Mfahamu Mtanzania Abdulrazak Gurnah aliyeshinda tuzo ya Nobel
- Ni mzaliwa wa Zanzibar ambaye alienda kuishi Uingereza tangu 1960.
- Ameandika riwaya 10 na hadithi fupi mbalimbali.
- Anakuwa Mtanzania wa kwanza kupata tuzo hiyo.
Dar es Salaam. Ni Abdulrazak Gurnah (73) ambaye ni mwandishi wa riwaya kutoka Zanzibar anayeshika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo ya Nobel katika fasihi 2021.
Gurnah ambaye asili yake ni Zanzibar, kwa sasa ni mkazi wa nchini Uingereza ambako aliwasili kama mkimbizi katika mwishoni mwa mwaka 1960.
Hadi sasa mwandishi huyo ameandika riwaya 10 na hadithi fupi zikiwemo ‘Paradise’ na ‘Desertion’, kazi ambazo zinazungumzia athari za ukoloni na hatma ya wakimbizi katika ghuba baina ya tamaduni na mabara.
Huenda Gurnah anaishi ndoto ya mhusika wa kwenye riwaya ya ‘Paradise’ aliyoandika mwaka 1994 ambayo ilikuwa inazungumzia hadithi ya mvulana aliyekulia nchini Tanzania mapema mwanzoni mwa karne ya 20 na kushinda tuzo ya mwandishi wa kitabu.
“Kujitolea kwa Abdulrazak Gurnah kuangazia ukweli na kutopenda urahisishaji ni jambo lililovutia na kufurahisha,” Kamati ya Nobel kitengo cha fasihi imesema katika taarifa yake.
Riwaya zake zimeangazia kuanzia ubaguzi, ufafanuzi wa ubaguzi wenyewe huku akitumia kazi zake kuitangaza Afrika Mashariki ambayo wengi katika maeneo mengine ya dunia hawaifahamu.
Tuzo hiyo ambayo hutolewa na taasisi ya Sweden ya Nobel ni mahususi kwa mtu ambaye atakuwa amechapisha kazi bora zaidi ya fahisi katika mrengo madhubuti.
Kabla ya kustaafu, Gurnah alikuwa profesa wa Kiingereza na fasihi. Picha| Vibes of India.
Gurnah avunja rekodi
Kwa waandishi wa fasihi wenye asili ya Afrika, Gurnah anaungana na malijendi wa fasihi wakiwemo Wole Soyinka wa Nigeria aliyesinda tuzo hiyo mwaka 1986 na Naguib Mahfouz kutoka Misri aliyetwaa tuzo hiyo mwaka 1988.
Gurnah anakuwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kushinda tuzo hizo za heshima kwa ueledi wa kazi za fasihi huku akijizolea kitita cha Sh2.6 bilioni
Gurnah amewahi kufanya kazi kama Profesa wa Kiingereza na fasihi baada ya uhuru katika Chuo kikuu cha Kent, Canterbury nchini Uingereza ambapo kwa sasa ni mstaafu.
Latest