Neuralink kuja na teknolojia itayowawezesha vipofu kuona

September 18, 2024 6:23 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Kifaa hicho cha majaribio kitawasaidia vipofu kuona kwa kutumia teknolojia ya vipandikizi vya ubongo na miwani maalum.

Dar es Salaam. Huenda watu wenye ulemavu wa macho duniani wakaondokana na changamoto hiyo siku za usoni mara baada ya kampuni ya Neurolink ya nchini Marekani kupewa kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya nchi hiyo (FDA) kitakachowezesha utengenezaji wa kifaa tiba cha majaribio kiitwacho ‘Blindsight’ kinachotarajiwa kuwapa uoni mamilioni ya vipofu duniani.

Kupitia mtandao wa X kampuni hiyo imethibitisha kupokea kibali hicho kutoka FDA ambapo utengenezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni na kuwafikia walemavu wa macho katika maeneo mbalimbali duniani.

Blindsight ni teknolojia iliyoundwa kuwasaidia watu ambao ni vipofu kabisa tangu wamezaliwa au kupata ajali ambapo hufanya kazi kama mbadala wa sehemu za macho zilizoathirika ikiwa sehemu ya ubongo inayohusika na kuona (visual cortex) bado inafanya kazi.

Mfumo huu unahusisha kuweka kifaa kidogo ‘microchip’ ndani ya ubongo ambacho huwasiliana na kifaa chenye mfano wa miwani kitakachovaliwa na mtu asiyeona kisha huchakata na kufasiri taarifa zilizopo kwenye taswira kwa wakati halisi.

Kifaa tiba hicho kimepewa hadhi maalum iitwayo ‘Breakthrough device designation’ kutokana na kurahisisha na kuharakisha mchakato wa ukaguzi na kibali cha kifaa tiba ili kiweze kuzalishwa na kufikia wagonjwa haraka. 

FDA hutoa hadhi hii baada ya kuona matokeo ya awali ya kliniki yanayoonyesha kuwa kifaa tiba au dawa iliyochunguzwa inaweza kuwa bora zaidi kuliko matibabu yanayopatikana hivi sasa.

Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X, mmiliki wa kampuni hiyo Elon Musk amesema kuwa teknolojia hiyo itaboreshwa kufikia uwezo bora wa kuona kuliko wa asili unaotumiwa na watu ambao si vipofu.

Hata hivyo, Neuralink haijatangaza bei rasmi ya kifaa hiki, huenda majaribio yake yakikamilika kikauzwa kwa bei ya juu zaidi kutokana na teknolojia ya kisasa inayotarajia kutumika.

Mfano wa teknolojia ya ‘Blindsight’ inayotarajiwa kuwasaidia watu wenye upofu kuwa na uwezo wa kuona. Picha l Akili mnemba

Upandikizaji kwenye ubongo

Mbali na ‘Blindsight’, Neuralink imefanya pia utafiti wa kuunda teknolojia nyingine ambazo zinaweza kusaidia watu wenye matatizo kwenye mifumo ya fahamu yakiwemo ya kupooza na unyogofu.

Kampuni hiyo imetengeneza kifaa chenye mfumo ulioundwa kutafsiri mfumo wa famahu wa binadamu ili aweze kutumia kompyuta au simu janja bila ulazima wa kutumia viungo vya mwili hususan mikono.

Majaribio ya mfumo huo yaliyotangazwa Januari 30, 2024 yalijumuisha watu wenye umri wa miaka 22 na zaidi ambao wanaishi na hali ya kupooza kwa viungo ‘quadriplegia’ kutokana na jeraha la uti wa mgongo au ugonjwa wa ‘amyotrophic lateral sclerosis’ (ALS) ambao huondoa uwezo wa mtu kudhibiti mwili wake.

Mafanikio ya teknolojia hii yataleta ahueni zaidi na kuboresha maisha ya watu wenye majeraha ya uti wa mgongo au matatizo mengine ya mfumo wa fahamu kama vile kuwasaidia watu waliopooza kudhibiti viungo vyao vya bandia au kutumia kompyuta kwa kutumia fikra zao.

Aidha, Neuralink pia imelenga  kutibu magonjwa ya Parkinson’s, kifafa, na unyogovu ‘depression’ kwa kutumia teknolojia inayoitwa ‘brain-computer interface (BCI)’ inayohusisha kupandikiza vifaa vidogo moja kwa moja kwenye ubongo ili kurekodi na kuchochea shughuli maalum za neva, hivyo kuruhusu kudhibiti sehemu za ubongo zinazohusiana na magonjwa haya. 

Mfumo huu hukusanya ishara za umeme kutoka kwenye ubongo kwa kutumia vifaa maalum kama vile elektrodi ambavyo hupandikizwa moja kwa moja kwenye ubongo kwa ufanisi zaidi, ishara zilizokusanywa hutafsiriwa na programu maalum ili kuelewa nia ya mtumiaji, baada ya hapo mfumo huo hutuma amri kwenye kifaa kilichounganishwa iwe ni kompyuta au kiungo bandia ili kutekeleza matendo yaliyokusudiwa na mtumiaji.

Enable Notifications OK No thanks