Mikoa minne yang’ang’ania pale pale matokeo kidato cha sita
- Mikoa hiyo ni Tabora, Simiyu, Kagera na Mjini Magharibi ambayo hufaulu wake kimkoa haujabadilika kwa miaka miwili mfululizo.
- Mkoa wa Mjini Magharibi bado unafanya vibaya, licha ya kubaki palepale.
Dar es Salaam. Ni zaidi ya siku tatu tangu Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya kidato cha sita na kutoa orodha ya mikoa iliyofanya vyema na vibaya katika mitihani hiyo, lakini ipo mikoa ambayo matokeo yake hayajabadilika ikilinganishwa na mwaka 2018.
Uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz umebaini mikoa minne ya Tabora, Simiyu, Kagera na Mjini Magharibi wa Visiwani Zanzibar imebaki katika nafasi ilizoshikilia katika matokeo ya mwaka jana.
Kwa mujibu wa mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha sita 2019 uliotolewa na Necta unaonyesha kuwa mkoa wa Tabora umeendelea kung’ang’ania nafasi yake ya nane kitaifa mwaka 2019 kama ilivyokuwa mwaka jana.
Katika matokeo ya mwaka huu, licha ya mkoa huo kubaki nafasi yake ya nane, umeingiza shule moja ya Tabora Boys kwenye shule 10 bora kitaifa ambapo shule hiyo imeshika nafasi ya tano baada ya kupanda kutoka nafasi ya 15 mwaka 2018.
Mkoa wa Simiyu ambao umekuwa ukifanya jitihada mbalimbali za kuinua elimu kupitia makambi ya kitauluma nao umefanikiwa kung’ang’ania nafasi yake ya 10 kwa mwaka wa pili mfuluizo kutoka nafasi ya 26 iliyopata mwaka 2017.
Simiyu imefanikiwa kuongeza ufaulu wake kutoka asilimia 98.58 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 99.7 ambapo wanafunzi waliopata daraja sifuri kimkoa wamendelea kupungua hadi kufikia wa tatu ukilinganisha na 14 wa mwaka 2018.
Mkoa wa Kagera nao umebaki katika nafasi ya 14 kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo kwa mujibu wa takwimu za Necta, mkoa huo umeshindwa kurudi katika nafasi yake ya tisa iliyoshikilia mwaka 2017 na iliyoifanya uwe katika orodha ya dhahabu ya mikoa 10 bora kitaifa.
Zinazohusiana:
Hata hivyo, mkoa huo umepata faraja baada ya kufanikiwa kuingiza shule ya Kemebos katika orodha ya shule 10 bora kitaifa ambapo imeporomoka kutoka nafasi ya tatu iliyoshika mwaka 2018.
Pia mkoa huo umefanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata daraja sifuri kutoka 34 mwaka 2018 hadi 14 mwaka huu.
Lakini kwa mkoa wa Mjini Magharibi, hali bado tete baada ya kuendelea kung’ang’ania katika nafasi ya pili kutoka ya mwisho kitaifa kwa miaka miwili mfululizo. Katika matokeo ya mwaka huu mkoa huo umeshika nafasi ya 27 kati ya mikoa 29 iliyofanya mitihani ya kidato cha sita mwaka huu.
Kwa matokeo hayo, Mjini Magharibi imeongoza kwa kuingiza shule nne kati ya shule 10 za mwisho kitaifa ukifuatiwa na mkoa wa Mara uliongiza shule tatu.
Mikoa hiyo minne itaendelea kung’ang’ania katika nafasi zake ilizoshikilia miaka miwili mfululizo au itafanya maajabu kwa kuongeza ufaulu na kuingia katika orodha ya dhahabu ya mikoa 10 kitaifa mwaka 2020?