Majaliwa aondoa utata ujenzi ofisi halmashauri ya Kigoma

September 17, 2021 11:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Aagiza mapendekezo ya wananchi yahishimiwe.
  • Jengo la ofisi hiyo imepangwa kujengwa kata ya Mahembe.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ihakikishe inasimamia ujenzi wa majengo ya ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma unafanyika katika Kata ya Mahembe kama ilivyopendekezwa katika vikao vya Baraza la Madiwani si katika Kata ya Kamala inayopendekezwa na watalamu.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Septemba 17, 2021 mara baada ya kusimamishwa na wakazi wa Kata ya Mahembe  ambao wamedai  maamuzi ya madiwani yamebadilishwa ambapo amesisitiza kuwa kama sababu ni eneo kutofaa kwa ujenzi wa majengo ya ghorofa wabadilishe ramani Ili yajengwe majengo ya kawaida.

Wananchi hao ambao wamewasilisha malalamiko yao kupitia mabango wamemueleza Waziri Mkuu kuwa hawaridhishwi na maamuzi ya Serikali ya kuhamishia ujenzi wa ofisi za halmashauri katika Kata ya Kamala wakati Baraza la Madiwani lilishatoa maamuzi kupitia vikao rasmi.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Waziri Mkuu amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchata atoe ufafanuzi juu la suala hilo ambapo kiongozi huyo amekiri kuwa ni kweli ujenzi ulipendekezwa ufanyike katika eneo hilo ila uamuzi wa kubadilisha ulitokana na ushauri wa wataalamu ambao walisema eneo hilo halifai kujengwa majengo ya ghorofa kama ramani inavyoonesha.

“Kama eneo hili halifai kujengwa ghorofa ni lazima mjenge majengo ya ghorofa? Wananchi wanahitaji majengo ya kutolea huduma. Unajua maamuzi ya eneo la ujenzi yameamuliwa na wananchi kupitia Baraza la Madiwani, hivyo yazingatiwe huko msiende kujenga,” amesisitiza Majaliwa.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahembe alisema baada ya kupeka taarifa kwamba eneo lao limechaguliwa kujengwa ofisi za halmashauri walitoa bure eneo la ukubwa wa ekari 25 kwa Serikali ili liweze kutumia kwa ajili ya ujenzi huo.

Wakati wakisubiri ofisi hizo zijengwe, wakazi wa kijiji hicho walitoa majengo ya shule ya msingi yatumike kama ofisi na wao kuamua kujenga shule nyingine, hivyo wanashangazwa na taarifa za kuhamishwa kwa makao makuu ya halmashauri yao.

Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Assa Makanika amesema Baraza la Madiwani lilipendekeza kuwa ujenzi wa jengo la halmashauri lijengwe katika eneo hilo na ameshangaa kusikia ujenzi huo ukihamishiwa katika eneo lingine, ameomba maombi ya wananchi yasikilizwe.

Pia, Diwani wa Kata ya Mahembe, Mamisho Seif amesema Baraza la Madiwani lilifanya vikao na kupiga kura kuamua eneo ambalo zitajengwa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambapo kata ya Mahembe ilichaguliwa kati ya kata sita zilizopendekezwa.

“Jambo la kusikitisha ni kitendo cha wataalamu kufanya mabadiliko ya eneo la ujenzi na kuhamishia katika Kata ya Kamala. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba maamuzi ya Baraza la Madiwani yafuatwe,” amesema Seif.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW