Makosa ya kuepuka wakati wa kusajili kampuni, jina la biashara

October 10, 2020 5:55 am · Hamza Yusuph
Share
Tweet
Copy Link
  • Usajili unatakiwa kufanywa na mtu ambaye ana weledi wa kutosha kwenye masuala ya sheria.
  • Kusoma kwa makini nyaraka za kampuni kabla ya kusaini.
  • Taarifa za Wakurugenzi ziwe wazi na zipatikane kwa urahisi wakati wa usajili wa kampuni husika.

Usajili wa kampuni au jina la biashara kwa siku za karibuni umekua ukifanyika mtandaoni kwa kutumia mfumo unaoitwa BRELA ORS.

Ili mtu aweze kusajili kampuni au jina la biashara anapaswa kuwa na akaunti maalumu kwenye mtandao huo ulio chini ya Wakala wa Usajili na Utoaji wa Leseni za Biashara (BRELA).

Uwepo wa nyenzo hii umesaidia zoezi la usajili kufanyika kwa urahisi na haraka, jambo lilopunguza urasimu

Kwa jicho lingine imesababisha uwepo wa vishoka wengi ambao wamekua wakiharibu taswira zima ya zoezi la usajili wa kampuni au jina la biashara.

Kuepusha shida wakati wa usajili na kupunguza kesi za jinai kwa wamiliki wa makampuni au majina ya biashara kuna mambo kadhaa ambayo wamiliki wa makampuni au majina ya biashara wanapaswa kuyazingatia.

    1. USAJILI KUFANYWA NA MTU MWENYE WELEDI

Usajili wa kampuni ni suala nyeti, hivyo basi unatakiwa kufanywa na mtu ambaye ana weledi wa kutosha kwenye masuala ya sheria zinazosimamia masuala ya kampuni na usajili wa majina ya biashara. 

Ni vyema usajili ukafanywa na wakili ambaye yuko thabiti na imara kwenye masuala ya sheria za makampuni ili kuondoa sintofahamu mbalimbali yanapokuja masuala ya kisheria juu ya kampuni husika.

Wakili huyu anakua anabanwa vilivyo na miiko ya kisheria ya ufanyaji wake kazi na kumfanya afanye kazi kwa weledi.


    2. KUSOMA NYARAKA (MEMART) KABLA YA KUSAINI

Wamiliki wengi wakishatoa kazi ya kusajili kampuni hawafuatilii kujua nini tena kinaendelea zaidi ya kuwa watia saini tu. Ni vyema kuisoma “memart” kwa sababu ndiyo injini kuu wakati wa uundwaji wa kampuni husika. 

Memarts inaonyesha kila kitu kuhusu kampuni kama:

  1. Lengo na shughuli za kampuni
  2. Jina La kampuni
  3. Wanachama wa kampuni
  4. Hisa na mengineyo

Kusoma na kuelewa kilichomo kwenye memarts kinasaidia kuondoa matatizo baaada ya usajili wa kampuni kufanyika.


Soma zaidi:


     3. KUWA NA TAARIFA ZA WAKURUGENZI

Taarifa za wakurugenzi wa kampuni ni taarifa za awali wakati wa usajili wa kampuni. Hivyo basi lazima ziwe wazi na zipatikane kwa urahisi wakati wa usajili wa kampuni husika. 

Ni vyema mmiliki atambue kuwa wakurugenzi lazima wawe na vitambulisho vya utaifa kama ni Watanzania na pasi za kusafiria (passport) kama ni raia wa kigeni. Hii itasaidia kuondosha uwepo wa makosa ya jinai juu ya kampuni husika.

    4. KUSOMA ‘CONSOLIDATED FORM’ 

Hii ni nyaraka muhimu ya awali baada ya kuanza kusajiliwa kwa kampuni. Nyaraka hii inaonyesha taarifa zifuatazo:

  1. Jina la kampuni
  2. Majina ya wanachama wa kampuni
  3. Shughuli za kampuni na anuani ya kampuni
  4. Wakurugenzi wa kampuni na katibu wa kampuni

Hivyo basi mmiliki anapaswa kuisoma nyaraka hii ili kujiridhisha kama wanachama waliopo ni sahihi na wametia saini zao na pia kuweza kutambua kama katibu wa kampuni ni yule ambaye ameidhinishwa kwa ajili ya kampuni husika.

Hivi ni baadhi ya vitu muhimu ambavyo wamiliki wa makampuni wanatakiwa kuvizingatia kabla na wakati wa usajili wa kampuni au jina la biashara.


Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule,

Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini

Kwa msaada wa kisheria wasiliana nami kupitiaTwiter@Hamzaalbhanj

Mob; 0717521700

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...