Mwelekeo mpya uzalishaji makaa ya mawe Tanzania
- Serikali yazindua kiwanda cha nishati hiyo Dar es Salaam.
- Kitasaidia kupunguza ukataji wa miti na gharama za maisha.
Mwanza. Shirika la Taifa la Madini (Stamico) limeanza uzalishaji wa makaa ya mawe ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na matumizi ya mkaa na kuni.
Nishati hizo zimekuwa zikichochea ukataji wa miti ambao umekuwa ukichangia ukame, kupungua kwa mvua, ongezeko la gesijoto ambazo zimekuwa na athari hasi kwa viumbe hai na binadamu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa shirika hilo amesema shirika lina mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa kutosha wa makaa ya mawe ili kukidhi mahitaji ya Watanzania.
Tayari Stamico imeagiza mitambo miwili yenye uwezo wa kuzalisha tani 20 za makaa ya mawe, ambayo yamezua mjadala mpana duniani kama ni nishati mbadala kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dk Mwasse amesema, mradi huo unatarajia kuwanufaisha Watanzania kwa kutoa ajira na utapunguza janga la ukataji miti kwa ajili ya mkaa hivyo kuchangia kutunza mazingira.
“Kwa sasa Stamico imeanza kusambaza nishati hiyo ambayo ni nafuu zaidi na rafiki kwa mazingira baada ya kuidhinishwa na Shirika la Viwango la Taifa (TBS) tayari kwa matumizi baada ya uzalishaji wa majaribio kufanyika kwa ufanisi,” amesema Dk Mwasse
Dk Mwasse amesema mkaa huo una faida lukuki ikiwa ni pamoja na rafiki wa mazingira, kuokoa pesa nyingi zinazotumika kwenye nishati nyingine.
Mkaa wa mawe wa kupikia unadumu jikoni kwa muda mrefu kuliko mkaa wa miti hivyo kuzidi kupunguza gharama za matumizi ya nishati hiyo, huboresha usafi wa jikoni na maeneo ya nyumbani yanayochafuliwa na mkaa wa miti.
Pamoja na mambo mengine, Dk Mwasse amesema, misitu ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai kwa kuwa huifadhi vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, malisho ya mifugo, kuboresha shughuli za kilimo na kuboresha mandhari ya nchi mijini na vijijini.
Amewataka Watanzania kuunga mkono matumizi ya makaa hayo ambayo matumizi yake ni rahisi na hupika kwa haraka zaidi na yana faida nyingi kuliko mkaa wa miti ambao athari zake kimazingira ni kubwa.
Stamico inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa jamii kubwa inanufaika na inatumia mkaa huo ambao ni wazi utasaidia kufanikisha kampeni ya utunzaji wa misitu.
Makamu wa Rais Dk Philip Isidor Mpango anatarajiwa kuuzindua rasmi mkaa huo Agost 12, 2022 ili uanze kutumika rasmi na Watanzania wote.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Dk Doto Biteko amepongeza jitihada na ubunifu unaofanywa na shirika hilo.
Dk Biteko ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala wa kupikia unaojulikana kama “Rafiki Coal Briquettes” unaotokana na makaa ya mawe kilichopo jijini Dar es Salaam.
Waziri amesema Stamico imeagiza mitambo mipya 11 kwa ajili ya uchorongaji na mitambo 4 kwa ajili ya kuzalisha makaa ya mawe ili kuongeza uzalishaji wa makaa hayo na kukidhi mahitaji ya watanzania ambapo mitambo hiyo itasimikwa jijini Dodoma, Songwe, Pwani na Kanda ya Ziwa.
Latest
