Maujanja yatakayowabeba vijana mahali pa kazi
- Wameshauriwa kuwa wavumilivu na watatuzi wa changamoto na mazingira yasiyoridhisha ya kazi.
- Mawasiliano na mahusiano mazuri na waajiri wao ni kete nyingine itakayowaweka kazini muda mrefu.
Dar es Salaam. Malengo ya kila kampuni au shirika ni kukua na kupata wafanyakazi wanaoweza kuendesha kampuni vizuri kupitia ujuzi na maarifa waliyonayo ili kuongeza ufanisi katika kazi mbalimbali ndani ya kampuni.
Pamoja na malengo hayo, huenda ikawa vuta nikuvute kati ya mabosi na waajiri pale malengo hayo yanapokwama kutokana na baadhi ya wafanyakazi kushindwa kutumiza wajibu wao.
Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao kibarua chako kinatishiwa kuota nyasi kwa sababu tu umeshindwa kutimiza malengo ya kampuni, usijali kwa sababu unaweza kubadili hali ya mambo kwa muda mfupi.
Zingatia mambo haya unapokuwa kazini ili kuhakikisha unakua kitaaluma na mwajiri wako aendelee kukuamini na kuifanya kampuni izalishe faida iliyokusudiwa:
Jifunze kufanya kazi kulingana na mazingira uliyopo. Hii inahusisha kuwa tayari na hali yoyote inayoweza kutokea ndani ya kampuni wakati wowote. Tumia ujuzi wako kulifanya eneo la kufanyia kazi kuwa sehemu ya kukamilisha malengo ya kampuni.
Wakati mwingine mwajiri anaweza kukuweka katika mazingira fulani ya kazi ili kupima uvumilivu wako katika kukabiliana na changamoto mbalimbali pale zinapoibuka.
Unashauriwa kuyasoma mzingira unayofanyia kazi ni ya namna gani na kutafuta njia ya kuendana nayo. Kama mazingira uliyopo yanakiuka haki zako msingi unaweza kuchukua uamuzi mwingine lakini iwe hatua ya mwisho kwa sababu una nafasi kubwa ya kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
Zinazohusiana
- Hapa ndipo waombaji wa kazi hukwama wakiitwa kwenye “interview”
- Mbinu zitakazowasaidia wahitimu wa vyuo vikuu ‘kutoboa’ soko la ajira
- Haya ndiyo makosa yanayowamaliza vijana wengi wakati wa kuomba kazi
Jifunze kuwa na mawasiliano mazuri na wafanyakazi wenzako hasa unavyozungumza na kutumia vizuri mifumo ya kuposhana habari iliyowekwa na kampuni.
Uwezo ulionao wako wa kuzungumza na kuwasikiliza watu ndani na nje ya kampuni ni nyenzo muhimu sana kwani inampa mtu kujua namna ya kuwasilisha mawazo mbalimbali kwako kwa lengo la kukuza na kuendeleza biashara.
Uwezo wa kujisimamia na kusimamia wenzako ni nyenzo nyingine muhimu itakayokuhakikishia usalama wa kazi. Jifunze kutekeleza majukumu yako bila kusukumwa na kwa viwango vinavyohitajika.
Ukiweza kujisimamia mwenyewe utaweza kuwasimamia wengine ikiwa utapewa jukumu la kuwaongoza wengine pale unapokuwa umepanda cheo.
Sambamba na hilo, hutaweza kujisimamia mwenyewe kama huna uwezo wa kutatua matatizo katika kampuni. Wakati wowote changamoto inaibuka ndani ya kampuni na inakuhusu, uwe na mtazamo chanya wa kutafuta njia za kutatua ili kupata majibu.
Hii itakufanya mwajiri wako akuamini na kukupandisha cheo kuliko mfanyakazi ambaye wakati wote analalamika na hachukui hatua yoyote ya kuboresha mazingira ya kazi.
Unaweza kutimiza yote, lakini ukishindwa kutunza muda kwa kila ulifanyalo kazini, inaweza kuwachangamoto. Tunza muda hasa katika kutimiza malengo uliyowekewa. Wasilisha kazi na ripoti kwa wakati zikiwa na ubora unaotakiwa.
Wakati mwingine mwajiri anaweza kukuweka katika mazingira fulani ya kazi ili kupima uvumilivu wako katika kukabiliana na changamoto mbalimbali pale zinapoibuka. Picha| John Schnobrich/ Unsplash.
Jenga na imarisha mahusiano mazuri na mwajiri wako. Hakikisha unatii na kuheshimu uongozi na taratibu zilizopo. Hata kama kuna changamoto imetokea fuata taratibu zilizowekwa kutafuta suluhisho.
Mahusiano mazuri yatakubeba mahali pa kazi. Acha dharau kwa wafanyakzi wenzako. Fanya kazi kwa ushirikiano ili kutimiza malengo ya kampuni kwa pamoja.
Mambo hayo unaweza kujifunza mwenyewe kwa njia mbalimbali ikiwemo mtandaoni au kwa kushirikiana na wenzako kazini. Unaweza kuwa unachapakazi vizuri lakini ukipungukiwa na ujuzi huo, kazi yako inaweza kuwa mashakani.
Afisa Rasilimali Watu wa kampuni ya Shellys Phamaceticals, Hope Japhet ameiambia www.nukta.co.tz kuwa asilimia kubwa ujuzi wa mtu anapokuwa kazini ndiyo unaomwokoa na kumweka kazini kwa muda mrefu.
“Kwa asilimia kubwa kazi zinakamilishwa na jitihada zinazoenda sambamba na ujuzi. Ukimpata mtu mwenye kujituma na kujiongeza ni bora kuliko mtu mwenye CV (wasifu) nzuri,” amesema Japhet.
Latest