Kiwanja cha ndege kilichojengwa na wakoloni kupanuliwa- Kwandikwa
- Ni kiwanja cha ndege cha Njombe kilijengwa na wakoloni kabla ya uhuru miaka ya 1940 na kuanza kutumika rasmi mwaka 1945.
- Taratibu zote za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umefanyika na kinachosubiriwa ni fedha za kukarabati na kupanua uwanja huo.
- Utasaidia kufungua milango kwa wananchi kufaidika na fursa mbalimbali za uzalishaji, biashara na usafiri wa anga.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwaamesema Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta pesa za ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Njombe ili kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazowanufaisha wananchi wa mkoa huo.
Ukarabati huo pia utahusisha viwanja vya ndege vya Iringa, Songea, Lindi, Kilwa Masoko, Tanga, Moshi, Ziwa Manyara, Singida, Musoma na ujenzi wa kiwanja kipya cha mkoa wa Simiyu.
Kwandikwa ametoa maelezo hayo bungeni leo (Februari 6, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), LucyMlowe ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuuendeleza au kuhamisha uwanja huo ambao umekuwa kero kwa wananchi kwasababu uko katikati ya mji na haujakarabatiwa kwa muda mrefu.
Akijibu swali hilo, Kwandikwa amesema kwa sasa Serikali haina mpango wa kuhamisha uwanja huo kwa sababu taratibu zote zaupembuzi yakinifu na usanifu wa kina umefanyika na kinachosubiriwa ni fedha za kukarabati na kupanua uwanja huo.
“Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika kwa viwanja hivyo ambapo taarifa ya mwisho iliwasilishwa Machi 28, 2017. Hatua iliyopo kwa sasa ni utafutaji fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho,” amesema Kwandikwa.
Amesema kiwanja cha ndege cha Njombe kilijengwa na wakoloni kabla ya uhuru miaka ya 1940 na kuanza kutumika rasmi mwaka 1945. Miaka hiyo mji wa Njombe ulikuwa mdogo sana na hivyo kiwanja kilikuwa mbali na makazi ya watu.
Upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Njombe utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Picha| K-VIS.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za usalama wa anga, hairuhusiwi watu, wanyama, magari kufanya shughuli zozote kwenye viwanja vyote vya ndege.
“Kwa mantiki hiyo vitendo vya baadhi ya wananchi wa maeneo hayo kukatiza katika kiwanja hicho ni vya uvunjifu wa sheria na ndiyo maana wananchi hao hukamatwa na kutozwa faini au kuadhibiwa,” amesema.
Kupatikana kwa fedha hizo za upanuzi wa kiwanja hicho pia utahusisha ujenzi wa uzio kuzunguka eneo lote la kiwanja kudhibiti wananchi wanaokatisha kiwanjani hapo kinyume cha taratibu.
Zinazohusiana:
- Fastjet yafanya mabadiliko makubwa huduma za vyakula, mizigo
- Mkimbizi wa zamani wa Afghan azunguka Dunia kwa ndege
Kukamilika kwa upanuzi wa kiwanja hicho kutachochea shughuli za kiuchumi ikiwemo usafiri wa anga, uzalishaji na biashara ya bidhaa katika mkoa huo ambapo Serikali iko katika mazungumzo na kampuni ya Sichuan Hongda Group Limited(SHG) ya China kuangalia namna ya utekelezaji wa mradi wa uzalishaji wa chuma –Liganga na Mchuchuma.
Tanzania inatarajia kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa chuma barani Afrika kwa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka.