Rais Samia ataka viongozi wapya kusimamia mabadiliko, kujiandaa na uchaguzi 2024
- Watakiwa kusimamia utekelezaji wa mipango iliyowekwa kutimiza ahadi za Serikali
- Waziri Mchengerwa apongezwa kwa kasi na utendaji mzuri
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wateule walioapishwa kufanya kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya na kuhakikisha utimizaji ahadi za Serikali kwa wananchi kuelekea kipindi cha uchaguzi mwakani.
Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mwaka 2024, ambao hutangulia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais ambao utafanyika 2025.
Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha viongozi wateule Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Septemba 01, amehimiza viongozi hao, kuhesimu viapo vyao na kuzingatia utekelezaji wa falsafa ya R4 inayohusisha mabadiliko ili kutayarisha njia ya mafanikio ya chaguzi zinazokaribia.
“Mabadiliko haya ni marekebisho, maendeleo lazima yawe na bandika bandua…tunachotaka ni mabadiliko tunayowaahidi watu, tunaahidi mambo mengi, twendeni tubadilikeni, ” amesema Rais Samia.
Soma zaidi
-
Rais Samia afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri, afuta na kuunda wizara mpya
-
Rais Samia atoa wito ushiriki wa wananchi Dira ya Maendeleo 2050
Aidha Rais Samia amewataka viongozi waliapishwa leo kumtumia aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mohamed Mchengerwa kama mfano katika kuleta mabadiliko chanya kwenye maeneo yao ya kazi.
“michezo kaenda kazi aliyofanya mmeiona, kaacha kazi nzuri sana. Nimempeleka utalii mipango aliyoiweka sekta ile inakwenda kupanda, sasa nimempeleka Tamisemi mwakani kuna kivumbi, najua unaweza, ni kazi kazi ili mwakani tuuze vizuri,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amesisiza viongozi wateule kufanyia kazi kero za wanachi ikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Serikali.
Uapisho huu ni baada ya mabadiliko yaliyofanyika Agosti 30, 2023 ambapo mara baada ya kupita miaka 29, Rais amerejesha nafasi ya naibu waziri mkuu ambapo pia aliwateua mawaziri wanne, manaibu waziri watano, makatibu wakuu watatu na naibu makatibu watatu na kuwabadilisha wizara baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu.
Latest



