Malipo ya huduma za utalii kwa kadi za kielektroniki yanaongezeka lakini…

February 27, 2019 7:27 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni asilimia 19.3 ya wageni walifanya malipo kwa njia ya kadi mwaka 2017 ukilinganisha na asilimia 15.8 mwaka 2016.
  • Malipo kwa njia ya pesa taslimu yameendelea kutawala soko la utalii nchini kwa zaidi ya asilimia 70.
  • Wadau wa sekta ya utalii wamesema hali hiyo inachangiwa na kutokuimarika kwa mifumo ya malipo ya kadi, uhamasishaji mdogo na changamoto za ulipaji kodi.

Dar es Salaam. Licha ya matumizi ya kadi za malipo za kielektroniki (Credit Cards) katika huduma za utalii kuongezeka mwaka hadi mwaka, bado kiwango cha matumizi ya mifumo hiyo ya malipo hayaridhishi jambo linaloweza kupunguza kasi ya Serikali katika ukusanyaji mapato ya kodi na usalama wa watalii kwa kubeba maburungutu ya fedha taslimu. 

Kadi za malipo ni zile zilizounganishwa na mifumo ya kibenki duniani zikiwemo ‘Mastercard’ na ‘Visa card’ ambazo mtu anaweza kulipia huduma au bidhaa bila kuhitaji pesa taslimu ikiwa sehemu yoyote inayokubali malipo hayo. 

Ripoti ya utafiti ya wageni wa nje ya nchi (International Visitors’ Exit Survey Report 2017) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la wageni wanaotumia kadi za malipo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo hadi kufikia 2017, asilimia 19.3 ya wageni walitumia kadi ukilinganisha na asilimia 15.8 ya mwaka 2016. 

Kiwango hicho ni cha juu zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo kiwango cha juu kuwahi kurekodiwa kilikuwa mwaka 2015 cha asilimia 18.6 kabla ya kushuka kidogo katika mwaka uliofuata. 

Ripoti hiyo imebainisha kuwa kiwango cha matumizi ya kadi siyo cha kuridhisha kwa sababu malipo ya huduma za utalii yametawaliwa zaidi na pesa taslimu ambapo mwaka 2017 pekee asilimia 73 ya wageni walitumia pesa taslimu. 

Hii ina maana kuwa kwa kila wageni 10 basi saba wanatumia pesa taslimu kufanya malipo huku wawili tu wakitumia kadi.

“Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa kutokubalika kwa kadi za malipo katika maeneo mengi ya utalii kumeendelea kuwa tatizo,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Licha ya malipo ya fedha taslimu kutawala soko la utalii, bado matumaini ya ongezeko la matumizi ya kadi yapo ikizingatiwa kuwa idadi ya watumiaji inaongezeka taratibu. 

Hata hivyo, ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni haijaeleza ni watalii wangapi wanatumia huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi ambazo zimejipatia muitikio mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na usalama na urahisi wa kutumia.

Baadhi ya wadau wa utalii nchini wameiambia Nukta kuwa matumizi yasiyoridhisha ya kadi za malipo yanatokana na kutokuwepo kwa mifumo ya kisasa katika maeneo mengi hasa katika maduka ya vifaa vya utalii iliyounganishwa na huduma za kimataifa za malipo. 

Muungozaji wa watalii, Makarious Judica amesema changamoto nyingine ya matumizi yasiyoridhisha ya kadi za malipo ni uhamasishaji mdogo wa teknolojia hiyo hasa kwa watoa huduma za utalii na kusababisha wageni kubeba pesa kwenye mabegi ili kuendana na mazingira yaliyopo. 

“Wageni wanakuja na mitazamo tofauti Afrika yaani watu kutoka Ulaya wanahisi wanaenda shimoni hawana hisia kwamba wakifika hapa mifumo ipo na wanaweza wakatumia.

“Lakini mifumo yenyewe iko chini sana, anaweza akafanya hivyo mgeni anayekuja mara ya pili au ya tatu baada ya kwamba amezoea kidogo mazingira,” amesema Judica. 


 Zinazohusiana: 


Ukwepaji kodi inaweza kuwa sababu nyingine kwa watu kutotumia mifumo ya kadi za malipo ambazo zinaiwezesha Serikali kupata kodi kirahisi ikilinganishwa na pesa taslimu. 

“Watoa huduma wa Tanzania hatusisitizi sana matumizi ya ‘credit card’ sijui lakini sababu kubwa huenda ni tabia za ukwepaji kodi na mambo madogo madogo,” amesema.

Mwaka 2016 Serikali ilifanya mabadiliko katika Sheria ya Kodi ya mwaka 2004 na kuanzisha kodi mpya ya ongezeko la thamani (VAT) ya asilimia 18 katika huduma za utalii. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kuna haja ya kuwashawishi wamiliki wa kampuni za utalii na wadau wengine umuhimu na manufaa ya kuwaruhusu wageni kutumia kadi kufanya malipo wakati wakipata huduma. 

Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Catherine Mbena ameiambia Nukta kuwa kwa kutambua umuhimu wa malipo kwa njia ya kadi, mamlaka hiyo hairuhusu malipo ya pesa taslimu badala yake wageni na watalii wanaotumia huduma zao hulipa kwa kutumia kadi na simu za mkononi kama TigoPesa, M-Pesa na Airtel Money. 

Malipo ya kadi yanasaidia kuongeza usalama wa mtu na pesa zake na kumuepusha kubeba fedha nyingi kwenye mfuko ambapo anaweza kujiweka katika hatari ya kuibiwa au kuvamiwa na wahalifu. 

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
21 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
21 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
21 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Nukta TV

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Nukta TV

FAHAMU KUHUSU SIKOSELI | Part 1: Ugonjwa wa kurithi, unaotesa maelfu ya watoto Tanzania

FAHAMU KUHUSU SIKOSELI | Part 1: Ugonjwa wa kurithi, unaotesa maelfu ya watoto Tanzania

Nukta TV