Teknolojia zilizotikisa Tanzania miaka 10 iliyopita
- Teknolojia hizo ni pamoja na simu za mkononi zisizo na vibonyezeo na malipo ya kidijitali.
- Kwa kiasi kikubwa, zimesaidia kuleta maendeleo makubwa kwenye jamii ikiwemo mawasiliano rahisi.
- Hata hivyo, teknolojia hizo zina changamoto zake ikiwemo kupoteza muda na kuchochea matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.
Dar es Salaam. Ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali ni ndoto ya kila mdau wa teknolojia. Nyuma ya ubunifu na uvumbuzi huo kunakuwepo kiu ya kuhitaji kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinaikumba jamii fulani au ulimwengu kwa ujumla.
Miaka 10 yaani kutoka mwaka 2010 hadi 2019 wadau wa teknolojia na wanasayansi wamegundua mambo mengi ambayo kwa namna moja ama nyingine yamechochea maendeleo katika jamii na dunia kwa ujumla.
Uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz unakuletea baadhi ya teknolojia ambazo zimeingia Tanzania miaka tisa iliyopita na jinsi zinavyochangia kuboresha maisha ya Watanzania:
Teknolojia ya malipo kwa “QR code”
Teknolojia hii inafanya kazi kwa kutumia kamera ya simu janja ambayo ina skani msimbo (CODE) na kisha kukamilisha malipo ndani ya muda mfupi.
Teknolojia hiyo, kwa mujibu wa tovuti ya The Asian Banker, ilianzishwa mwaka 2016 ikiwa na lengo la kurahisisha maisha na kupunguza ubebaji wa fedha taslimu ambazo mara kadhaa watu wameripoti kuibiwa.
Baadhi ya wadau wamesema teknolojia hiyo imechochea manunuzi ya holela kwani imempatia mtu fursa ya kutumia fedha zake mahali popote tofauti na awali ambapo zilitumika mashine za kutolea fedha (ATM) ambazo zilimlazimu mtu kwenda kutoa fedha sehemu husika.
Praxeda Mathias ambaye ni mtumiai wa teknolojia hii amesema, “ni teknolojia nzuri lakini tangu nimeanza kuitumia hata hali ya uhifadhi wangu wa fedha imetetereka kwani nina uwezo wa kuitumia mahali popote nionapo kitu kizuri.
Hivi karibuni kampuni ya kimataifa ya Visa yenye makao makuu yake nchini Marekani inayojihusisha na huduma za kifedha ilizindua huduma ya kuskani QR Code hapa nchini Machi 12, 2019 ili kurahisisha malipo ya huduma na bidhaa mbalimbali.
Visa imeungana na taasisi 15 zinazotoa huduma za kifedha zikiwemo benki za CRDB, NBC, NMB, na kampuni ya simu ya Halotel kumpa mteja mawanda mapana zaidi ya kuchagua namna ya kulipa.
Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana katika sheli na maduka ya jumla ya watoa huduma zaidi ya 2,000 nchini.
Mteja anaweza kuskani QR Code kwa kutumia simu janja na kulipia bidhaa na huduma kirahisi |Picha na Rodgers George
Teknolojia za usafiri wa kidijitali
Licha ya kwamba teknolojia imeanza zamani lakini kwa nchi ya Tanzania usafiri wa kidijitali umeanzishwa na kampuni ya kimarekani ya Uber. Nchini Marekani ilianza kutumika mwaka 2009 na kwa Tanzania, imeanza kutumika rasmi Juni 2016.
Baada ya Uber, Taxify/Bolt ilifuatia ikifuatiwa na Little ride na zinginezo ambazo mbali na kurahisisha usafiri, imeondoa ulazima wa kusubiria usafiri wa umma kama una haraka.
Programu hizo (Apps) za Uber na Bolt zinazidi kuwa maarufu kila uchwao katika jiji la Dar es Salaam lenye tatizo la usafiri kutokana na uwepo wa foleni kubwa na uhaba wa daladala hasa nyakati za mahitaji ya juu ya asubuhi na jioni licha ya kuwepo mabasi ya mwendokasi na huduma za treni.
Kutokana na shuruba hizo, Uber and Taxify zimekuwa wakombozi kwa kuwa zinatoa usafiri kwa bei nafuu ikiwa ni nusu ya nauli za taxi za kawaida. Kati ya hizo, Uber imekuwa maarufu kwa sababu ndiyo ilikuwa ya kwanza kufika mwaka mmoja na nusu uliopita.
Zinazohusiana
- Toolboksi ya Tanzania yapenya tuzo za ‘Startups’ bora kusini mwa Afrika
- Mfahamu Given Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu
- Mtanzania atwaa tuzo ya ubunifu nchini Misri
Simu za Samsung Galaxy “S Series”
Licha ya kutoa matoleo kadhaa yenye mfumo endeshi wa Android yakiwemo ya Samsung i7500 kabla ya mwaka 2010, toleo la kwanza la “S Series” ndilo lilikuwa toleo la Samsung lililokusudiwa kushindana na simu za IPhone.
Ni matoleo ya Samsung Galaxy S ambayo yamefungua pazia la simu za Samsung zisizokuwa na vibonyezeo vingi. Galaxy ya kwanza yaani Samsung galaxy S1 ilikuwa na kibonyezeo kimoja tu endapo vile vya kuwasha na sauti havitohesabiwa.
Fahamu kwamba, Galaxy S1 ambayo ilitolewa rasmi Juni, 2010 pamoja na S2 na S3 ziliweza kuuza hadi kufikia takribani mauzo ya simu milioni 100 hadi 2013 na hivyo kuleta ushindani mkubwa wa kibiashara kati yake na simu za IPhone zinazotengenezwa na kampuni ya Apple ya Marekani.
Hadi sasa, simu za Samsung toleo la S series zimefikia toleo la S10 kwa mwaka 2019 orodha ambayo ilianza na S1.
Simu hizi zimesaidia sio tu kurahisisha mawasiliano bali kusogeza teknolojia nyingine karibu kwani zimeambatana na redio, tochi, muziki na vinginevyo vikiwemo kamera na kinasa sauti.
Ili kuzipata simu hizo hasa Galaxy S10, lazima mfuko wako uchanike kidogo kutokana na gharama kubwa inayotokana ma uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi vitu na teknolojia iliyotumika katika kuitengeneza ikiwa ni ya juu kuliko matoleo yaliyopita.
Simu za I phone
Huwezi kuongelea Samsung na kusahau iPhone kwani wakati Samsung ikitambulisha simu zao za S series, iPhone waliingiza simu aina ya iPhone 4s mnamo Juni 2010 ambapo kwa mujibu wa tovuti ya tecnobezz, iPhone 4s pekee imeuza zaidi ya simu milioni 60 kufikia Septemba 2019.
Mbali na 4s, iPhone Imekuwa mshindani mkubwa wa Samsung kwani hadi kufikia 2019, simu zake zimefikia toleo la 11 (Iphone 11).
Matoleo mengine ya kampuni ya kiteknolojia ya Apple ni pamoja na iPhone 5, iPhone 6, iPhone 10 ambazo mbali na kusaidia mawasiliano, kama Samsung zimesogeza karibu teknolojia ya intaneti, tochi, televisheni na nyinginezo ikiwemo teknolojia ya ramani za kidijitali.
Hata hivyo, baada ya makampuni haya kuchuana vilivyo kwenye uzalishaji wa simu janja makampuni mengine yameibuka na kuungana nayo kwenye mashindano hayo yakiwemo Huawei, Tecno, HTC na mengine mengi kama Motorola.
Ushindani huo, unawapa Watanzania kuwa na machaguo mbalimbali yanayokidhi mahitaji yao ya kikazi, kibiashara na kijamii.
iPhone Imekuwa mshindani mkubwa wa Samsung kwani hadi kufikia 2019, simu zake zimefikia toleo la 11 (Iphone 11). Picha|Unsplash.
Mafunzo ya mtandaoni
Kabla ya mwaka 2010 katika nchi yetu, masomo ya ziada (tution) ilikuwa ni mpango mzima kwa kujifunza nje ya shule. Watoto pia walilazimika kusubiri umri wa shule ili kujifunza lakini teknolojia imekuja na programu tumishi zikiwemo Ubongo Kids na Shule Direct.
Programu hizo zimesaidia wanafunzi kujifunza mahali popote walipo na kurahisisha upatikanaji wa maarifa na ujuzi, licha ya kuwa utumiaji wake unahitaji usimamizi wa wazazi ili kuwaepusha wanafunzi na athari za mtandaoni.
Baada ya teknolojia hizi kuwa sehemu ya kuboresha maisha ya Watanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu na usafiri, ni teknolojia gani zitavumbuliwa na kubuniwa mwaka ujao wa 2020?
Siyo tu wanafunzi, hata upatikanaji wa taarifa na habari umekuwa mrahisi zaidi kwa sasa, watu hawana ulazima wa kusoma magazeti, kuangalia televisheni au kusikiliza redio nyumbani.
Kwa kutumia simu janja, wanapata kila kitu katika viganja vyao, jambo linalosaidia kuondoa pengo la upatikanaji wa taarifa muhimu za jamii kwa wakati.
Hata hivyo, ukuaji wa teknolojia ya upatikanaji wa taarifa, umeathiri utendaji na mapato ya vyombo vya habari vya asili. Vyombo hivyo havina namna tena, zaidi ya kukumbatia mabadiliko hayo ili viendelea kutoa huduma na kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa.
Watoto pia walilazimika kusubiri umri wa shule ili kujifunza lakini teknolojia imekuja na programu tumishi zikiwemo Ubongo Kids na Shule Direct. Picha| Economydirect.