha muuaji wake anajiunga kwenye safari aliyoianzisha, anatuma majasusi kwa ajili ya kulipiza kisasi cha damu yake iliyotangulia mbele za haki.
Filamu ya ‘Bullet Train’ inaanza na jasusi Ladybug ambaye amemaliza vipindi vyake na msaikolojia kutokana na kuwa na msongo wa mawazo unaotokana na mlolongo wa matukio yake aliyoyafanya kuhusisha mauaji ya watu hata kama hakuwaua yeye.
Ladybug anapewa kazi moja tu ambayo ni kuiba mkebe ambao unasafirishwa kwa njia ya treni inayoelekea kwenye mji wa Kyoto.
Kuiba tu? Mbona siyo shida kwa Ladybug, Taratibu kama kuchukua peremende kwa mtoto, mkebe unaibwa na Lady Bag lakini safari yake kumbe ndiyo imeanza.
Uhalisi ni kuwa, mkebe huo unatafutwa na majasusi kama wote na wote wapo ndani ya hiyo treni.
Ugomvi wa nani atabaki na mkebe huo unaanza huku majasusi wengine wakiwa na kisasi cha kujilipizia wenyewe kwa majasusi wengine, yaani uhasama ambao unasababisha mmoja baada ya mwingine kuungana na Israeli mtoa roho kurudi walikoumbwa.
Siri iliyopo ni kuwa, mkebe ule ni mali ya White Death ambaye aliwapa kazi majasusi wote waliopo kwenye treni ile bila kujua akiwemo mwanae wa kiume.
White Death anasema, aliwapa kazi hiyo akiwa na matumaini ya wote kuuana kwa sababu kila jasusi aliyepo ndani ya treni isipokuwa Ladybug na Wolf wamehusika na kifo cha mke wake.
Mkebe ule ulikuwa ni mtego wa kuhakikisha uhai wao unarudi ulipotoka.
Kilitokea nini? Tazama filamu hii katika kumbi za sinema zilizo karibu na wewe kujibu maswali yote uliyonayo huku waigizaji “konki” wakionekana tena kwenye skrini yako.
Kutana mastaa kaam Brad Pitt, Aaron Taylor, Joey King, David Leitch na Sandra Bullock katika filamu hiyo ya kusindikiza wikiendi yako.
Latest
