Mkombozi Bank yapata bosi mpya
- Ni kigogo aliyewahi kufanya kazi katika benki za NMB, Exim na Standard Chartered.
- Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Edwina Lupembe aliyestaafu.
Dar es Salaam. Sekta ya benki nchini imempokea bosi mpya, baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya biashara ya Mkombozi kumteua George Shumbusho kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya kuanzia kuanzia Desemba mosi, 2017.
Shumbusho, ambaye ni moja ya watu maarufu katika sekta hiyo ya fedha, anachukua nafasi ya iliyoachwa wazi na Edwina Lupembe aliyestaafu Desemba 31 mwaka jana baada ya kuhudumu benki hiyo tangu Agosti 2009.
Edwina alikuwa moja ya vigogo wachache wanawake katika sekta ya benki nchini akiwa sambamba na wenzie kama Ineke Bussemeker wa NMB, Jacqueline Woiso wa Bank M na Mwanahiba Mzee wa Eco Bank.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Menejimenti ya Bodi katika vyombo vya habari leo, Januari 24, 2017 imemshukuru Lupembe kwa kazi yake nzuri ya mfano aliyoifanya katika miaka minane aliyoongoza benki hiyo iliyooanzishwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) mwaka 2009.
“Bodi ina imani kuwa mkurugenzi mpya atatumia uzoefu wake wa kitaaluma kwa kufanya kazi karibu na wafanyakazi wa benki, Bodi na wadau wengine katika kuindeleza benki yetu wakati wa uongozi wake,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kabla ya uteuzi huo mpya katika benki hiyo inayotoa huduma za mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, Shumbusho alishawahi zitumikia benki kubwa nchini zikiwemo Exim Bank, Stanbic Bank, Standard Chartered na NMB.
Shumbusho mwenye shahada ya uzamili ya biashara (MBA) kutoka Shule ya Usimamizi wa Biashara ya Maastricht nchini Uholanzi, ni mtaalamu wa masoko na huduma za kibenki.
Kigogo huyo anaingia kuiongoza benki hiyo katika kipindi ambacho sekta ya benki inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 9.1 Septemba 2016 hadi asilimia 12.5 Septemba, 2017, kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango. Mwenendo huo umekuwa ukitishia mustakabali wa benki nyingi nchini hususan zenye mitaji midogo.
Mkombozi Bank ni moja ya benki muhimu kwa ukuzaji wa biashara nchini kutokana na kutoa huduma za mikopo ya vikundi, kilimo, biashara, vifaa na uwekezaji na mikopo inayotokana na dhamana ya mishahara.