Maporomoko ya Kinole: Uzuri asilia wa Morogoro

March 16, 2021 11:30 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni maporomoko ya Kinole ambayo yanatajwa na wageni kuwa sehemu murua kwa ajili ya kuogelea na kufurahia mazingira.
  • Unashauriwa kufika katika ofisi za uongozi wa kijiji ili kupata mwenyeji anayeweza kukufikisha katika maporomoko hayo.
  • Hakikisha kubeba kofia na maji ya kunywa njiani kwani utalazimika kutembea kwa walau dakika 50 au zaidi.

Dar es Salaam. Mara nyingi watu huuita Mkoa wa Morogoro kama Jiji kasoro bahari huku ukipendezeshwa na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na Mwalimu Nyerere pamoja na milima ya Uruguru.

Wasichokijua ni kuwa, takribani kilometa 40 kutoka Morogoro Mjini kuelekea Kusini Mashariki mwa mkoa huo, kuna pepo ambayo haifahamiki na wengi ambayo imesheheni kila utajiri ambao macho ungetamani kuushuhudia. 

Katika pepo hiyo, tarajia maji safi ya kutosha kuakisi miale ya jua, hali ya hewa ya kusahaulisha changamoto za dunia na ukimywa ufaao kufikiria maisha huku nyimbo kutoka kwa ndege mbalimbali zikikufanya ujutie kubeba “eaphones” zako. Ni wewe na Mazingira tu.

Pepo hiyo ni maporomoko ya maji ya Kinole iliyopo katika Kijiji cha Kinole  ambayo wadau mbalimbali waliotembelea wamezitaja sifa zake kwa njia ya mtandao huku wakitaja matembezi chini ya miti, kuogelea na kufurahia uzuri wa mazingira kuwa kama vitu vya kufurahia unapoitembelea.

Maporomoko ya Kinole yaliyopo mkoani Morogoro ni kivutio kizuri cha watalii. Picha| VYmaps.com.

Kufika katika maporomoko hayo, ni mwendo wa saa mbili za kusafiri kwa gari na takriban dakika 50 za kutembea kufikia sehemu ambapo utaanza kufurahia uzuri huo asilia. 

Kama ndiyo unafika kwa mara ya kwanza, utahitaji kufika ofisi za serikali ya mtaa ili upatiwe mwenyeji wa kukutembeza ili upate kile unachokihitaji. 

Mtalii Alex kowalsky kupitia alama (tag) za ramani za Google (Google Maps) amesema ilimgharimu Sh25,000 kukamilisha utalii wake katika maporomoko hayo ambapo Sh10,000 alilipia katika ofisi za serikali za mtaa huku iliyobaki akimlipa mwenyeji wake.

“Kufika katika maporomoko hayo, nilikuwa nimeandikiwa jina la Shiringi mkononi mwangu, niliwaonyesha baadhi ya wakazi ilitosha kukutana na Shiringi,” ameandika Kowalsky aliyesisitiza umuhimu wa kufika katika uongozi wa kijiji cha Kinole.


Soma zaidi:


Ukiwa njiani kuelekea maporomoko ya Kinole, utapita katika mashamba ya ndizi, mananasi na miti ya mafenesi ambayo itakuwa inakusigeza zaidi katika uzuri wa sehemu hiyo ya utalii. 

Kufanikisha safari yako ya utalii, unashauriwa kubeba kofia kwa ajili ya kujikinga na jua, maji ya kunywa bila kusahau nguo za kuogelea.

Watu waliofanikiwa kufika eneo hilo, wamesema walifurahia matembezi yao kwa sababu kuna mambo tofauti ambayo hawayakuyaona maeneo mengine.

Katiba ratiba zako za utalii mwaka huu, umeshawishika kwenda kwenye maporomoko ya Kinole?

Enable Notifications OK No thanks