RC Mwanza aagiza haki itendeke ulipaji fidia ujenzi reli ya kisasa

August 2, 2021 8:15 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Aiagiza TRC kulipa fidia stahiki kwa wananchi watakaochuliwa maeneo yao.
  • Ni wale watakaopitiwa na kipande cha Mwanza hadi Isaka.

Mwanza. Wakati ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga ukianza, Serikali imeitaka timu ya wataalam wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya tathmini nzuri ya maeneo itakapopita reli hiyo ili kutokuacha maumivu kwa wananchi.

Kipande hicho cha tano ni sehemu ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka mkoani Dar es Salaam hadi mkoani Mwanza, kwa mujibu wa TRC, kipande cha kwanza ilikuwa ni Dar  es Salaam – Morogoro, kipande cha pili (Morogoro-Makutupora), kipande cha tatu (Makutupora-Tabora), kipande cha nne ( Tabora – Isaka) na kipande cha mwisho ni Isaka-Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert  Gabriel aliyekuwa akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kampeni ya uelewa kwa wananchi watakaopitiwa na reli hiyo jijini Mwanza,  ameiagiza TRC kuhakikisha  wanazingatia vigezo vya kulipa fidia kwa wananchi  wanaoishi maeneo  yatakayoguswa na mradi juo.

Amesema umakini katika tathmini utasaidia kuepusha migogoro chonganishi na kutia doa mradi huo. 

“Wote watakaoguswa maeneo yao ulipaji wa fidia utakuwepo,  na nitoe onyo kwa wataalam kuzingatia uadilifu na wapime sawa sawa na vigezo na fidia itolewe kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo bila kumdhurumu mtu,” amesema Gabriel.

Wananchi ambao watapata changamoto yoyote wakati wa zoezi la upimaji maeneo yao, wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao katika ofisi ya mkuu wa mkoa huo.

Mtaalam wa masuala ya kijamii wa mradi huo,  Lightness Mdulu amesema katika suala la fidia hakuna mwananchi atakayepunjwa au kuonewa kwa sababu zoezi  hilo litafuata sheria na taratibu zote za kitaifa.

Reli hiyo ya kisasa itakuwa na urefu usiopungua kilomita  2,561 ikiunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zinazokuwa na bandari za Rwanda, Burundi na Congo DRC.

Ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha tano ulizinduliwa Juni 14 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan  katika kijini cha Fella wilayani Misungwi mkoani hapa. 

Tayari mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni kampuni za Yapi Markes na Motaengel Africa ameshaanza kazi katika vijiji mbalimbali kwa kujenga nyumba za kulala watumishi. 

Kuanza kwa mradi huo kutatoa ajira za moja kwa moja 11,000 na zingine zisizo za moja kwa moja. 

Katika ajira hizo, Gabriel ametoa angalizo kuhakikisha wanaajiri watu wanaopatikana kwenye mradi husika na si kutoa watu nje ya Mwanza. 

Enable Notifications OK No thanks