Mama Samia ahimiza uwekezaji katika teknolojia, uwajibikaji Afrika
- Amesema uwekezaji wa utafti katika sekta ya sayansi na teknolojia na kutengeneza taasisi imara za uwajibikaji ndio siri ya ukuaji wa uchumi wa bara hilo.
- Nchi za Afrika zimekuwa zikitafuta namna ya kujikwamua kiuchumi lakini bado zimendelea kukabiliwa na changamoto za uongozi.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika teknolojia, utawala wa sheria na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali asilia ili kuharakisha mageuzi ya kiuchumi katika bara hilo.
Amesema Afrika bado iko nyuma katika uendelezaji wa rasilimali zake, jambo ambalo limesababisha wananchi wake waendelee kuwa maskini.
Mama Samia aliyekuwa akihutubia mkutano wa ‘Africa Now Summit’ jana (Machi 12, 2019) katika jiji la Kampala, Uganda amesema uwekezaji wa sayansi, teknolojia na ubunifu unaweza kuleta suluhisho kwa matatizo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi katika bara la Afrika.
“Iwe maendeleo ya miundombinu au kuongeza uzalishji kwenye kilimo, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno au kushughulikia athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kutengeneza ajira, uchimbaji wa rasilimali asilia na kuongeza usafirishaji wa bidhaa zilizochakatwa, yote haya yatawezekana kama tutafanya mabadiliko kwenye sayansi na teknolojia,” amesema Mama Samia katika hotuba iliyotumwa kwa vyombo vya habari na ofisi yake.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia mkutano wa ‘Africa Now Summit’ jana (Machi 12, 2019) ambapo alisisitiza uwajibikaji, utawala wa sheria na uwekezaji katika sayansi na teknolojia. Picha| Ofisi ya Makamu wa Rais.
Amesema bado Afrika na nchi moja moja ziko nyuma sana katika kutenga bajeti ya tafiti na shughuli za maendeleo zinazochochea matumizi ya teknolojia ya kisasa ambazo zinaweza kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Ikiwa tunataka kuwa sehemu ya karne ya 21 ni lazima tuwekeze katika sayansi na teknolojia,” amesisitiza na kubainisha juhudi hizo zinapaswa zianze katika mifumo ya elimu hasa ngazi ya chini ili kuongeza usawa wa ujuzi katika fani zote.
Soma zaidi: Mama Samia kuiwakilisha Tanzania mkutano ‘Africa Now Summit’
Hata hivyo, Mama Samia ambaye pia alipata nafasi ya kutoa mada ya uongozi na mabadiliko ya kijamii na uchumi, amesema uwekezaji huo hautakuwa na maana kama misingi ya utawala bora na uwajibikaji hautazingatiwa katika matumizi ya rasilimali.
Amesema kazi kubwa iliyopo sasa ni kuimarisha taasisi za uongozi, utawala wa sheria na mijadala na mawasiliano yanayoleta tija na matumaini kwa vijana kuwa sehemu ya mageuzi ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Mama Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Rais wa Kenya William Ruto wakati wa mkutano huo unaoendelea katika hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort jijini Kampala.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na kituo cha Uongozi cha Afrika (ASLC) unafanyika kwa siku tatu na utafikia kilele chake kesho (Machi 14, 2019) na umewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo zaidi ya 1,000 ambapo wanajikita kujadili mada mbalimbali za uongozi katika kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.
Viongozi wengine wa Afrika wanaotoa mada ni pamoja na Rais wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA), Abdel Fattah el Sisi; Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa; Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Ahmed Abiy.
Latest
