Namna unavyoweza kuchunguza afya ya betri ya simu yako
- Ni pamoja na kuangalia taarifa za betri zilizopo kwenye simu.
- Chunguza mzunguko wa matumizi ya simu na kutumia programu maalum.
- Usipozingatia uchunguzi huo unaweza kupata madhara ya simu kujizima au kulipuka.
Dar es Salaam. Kila mara unaponunua simu jambo la kwanza kuangalia huwa ni kamera au muonekano wa nje lakini je umeshawahi kuchunguza afya ya betri la simu kabla hujatoboa mfuko wako?
Kwa watumiaji wa simu za iPhone na baadhi ya simu zinazotumia mfumo endeshi wa Android watakubaliana na mimi kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo wakati wakitumia simu hizo ni uwezo wa betri kutunza chaji kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Apple Store, afya ya betri humuwezesha mtumiaji kutumia simu bila kuhofia kuishiwa chaji hata akiwa mbali na umeme.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Coxstore, Constantine Madalali anasema kuchunguza afya betri ya simu inayotaka kununua kunaweza kusaidia kujua ikiwa simu ni mpya au umeuziwa iliyotumika.
“Kwa kawaida kadri unapoitumia simu ndipo uwezo wake wa kukaa na chaji au afya yake hupungua na inaweza kufanya simu ishindwe kufanya kazi kama ilivyokuwa mpya,” anasema Madalali ambaye ni mtaalam wa masuala ya kompyuta.
Madalali anasema kwa sasa sokoni kuna simu nyingi za iPhone zilizotumika na mtu asipikuwa makini kujikuta ameuziwa iliyotumika wakati alikuwa anataka kununua mpya.

Uchunguzi makini wa taarifa zilizopo kwenye simu yako unaweza kukuepusha na kununua simu feki au iliyokwisha kuharibika.Picha Apple store.
Ili kufurahia matumizi ya simu yako ukiwa huna hofu ya chaji kuisha kabla ya wakati, njia zifuatazo zitakusaidia kufanya uchunguzi wa betri la simu kabla hujatoa fedha kumpa muuzaji:
1.Angalia taarifa za afya ya betri kwenye simu yako
Simu za iPhone na zile za Android zina mfumo kukuwezesha kuangalia hali ya betri ya simu hata kabla haijaanza kutumika.
“Ukikuta afya ya betri (battery health) ipo chini ya 100 basi ujue simu unayotaka kununua imeshatumika,”amesema ngeza Madalali.
Unachotakiwa kufanya ni kuingia kwenye “setting”, chagua kipengele cha betri kisha battery health (afya ya betri) hapo unaweza kuona asilimia za afya ya betri lako.
Ikiwa unanua simu mpya hakikisha asilimia ya afya ya betri ipo 100.
2.Chunguza mzunguko wa matumizi ya betri yako
Mzunguko wa matumizi ya betri ni kipengele muhimu unachoweza kuzingatia wakati ukifanya uchunguzi wa afya ya betri.
Kwa mujibu wa tovuti ya Apple store, mzunguko wa matumizi ya betri ni muda ambao kifaa hufanya kazi kabla ya kuhitaji kuchajiwa upya. Mzunguko huo huhesabiwa kila wakati unapochaji simu kutoka asilimia 0 mpaka 100 na kuitumia kutoka 100 mpaka 0.
Apple wanasema betri ya kawaida inatakiwa kuwa na mizunguko 500 ikiwa ni hesabu za matumizi mpaka kuichaji tena. Hii inamaanisha uwezo wake wa kutunza chaji hautakiwi kuwa chini ya asilimia 80.
Jambo la kufurahisha ni kwamba unaweza kuchunguza mizunguko hii ya matumizi yako mwenyewe na ukajua hali halisi ya betri lako kama ilivyoeleza Madalali
3. Tumia programu ya 3u Tools
Program hii inayopatikana kwenye kompyuta imeundwa kuwawezesha watumiaji wa IOS kutazama na kudhibiti faili na data za vifaa vya vya iOS ikiwemo simu, kompyuta za mezani na kompyuta mpakato.
Ukiwa na program hii pia ni rahisi kuona afya ya betri la simu yako ikiwa ipo sawa au utahitajika kununua lingine. Unachotakiwa kufanya ni kuingia kwenye program hiyo na kufuata maelekezo yatakayokuwezesha kupata taarifa unazozitaka.
“Programu hii inakuonyesha taarifa zote za simu yako ikiwa wamebadilisha chochote, iwe ni kamera au betri utakuta tu ujumbe ‘it might have been changed’ ikiashiria uwezekano wa vifaa hivyo kubadilishwa,” ameongeza Madalali.
Soma zaidi
-
Hakuna siri tena: Ifahamu ndege inayoweka wazi yaliyojificha ndani ya nyumba
-
Benki Kuu yatahadharisha udanganyifu wa fedha mtandaoni
Madhara ya kutofanya uchunguzi wa afya ya betri la simu
Ikiwa umenunua simu bila kuzingatia afya ya betri unaweza kukutana na madhara mengi ambayo yanaweza kudhoofisha utendaji kazi wa simu yako.
1#. Simu kujizima bila sababu
Kwa kawaida simu inatakiwa ijizime endapo umeitumia mpaka asilimia moja, juu ya hapo yanii kuanzia tano, 10 au 20 ni kiashiria tosha kuwa ulinunua simu yenye betri ambayo afya yake haikuwa vizuri au imekwisha kutumika sana.
“Unakuta simu ina asilimia 50 alafu inazima, wakati kwa kawaida ungeweza kutumia kwa masaa kadhaa, hapo ujue tu betri halipo sawa,” amesema Madalali.
2#. Kulipuka kwa simu kusikotarajiwa
Usipozingatia afya ya betri la simu unayonunua basi ujue unajiweka kwenye hatari ya kulipukiwa na simu.
“Simu imetengenezwa na betri aina ya Lithium-ion ambayo ipo reactive na inaweza kulipuka wakati wowote ikiwa itakutana na voti za umeme ambazo hazipo sawa. Mara nyingi simu kama hizo ukibadilisha betri hayo matatizo na madhara yote huondoka,” amesema mtaalam huyo wa vifaa vya kielektroniki anayepatikana jijini Dar es Salaam.

Latest